KUMBUKUMBU YA ASHURA NI KATIKA NEMBO ZA ALLAH.


Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, nchini Tanzania kumefanyika halfa kubwa za Taasua (Tisa Muharram) na Ashura (10 Muharram) katika kukumbuka kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW, Imam Hussein AS na wafuasi wake 72 watiifu katika jangwa la Karbala. Maelfu ya Waislamu walishiriki katika maombolezo hayo.

Moja ya hafla hizo ni ile iliyofanyika katika Madrassah ya Al Hudaa ambapo mwambata wa utamaduni wa Iran nchini Tanzania Ali Baqeri alihutubu na kusema Imam Hussein AS alikuwa shujaa ambaye hadi lahadha ya mwisho alipipamana kwa ajili ya Tauhidi na kumuabudu Mwenyezi Mungu. Aidha mjini Dar es Salaam kulifanyia matembezi (masir) katika siku ya Taasua ambayo yaliwashirikisha watu wa matabaka mbali mbali katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi hadi katika Msikiti wa Jamia ywa Khoja Shia Ithnaashari. Viongozi wa Kishia na Kisunni walishiriki katika mjumuiko huo akiwemo Shehe Mkuu wa Dar es Salaam Sheikh Mussa Salim Al Hadi. Akihutubu katika kikao hicho, Sheikh Hadi alisema: 'Ashura ni kati ya Siku za Allah na ni siku ya huzunu kwa Waislamu na Uislamu. Ashura haina madhehebu maalumu na ni ya Waislamu wote." Aidha aliashiria nafasi maalumu ya Bibi Fatima Zahra SA na Imam Ali AS mbele ya Mtume SAW na kusema: "Hussein AS alikuwa mjukuu wa Mtume SAW na aliuawa shahidi kidhalimu huko Karbala." Sheikh al Hadi amekumbusha kuwa Mtume SAW alisema: "Mwenye kumpenda Al Hassan na Al Hussein amenipenda na mwenye kuwachukia amenichukia."
http://iqna.ir/sw/news/3470614/kumbukumbu-ya-ashura-ni-katika-nembo-za-allah

KISOMO CHA DUA KWA AJILI YA MAMA HAJRAH (Mke wa Al Hajj Mputa).

Dua imefanyika nyumbani kwa marehemu Chanika jijini Dar es Salaam, Wanaharakati wa dini ya Kiislamu wamejuika pamoja na mwanaharakati mwenzao ndugu Al Hajj Mputa katika kisomo cha Qur'ani Tukufu na kumfariji.

Tusome Suratul Fatha kwa ajili ya marehemu waliyotutangulia mbele ya haki.

25/09/2016

PICHA ZA MAZISHI YA MAMA HAJRAH (Mke wa Al Hajj Mputa)
Picha za mazishi ya mke wa Mwanaharakati ndugu Al Hajj Mputa, yaliofanyika Kisarawe jijini Dar es Salaam wiki hii.
Mwenyezi Mungu alifanye kaburi laka liwe viwanja katika viwanja vya peponi.
Hakika sisi sote ni waja wa Mwenyezi Mungu na kwake ni marejeo."

14/09/2016

WANIGERIA WATAKA KUACHILIWA HURU SHEIKH ZAKZAKY.

Wananchi wa Nigeria wameandamana na kutoa wito wa kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Kanali ya Press TV inaripoti kwamba, wakazi wa mji wa Abuja nchini Nigeria jana walifanya maandamano, ambapo mbali na kulalamikia vitendo vya utumiaji mabavu na mashinikizo ya serikali dhidi ya Waislamu wametaka kuachiliwa huru mara moja, Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa kizuizini kwa miezi kadhaa sasa.
Waandamanaji hao walisikika wakipiga nara za kukemea vikali utumiaji mabavu na mauaji ya vikosi vya usalama vya Nigeria dhidi ya Waislamu katika mji wa Zaria miezi kadhaa iliyopita.

Maandamano ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Waandamanaji hao wametia saini barua ambayo wameituma kwa Kamisheni ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini humo wakitaka kuachiliwa huru mwanazuoni huyo wa Kiislamu.
Ripoti zinasema kuwa, hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky kizuizini ni mbaya. Pamoja na hayo, serikali ya Nigeria imekataa kumuachilia huru alimu huyo wa Kiislamu.
Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, jicho la kushoto  la Sheikh Zakzaky limepofuka na kwamba maafisa usalama wamekuwa wakikataa mwanazuoni huyo wa Kiislamu kupatiwa matibabu.
Wananchi wa Nigeria wamekuwa wakiandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kuachiwa huru haraka kiongozi huyo wa Kiislamu.

