LENGO LA VITA DHIDI YA SYRIA NI KUILINDA ISRAEL.


Kamanda wa Jeshi la Kujitolea Iran, Basiji, amesema kuwa, vita vya Marekani dhidi ya Syria ni sehemu ya siasa za kupenda vita za Marekani zenye lengo la kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel. Brigedia Jenerali Mohammad-Reza Naqdiameeleza kwamba lengo si kupambana na ugaidi au silaha za kemikali bali lengo la Marekani ni kutawala, ukandamizaji na kuulinda utawala ghasibu za Kizayuni.

Wakati huo huo,  huku Marekani ikiendelea kupiga ngoma za vita dhidi ya Syria,  Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa na Kamati ya Siasa za Nje ya Bunge la Iran ametahadharisha juu ya taathira mbaya ya nchi za kigeni kuingilia kijeshi Syria. Alaeddin Boroujerdi amesema hayo katika mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Syria Mohammad Jihad al-Laham na kuongeza kwamba mashambulizi yoyote dhidi ya Syria yatapanuka hadi nje ya mipaka ya nchi hiyo.


Wanamgambo waliohojiwa 
wamedai kuwa Saudi Arabia haikuwafahamisha kuwa silaha hizo ni za kemikali wala hawakupokea maelezo kuhusu namna ya kuzitumia. Wanamgambo hao wanawatuhumu magaidi Mawahabi wakufurishaji kutoka kundi linalojiita an-Nusra ambalo linafungamana na al-Qaeda, kuwa waliwatumia vibaya wapiganaji wengine na kuwapa silaha za kemikali pasina kuwapa maelezo. Aidha wanamgambo wengi waliohojiwa wanasema wao hupokea mishahara kutoka serikali ya Saudia. Wamesema mkuu wa shirika la kijasusi Saudia amepewa lakabu ya al-Habib , yaani kipenzi, na wapiganaji wa al-Qaeda wanaoipiga vita serikali ya Syria. Hii ni kwa sababu amekuwa akiwapa misaada kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Syria. Ikumbuwke kuwa Saudi Arabia ni muitifaki mkubwa wa Marekani na Bandar bin Sultan aliwahi kuwa balozi wa Saudia nchini Marekani kwa zaidi ya miaka 20.

Rais Barack Obama wa Marekani ambaye kwa muda wa wiki sasa amekuwa akipiga ngoma ya vita dhidi ya Syria, anaonekana kulegeza msimamo kuhusiana na kadhia hiyo. Licha ya Obama kusema kwamba, shambulio la silaha za kemikali nchini Syria ni tishio kwa Marekani na washirika wake, lakini pamoja na hayo amesema kwamba, uingiliaji wa kijeshi wa Washington nchini Syria unapaswa kupata idhini na ridhaa ya Kongresi ya nchi hiyo. Obama amesema kama ninavyomnukuu, "licha ya kuwa mimi ni Rais wa Marekani na nina uwezo wa kutoa idhini ya kufanywa shambulio la kijeshi, lakini naitaka Kongresi ichukue uamuzi kuhusiana na hili" mwisho wa kunukuu. Rais wa Marekani ametangaza kwamba, nchi yake ni lazima iingilie kijeshi suala la Syria. Obama ameashiria kwamba, shambulio la kijeshi dhidi ya Syria linaweza kufanywa kesho, wiki ijayo au mwezi ujao na kuongeza kwamba, nchi yake ni Marekani na kwamba, haiko tayari kufumbia macho kile kinachojiri nchini Syria. Obama amebainisha kwamba, amefanya mazungumzo na viongozi wa Demokrast na Repulican na kwamba, viongozi hao wametangaza kukubaliana na shambulio la kijeshi la Washington dhidi ya Syria.

Inaonekana kuwa, hatua ya Rais Obama ya kulegeza msimamo ina mfungamano na matukio ya hivi karibuni kieneo na kimataifa. Ukweli wa mambo ni kwamba, Obama amejikuta yuko peke yake baada ya kushindwa kupata idhini ya jamii ya kimataifa kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuishambulia kijeshi Syria. Hadi sasa rasimu tatu za maazimio yaliyopendekezwa na Wamagharibi na waitifaki wao kwa ajili ya kuishinikiza Syria zimegonga mwamba katika Baraza la Usalama baada ya kupigiwa kura ya veto. Pigo la hivi karibuni kabisa la Wamagharibi katika uwanja huo ni kukwama pendekezo la Uingereza lililowasilishwa katika Baraza la Usalama la kutaka idhini ya kuishambulia kijeshi Syria. Baada ya Uingereza kujiweka pembeni, Marekani imebakia na mshirika mmoja tu yaani Ufaransa katika propanga za kupigia upatu shambulio la kijeshi dhidi ya Syria. Hata hivyo Ufaransa nayo mambo yake hayako shwari sana hasa kutokana na kuwa, kuna wimbi kubwa la upinzani nchini humo ambalo halitaki kuiona Paris ikishirikiana na Washington katika shambulio la kijeshi dhidi ya Syria. Vyombo vya habari nchini Ufaransa vinamtaja Rais Francois Hollande wa nchi hiyo kwamba, ndiye swahiba na mshirika pekee wa Marekani  barani Ulaya katika kupiga ngoma ya vita dhidi ya Syria. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, matukio haya ndio yaliyomfanya Rais Obama afikirie mara mbilili hasa baada ya kujiona  kwamba, kwa namna fulani amebakia peke yake katika kadhia ya kutaka kuishambulia kijeshi Syria. Pamoja na hayo, Obama hataki kuubeba peke yake mzigo mzito wa kuishambulia kijeshi Syria. Mbali na kuachwa mkono na washirika wake katika kuishambulia kijeshi Syria, Obama anakabiliwa pia  na upinzani mkali wa fikra za waliowengi ndani ya Marekani. Kwani kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni zaidi ya asilimia 60 ya Wamarekani wanapinga nchi yao kuishambulia kijeshi Syria. Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, hatua ya Obama ya kuacha kutumia mamlaka aliyonayo kikatiba ya kutoa idhini ya kushambuliwa kijeshi Syria na badala yake kutaka Kongresi ya nchi hiyo ichukue uamuzi wa hilo, ni hila na ujanja wa kisiasa ambao lengo lake ni kutaka kupata himaya ya Kongresi kuhusiana na hilo hasa kwa kutilia maanani kwamba, Kongresi ya Marekani itaunga mkono kushambuliwa kijeshi Syria.

 Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wanatajiwa kukutana katika mji mkuu wa Misri Cairo ili kujadili mgogoro wa Syria. Ahmed Bin Hilli Naibu Katibu Mkuu wa Arab League amesema, ajenda ya mkutano huo ni kuangazia mageuzi yanayojiri kwa haraka nchini Syria na kwamba kikao hicho kimeitishwa na nchi kadhaa za Kiarabu. Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Jumanne iliituhumu serikali ya Syria kuwa eti imefanya shambulizo la silaha za kemikali pambizoni mwa mji mkuu Damascus tarehe 21 Agosti. Huko nyuma pia jumuiya hiyo ilisimamisha kwa muda uanachama wa Syria kwa madai kwamba serikali ya Rais Bashar la Assad imeshindwa kushikamana na mpango wa amani wa Kiarabu uliokuwa na lengo la kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo.
Hata hivyo baadhi ya nchi wanachama wa Arab League kama vile Misri, Iraq, Lebanon, Tunisia na Algeria zinapinga nchi za kigeni kuingilia kijeshi mgogoro wa Syria. 

Kamanda 
wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran (IRGC) Meja Jenerali Mohammad Ali Ja'afari amonya kuhusu natija mbaya ya hujuma yoyote ya Marekani dhidi ya Syria.
Ametahadharisha kuwa iwapo Marekani itaishambulia Syria, basi athari mbaya za hujuma hiyo zitaenea katika eneo lote la Mashariki ya Kati. Meja Jenerali Ja'afari ameishauri Marekani ipate funzo kutoka masaibu yake huko Afghanistan na Iraq. Ameongeza kuwa kama ambavyo uingiliaji wa Marekani katika ulimwengu wa Kiislamu umepelekea kuenea misimamo mikali, machafuko na ugaidi, kuishambulia Syria hakutakuwa na natija ghairi ya kueneza misimamo mikali.
Wakati huo huo Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo Iran Ayatollah Hashemi Rafsanjani naye pia ameonya kuwa Marekani na waitifaki wake wakianzisha vita Syria yamkini wasiweze kumaliza vita hivyo kwani vitatoka nje ya udhibiti wao. Amesisitiza umuhimu wa Syria katika eneo na kusema nchi hiyo ya Kiarabu ni ngome ya mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Kwingineko wabunge kadhaa wa Iran wako nchini  Syria kwa lengo la kufanya mazungumzo na wakuu wa nchi hiyo. Ujumbe huo uliowasili Damascus Jumamosi unaongozwa na mkuu wa Kamati ya Sera za Kigeni na Usalama wa Taifa katika bunge la Iran Bw. Allaudin Burujerdi.

Rais Barack Obama wa Marekani ameendelea kutengwa kimataifa katika ngoma zake za vita dhidi ya Syria lakini amesisitiza kuendeleza mpango wake wa kuishambulia kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu. Akizungumza Jumamosi mjini Washington, Obama alionekana kulegeza msimamo kidogo na kusema ataomba idhini ya Bunge la Kongress kabla ya kuingia vitani Syria. Bunge hilo linatarajiwa kurejea kutoka likizoni Septemba tisa ili kujadili kadhia ya uvamizi wa kijeshi Syria. Obama hatahivyo hakubainisha wazi iwapo atatumia uwezo wake kama amri jeshi mkuu kuishambulia Syria iwapo Kongress itapinga wito wake wa vita. Obama anapiga ngoma hizo za vita huku uchunguzi wa maoni ukionyesha kuwa asilimia 60 ya Wamarekani wanapinga vita dhidi ya Syria. Aidha maandamano ya kupinga vita Syria yanaendelea kote duniani huku waitifaki wa karibu wa Marekani kama vile Uingereza, Ujerumani, Canada na Italia wakisema hawatajihusisha na hujuma ya kijeshi dhidi ya Syria. Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wamemaliza uchunguzi wao kuhusu matumizi ya silaha za kemikali Syria na wamesema matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa kabla ya wiki mbili. Serikali ya Syria imekanusha vikali madai ya kutumia silaha za kemikali na kusema magaidi wanaopata himaya ya nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za eneo ndio waliotumia silaha hizo za sumu. Naye Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa, tuhuma za utumiwaji silaha za kemikali zinazoelekezwa kwa serikali ya Syria, ni upuuzi mtupu. Chanzo cha habari
http://kiswahili.irib.ir/habari