Kiongozi


 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Udhmaa Sayyid Ali Khamenei ni mwana wa marehemu Hujjatul Islam wal Muslimin al-Haj Sayyid Jawad Husaini Khamenei. Alizaliwa katika mji mtakatifu wa Mashhad, tarehe 28 Safar (Mfunguo Tano) mwaka 1358 Hijria, mwafaka na tarehe 18 Aprili 1939 Miladia. Yeye ni mwana wa pili wa kiume katika tumbo lao. Maisha ya baba yake yaani Sayyid Jawad Khamenei yalikuwa ya kawaida kabisa kama yalivyo ya wengi wa masheikh, wanazuoni, na waalimu wa masomo ya dini. Mkewe na wanawe walijifunza mengi mazuri kutoka kwake yeye mwenyewe mzee huyo, hasa juu ya maana halisi ya kukinai na kutosheka pamoja na kuishi maisha yasiyo na Makuu, kiasi kwamba sifa mbili hizo zikawa ni miongoni mwa matendo yaliyopamba maisha yao ya kila siku.

Kiongozi Muadhamu anaelezea kumbukumbu za mwanzoni mwa maisha yake na jinsi familia yao ilivyokuwa wakati huo, kwa kusema: ‘’Baba yangu alikuwa Sheikh mashuhuri, lakini licha ya umashuhuri huo alikuwa mcha Mungu mno na mtu aliyeipa mgongo dunia…. Tulikuwa tukiyapitisha maisha yetu ya kila siku kwa taabu na mashaka. Bado ningali nakumbuka pale tulipokuwa tukipitisha usiku wa baadhi ya masiku bila ya kupata mlo kamili wa usiku. Katika hali hiyo, mama yetu aliweza kwa taabu na mashaka kututayarishia chakula cha usiku… na chakula chenyewe basi kilikuwa ni mkate na zabibu kavu.”

Kuhusu nyumba ilimokuwa ikiishi familia yake, Ayatullah Khamenei anauelezea wasifu wake kwa kusema: ‘’Nyumba ya baba yangu nilimozaliwa na kuishi humo hadi nilipofikisha umri wa miaka minne au mitano hivi, ilikuwa na ukubwa wa takriban mita 60 hadi 70 katika mtaa wa watu masikini mjini Mashhad, ambayo ilikuwa na chumba kimoja na kijichumba cha chini ya ardhi kilichokuwa na giza totoro! Wakati baba alipokuwa akijiwa na mgeni (kwa vile alikuwa aalimu na marejeo ya watu kutaaradhia shida zao ilikuwa ni kawaida kupata wageni mara kwa mara), sote tulikuwa tukilazimika kwenda kwenye kijichumba cha chini ya ardhi na kubaki huko hadi mgeni anapoondoka. Tuliendelea kuishi katika hali hiyo hadi pale baadhi ya watu waliokuwa na mapenzi maalumu na baba, walipomnunulia kijiardhi kidogo kando ya nyumba yetu kilichojengwa na kuunganishwa na nyumba yetu, na ndipo idadi ya vyumba vya nyumba yetu ilipoongezeka na kufikia vitatu.”

Hivi ndivyo alivyokulia; na kuanzia umri wa miaka minne yeye pamoja na kaka yake Sayyid Muhammad walipelekwa chuoni kwa ajili ya kujifunza kuandika na kusoma Quran. Baada ya hapo ndugu hao wawili walipelekwa kwenye madrasa ya kidini ambayo ilikuwa ndio kwanza imeanzishwa wakati huo iliyokuwa ikiitwa ‘Daru-ttaalimi Diyanati’ kwa ajili kupata elimu ya msingi ya mafunzo ya dini.


• KATIKA CHUO KIKUU CHA KIDINI (HAWZAT):-

Baada ya kumaliza masomo ya sekondari ambako pia alisoma vitabu vya lugha na sarufi ya Kiarabu, k.v. Jami’u ‘l-Muqaddamaat, Sayyid Ali Khamenei alijiunga na Hawza (chuo kikuu cha kidini) ambako alianza kujifunza kwa baba yake na walimu wengine fasihi na masomo mengine ya kimsingi. Kuhusu kujiunga kwake na chuo cha kidini anasema: “Baba yangu ndiye aliyekuwa sababu kuu ya mimi kuichagua njia hii ya nuru ya kusomea taaluma za dini; na mama yangu naye pia alipendelea jambo hilo na kunishajiisha pia”.