Jeshi la Nigeria lilipowashambulia Waislamu mjini Zaria Disemba 2015
Itakumbukwa kuwa Disemba mwaka jana askari wa jeshi la Nigeria walishambulia marasimu ya kidini ya Waislamu wa Kishia katika mji wa Zaria kwa kuwatuhumu kuwa walizuia msafara wa mkuu wa jeshi na pia kujaribu kumuua, madai ambayo yalikanushwa na Waislamu hao. (parstoda)

ROUHANI: SAUDIA INATUMIKIA MASLAHI YA ISRAEL KWA KUWAZUIA MAHUJAJI WAIRANI.
Rais Hassan Rouhani wa Iran amelaani hatua ya Saudia kuwazuia Wairani kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu na kusema hatua hiyo ni kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akizungumza Jumatatu katika mkoa wa Azarbaijan Magharibi, Rais Rouhani amesema ibada ya Hija na miji mitakatifu ya Makka na Madina ni ya Waislamu wote na kwamba Ibada ya Hija ni sehemu ya kutekelezwa matakwa ya Umma wa Kiislamu.
Ameongeza kuwa wale wanaodai kuwa eti ni wahudumu wa Misikiti Miwili Mitakatifu wanatekeleza hatua ya kitoto ya kuzuia Njia ya Mwenyezi Mungu na Hijja huku wakieneza machafuko katika eneo, na yote hayo ni kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Siku ya Jumapili Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran alisema njama na vizingiti vya Saudia ni jambo ambalo limewazuia Wairani kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu.
Naye Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara za Kidini la Iran Saeed Ohadi amebainisha sababu ambazo zimepelekea Mahujaji Wairani washindwe kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu. Amebaini kuwa Wasaudi wamepiga marufuku kuwekwa bendera ya Iran katika majengo ya Mahujaji Wairani. Aidha wameweka vizingiti kuhusu idadi ya zahanati za Iran katika msimu wa Hija sambamba na kuzuia madawa yanayotumiwa na Mahujaji Wairani. Aidha amesema Wasaudi wamekataa ushanga wa mkononi wa kielektroniki ambao Iran ilikuwa imetengeneza kwa ajili ya kuwatambulisha Mahujaji wake huku wakisema watatengeneza ushanga ambao watawalazimisha Wairani kuuvaa. Ohadi amesema Wasaudi pia wamepiga marufuku baadhi ya hafla za Mahujaji Wairani jambo ambalo Iran haikulikubali. Afisa huyo wa Hija wa Iran pia amesema Saudi Arabia inawadhalilisha Wairani kisiasa na hata wakati wa mazungumzo kuhusu Hija Wasaudi walionyesha muamala mbovu sana. Mkuu wa Shirika la Hija la Iran pia amesema maafisa wa Saudia kwa kawaida huvunjia heshima nakala za Qur’ani zilizochapishwa nchini Iran na kuwapokonya Mahujaji Wairani nakala hizo za Qur’ani huku wakizirusha huku na kule kwa madharau.

BILAL MUSLIM MISSION OF TANZANIA YAFANYA ZIARA MKOA WA TANGA WILAYA YA LUSHOTO.Taasisi ya Bilal Muslim Mission imefanya ziara katika mkoa wa Tanga wilaya ya Lushoto, imeendesha Semina kwa Wanaharakati wa wilaya hiyo huku wakiwata kujitolea zaidi katika mambo mbalimbali na kushikamana na visomo vya dua ili kuondokana na matatizo ya maradhi pamoja na umasikini katika Semina hiyo wametoa mafunzo kwa vitendo na kuonesha namna wanavyofanya kazi zao katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania.

MATAKFIRI WAVAMIA MSIKITI MWANZA, TANZANIA NA KUFANYA MAUAJI
 Watu wanaodhaniwa kuwa ni wakufurishaji wamevamia msikiti wa ‘Masjid Rahma’ mkoani Mwanza, Tanzania na kufanya mauaji.

Kwa mujibu wa mashuhuda mauaji hayo yalitokea jana usiku kwenye msikiti huo uliopo eneo la Ibanda Relini, kata ya Mkolani wilayani Nyamagana. Habari zaidi zinasema kuwa, kundi la watu wanaokadiriwa kama 15 na ambao walikuwa wamejifunika nyuso zao, waliwavamia Waislamu waliokuwa wakisali sala ya Isha ndani ya msikiti huo na kuanza kuwakatakata kwa mapanga. Miongoni mwa watu waliouawa katika hujuma hiyo ni pamoja na imamu wa msikiti huo, Ferouz Elias, Mbwana Rajab na Khamis Mponda ambaye ni dereva wa bodaboda. Aidha watu wengine walijeruhiwa katika tukio hilo. Mashuhuda wameeleza zaidi kuwa, wakati waumini hao walipokuwa wakiendelea na ibada ya Sala, ghafla kundi la watu hao waliingia msikitini hapo na kuanza kuhoji kwamba, ni kwanini walikuwa wanaswali ilhali wenzao wamekamatwa na kuendelea kushikiliwa na polisi, kauli ambayo iliendana na mashambulizi hayo. Habari zaidi zinasema kuwa, washambuliaji hao walikuwa na bunduki aina ya SMG pamoja na mabomu ya kutengeneza ambapo baada ya tukio hilo walirusha mabomu hayo lakini hayakuleta madhara yoyote.
Kufuatia hujuma hiyo, Shekh Hussein Ibrahim, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Nyamagana mbali na kulaani kitendo hicho, amesema vitendo vya namna hiyo havikubaliki katika Dini ya Kiislamu na kwamba, Waislamu wote wanapaswa kulaani matukio ya namna hiyo. Inafaa kuashiria kuwa, kwa muda mrefu kumekuwepo ugomvi kati ya waumini wa msikiti wa Rahma ambao ni wa Waislamu wa Kisuni na wale wa Kiwahabi, ugomvi ambao ulipelekea hivi karibuni polisi ya Mwanza kuwatia mbaroni vinara wa Kiwahabi.