NJAMA ZA WAZAYUNI DHIDI YA MASJDUL AQSWA.


Taasisi ya Waqfu na Turathi za Kiutamaduni ya al-Aqswa huko Palestina, imetahadharisha kuhusiana na njama mpya za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Masjdul Aqswa. Taarifa ya taasisi hiyo ya kiutamaduni imebainisha kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umeanzisha njama mpya za kuchimba mashimo mapya na kutaka kuanzisha njia za chini kwa chini katika msikiti mtakatifu wa al-Aqswa lengo likiwa ni kulibomoa eneo hilo takatifu. Taasisi ya Waqfu na Turathi za Kiutamaduni ya al-Aqswa huko Palestina imetahadharisha kuhusiana na matokeo mabaya na hatari yatakayosababishwa na mashimo hayo na kusisitiza kwamba, hatua hizo zitapelekea misingi ya kuta za msikiti huo kutetereka. Hivi karibuni Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitaka jamii ya kimataifa iilazimishe Israel kufuata sheria za kimataifa zinazoilazimisha kuheshimu maeneo ya kidini inayoyakalia kwa mabavu.