Alisoma katika madrasa za Sulayman Khan na Nawwab, huku baba yake akiwa anasimamia na kufuatilia masomo yake. Katika awamu hiyo alisoma pia kitabu cha Ma’aalim. Kisha baada ya hapo akasoma kwa baba yake na pia kwa kiwango fulani kwa marehemu Sheikh Mirza Mudarris Yazdi vitabu vya kifikihi vya vya Sharai’u ‘l-Islam na Sharh al-Lummah. Aidha alisoma vitabu vingine vya kifikihi na kiusuli, k.v. Rasa’il na Makasib kwa marehemu Sheikh Hashim Qazwini; na masomo yaliyobakia ya usul na fikihi katika kiwango cha kati (sat’h) alisomeshwa na baba yake. Ni jambo la kushangaza na lililo nadra sana kuona kwamba alifanikiwa kukamilisha masomo yote ya shahada ya msingi (muqaddamaat) na ya kati (sat’h) katika muda wa miaka mitano na nusu tu. Katika muda wake wote huo wa masomo, baba yake, marehemu Sayyid Jawad alikuwa na nafasi muhimu katika maendeleo ya mwanawe huyo hodari. Katika upande wa mantiki na falsafa, Sayyid Ali Khamenei alisoma kitabu cha taaluma hizo cha Mandhumah cha Sabzwari, kwanza kwa marehemu Ayatullah Mirza Jawad Agha Tehrani na baadaye kwa marehemu Sheikh Ridha Eisi.


• KATIKA HAWZAT YA NAJAF AL-ASHRAF:-

Akiwa na umri wa miaka 18, Ayatullah Khamenei alianza kuhudhuria darsa za khariji (masomo ya juu kabisa) katika taaluma ya fikihi na usuli kwa marjaa mkubwa wa wakati huo – Ayatullah Udhmaa Milani. Mnamo mwaka 1957, alifunga safari ya kuelekea mjini Najaf al-Ashraf kwa ajili kuzuru maeneo matakatifu. Baada ya kujionea mwenyewe na kushiriki pia katika darsa za khariji za mujtahidi wakubwa wa Hawza ya Najaf akiwemo marehemu Sayyid Muhsin Hakim, Sayyid Mahmud Shahrudi, Mirza Baqir Zanjani, Sayyid Yahya Yazdi na Mirza Hasan Bojnurdi, Sayyid Ali Khamenei alivutiwa na kupendezwa na hali ya masomo hapo, mfumo wa usomeshaji na uhakiki wake, hivyo akamjulisha baba yake nia yake ya kuendelea na masomo huko, lakini baba yake hakukubaliana na wazo hilo. Hivyo, baada ya muda akarejea Mashhad.

• KATIKA HAWZAT YA QUM:-

Kuanzia mwaka 1958 hadi 1964 Ayatullah Khamenei aliendelea na masomo ya juu kabisa ya fikihi, usuli na falsafa katika Hawza ya Qum na kufaidika na elimu za maulamaa wakubwa wakubwa, k.v. marehemu Ayatullah Udhmaa Borujerdi, Imam Khomeini, Sheikh Murtadha Haeri Yazdi na Allama Tabatabai. Mnamo mwaka 1964, walipokuwa wakiandikiana barua, Ayatullah Khamenei aligundua kwamba jicho moja la mzazi wake lilikuwa na mtoto, hivyo alihuzunika mno. Akiwa katika hali ya njia panda baina ya kubaki Qum na kuendelea na masomo katika chuo muhimu cha kidini cha mji huo na kurudi Mash-had kwa ajili ya kwenda kumtunza na kumhudumia baba yake, mwishowe Ayatullah Khamenei alifikia uamuzi wa kurudi Mashhad kwa ajili ya kumtunza na kumshughulikia baba yake. Akizungumzia kuhusu uamuzi wake huo, Ayatullah Khamenei anasema: “Nilielekea Mashhad; na Mwenyezi Mungu Mtukufu alinipa taufiki kubwa. Alakullihali nilikwenda huko kutekeleza wajibu wangu. Kama kuna taufiki nimepata katika maisha yangu, naamini kwamba imetokana na wema huo nilioufanya kwa baba yangu au niseme kwa wazazi wangu.” Kwa hakika, katika kuchagua moja kati ya njia mbili hizo, Ayatullah Khamenei alichagua njia sahihi zaidi. Baadhi ya walimu na watu aliokuwa akijuana nao walikuwa wakisikitika kwa nini aliamua kuondoka Qum mapema kiasi hicho, na kwamba laiti angebaki hapo, angekuja kuwa hivi na vile kimafanikio katika mustakabali. Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa uamuzi aliochukua ulikuwa sahihi, na kwamba takdiri ya Mwenyezi Mungu ilikuwa imemwekea majaaliwa mengine na yaliyo bora zaidi ya yale waliyokuwa wakifikiria wao. Je, kuna mtu aliyeweza hata kuwaza na kufikiria kwamba katika enzi hizo aalimu huyo kijana mwenye kipawa akiwa na umri wa miaka 25, aliyeamua kwa sababu ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kuondoka Qum na kurudi Mashhad ili kwenda kuwatunza na kuwashugulikia wazazi wake, miaka 25 baadaye angekuja fikia daraja ya juu ya kuwa kiongozi wa Umma wa Kiislamu? Aliporudi Mashhad hadi mwaka 1969, Ayatullah Khamenei aliendelea kusoma fikihi na usuli kwa maulamaa wakubwa wa Hawza ya Mashhad na hasa kwa Ayatullah Milani; na hakusitisha masomo yake isipokuwa katika siku za mapumziko au zile alizokuwa akijishughulisha na mapambano au alipokuwa safarini na kifungoni. Aidha kuanzia mwaka 1964 ambapo aliamua kubaki rasmi huko Mashhad kwa ajili ya kusoma na kumtunza baba yake ambaye alikuw amekwishakuwa mzee na mgonjwa, Ayatullah Khamenei alijishughulisha pia na kuwasomesha wanafunzi wa masomo ya kidini na wale wa vyuo vikuu vitabu vya kifikihi, kiusuli na mafunzo mengine ya dini.

• HARAKATI ZA KISIASA:-

Kama anavyoeleza mwenyewe, Ayatullah Khamenei ni miongoni mwa wanafunzi wa Imam Khomeini (Allah amrehemu) katika masomo ya fikihi, usuli na vile vile harakati za kisiasa na kimapinduzi. Hata hivyo, cheche ya kwanza ya harakati za kisiasa na za mapambano dhidi ya taghuti ilipenya katika akili yake kupitia kwa mujahid mkubwa na shahidi katika njia ya Uislamu, Shahid Sayyid Mujtaba Nawwab Safawi, pale Nawab Safawi pamoja na idadi kadhaa ya wanamapambano wengine wa harakati za Fadaiyane Islam walipokwenda Mashhad katika mwaka 1953 na kutoa hotuba kali ya kusisimua na ya kimwamko katika madrasa ya Sulayman Khan juu ya maudhui ya kuuhuisha Uislamu na utawala wa sheria za Mwenyezi Mungu, kubainisha hila na hadaa za Shah na dola la kikoloni la Uingereza, na uwongo wao kwa wananchi wa Iran. Ayatullah Khamenei ambaye siku hiyo alikuwa miongoni mwa vijana wanachuo wa kidini aliathiriwa mno na hotuba kali ya Nawwab. Akizungumzia kuhusu hotuba hiyo, anasema: “Pale pale cheche za hamasa ya kuleta mapinduzi ya Kiislamu zilipenya ndani ya nafsi yangu kutokea kwa Nawwab Safawi, na sina shaka yoyote kuwa marehemu Nawwab Safawi ndiye aliyewasha cheche ya kwanza ya mwamko ndani ya moyo wangu.”


BEGA KWA BEGA NA HARAKATI ZA IMAM KHOMEIN (QUDDISA SIRRUH):-

Tokea mwaka 1962, wakati Ayatullah Khamenei alipokuwa katika mji wa Qum na pale zilipoanza harakati za kimapinduzi na za upinzani za Imam Khomeini dhidi ya siasa za kupiga vita Uislamu na kuikumbatia Marekani za Muhammad Reza Pahlavi, aliingia kwenye uwanja wa mapambano ya kisiasa, ambapo licha ya taabu, mashaka, mateso, kutupwa gerezani na kupelekwa uhamishoni, kwa muda wa miaka 16 kamili aliendelea na mapambano katika njia hiyo bila ya kuhofu hatari yoyote. Kwa mara ya kwanza katika Muharram ya mwaka 1959, Ayatullah Khamenei alipewa jukumu na Imam Khomeini la kwenda kufikisha ujumbe kwa Ayatullah Milani pamoja na maulamaa wengine wa Khorasan, juu ya namna ya kupanga mikakati ya kampeni zitakazoendeshwa na maulamaa wakati wa mwezi wa Muharram za kufichua kwa wananchi siasa za Shah za kujikumbatisha kwa Marekani na juu ya hali ya nchi pamoja na matukio yaliyojiri Qum. Alitekeleza kazi hiyo aliyopewa, kisha yeye mwenyewe akaelekea mji wa Birjand kwa ajili ya tablighi na kufikisha ujumbe wa Imam Khomeini wa kufichua maovu ya utawala wa Kipahlavi na Marekani. Kwa sababu hiyo, tarehe 9 Muharram sawa na tarehe pili Juni mwaka 1963, Ayatullah Khamenei alitiwa nguvuni na kuwekwa rumande hadi siku ya pili yake ambapo aliachiwa huru kwa sharti kwamba asije akapanda mimbari na kutoa hotuba, na pia awe akifatiliwa nyendo zake. Kufuatia kujiri kwa tukio la Khordad 15 (Juni 5) Ayatullah Khamenei aliondolewa Birjand na kupelekwa Mash-had, akakabidhiwa kwenye mahabusu ya kijeshi na kuwekwa rumande kwa muda wa siku kumi huku akikabiliana na mazingira magumu kabisa ya maudhi na mateso.




• KUTIWA NGUVUNI MARA YA PILI:-

Katika mwezi wa Januari mwaka 1964 (Ramadhan 1383), Ayatullah Khamenei pamoja na wenzake kadhaa walipanga mkakati maalumu wa safari ya kuelekea Kerman. Baada ya kusimama kwa siku mbili tatu huko Kerman na kuhutubia na kukutana na maulamaa na wanafunzi wa kidini wa mji huo, waliendelea na safari yao hadi Zahedan. Hotuba kali na za hamasa za Ayatullah Khamenei ziliwavutia wananchi, na hasa zile alizotoa katika siku za kumbukumbu ya tarehe 26 Januari, siku ambayo ulifanyika uchaguzi bandia wa kura za maoni uliopangwa na Shah. Tarehe 15 Ramadhani ambayo ilisadifiana na siku ya kuzaliwa Imam Hasan AS, ushujaa, hamasa ya kimapinduzi na ujasiri ulioonyeshwa na Ayatullah Khamenei wa kufichua siasa za kishetani za Marekani na utawala wa Kipahlavi, zilifikia kilele chake kiasi kwamba usiku huohuo alitiwa nguvuni na Savak (askari wa usalama) na kusafirishwa kwa ndege hadi Tehran. Kwa muda wa karibu miezi miwili, Ayatullah Khamenei aliwekwa katika seli ya peke yake kwenye jela ya Qezel Qal’eh na kukabiliana na kila aina ya mateso na manyanyaso.

• KUTIWA NGUVUNI MARA YA TATU NA YA NNE:-

Darsa zake za tafsiri ya Qur’ani, hadithi na fikra za Kiislamu katika miji ya Mashhad na Tehran zilihudhuriwa kwa wingi mno na vijana wengi waliokuwa na hamasa kubwa ya kimapinduzi. Harakati zake hizo ziliwaghadhibisha Savak na hivyo wakaanza kumfuatilia. Kutokana na hali hiyo, katika mwaka 1967 Ayatullah Khamenei akawa anaishi kwa kujificha katika mji wa Tehran, na mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 1968, alitiwa nguvuni na kuwekwa korokoroni. Harakati hizo za kielimu na uwekaji vikao, usomeshaji na utoaji hotuba za kuiamsha na kuirekebisha jamii, ndizo zilizopelekea mnamo mwaka 1971 akamatwa tena na kikosi cha usalama (Savak) cha utawala wa Shah na kutiwa jela.


 • KUTIWA NGUVUNI MARA YA TANO:-

Akizungumzia kutiwa nguvuni kwake kwa mara ya tano na Savak, Ayatullah Khamenei (Allah ampe umri) amesema: “Kuanzia mwaka 1970, mazingira ya kuanzishwa harakati za mtutu wa bunduki yalianza kuhisika nchini Iran. Harakati za vyombo vya utawala wa wakati huo za kunifuatilia mimi zilikuwa kubwa mno na zikazidi kuongezeka kwa sababu vilihisi kwamba haingewezekana kuwepo harakati kama hizo bila kuwa na mahusiano na watu kama mimi. Mwaka wa 1971 na kwa mara ya tano nilitiwa jela tena. Vitendo vya kikatili vilivyokuwa vikifanywa na Savak huko jela, vilionyesha dhahiri kuwa vyombo vya dola vilikuwa na hofu kubwa ya kuungana harakati za mapambano ya silaha na zile za fikra za Kiislamu, na havikuwa tayari kukubali kwamba harakati zangu za kifikra na kitablighi za Mashhad na Tehran hazikuwa na mfungamano na harakati hizo. Baada ya kuachiwa huru, wigo wa darsa zangu za tafsiri kwa watu wote na zile za siri za masuala ya kiitikadi zilizidi kuongezeka.”

• KUTIWA NGUVUNI MARA YA SITA:-

Kati ya mwaka 1971-1974 darsa za tafsiri ya Qur’ani na masuala ya kiidiliojia (kiitikadi) za Ayatullah Khamenei zilikuwa zikifanyika katika misikiti mitatu: Karamat, Imam Hasan AS na Mirza Jaafar huko Mashhad na kuvutia watu wengi hasa vijana waelewa, walioamka kifikra, na wanafunzi wanamapinduzi wa kidini ambao walipata fursa ya kuelewa fikra sahihi za Kiislamu. Darsa zake za Nahju ‘l-Balagha, nazo pia zilikuwa na msisimko na hali ya aina yake, na zikawa zinachapishwa na kukathiriwa na mashine ya kurudufia kwa jina la “Nuru kutoka kwenye Nahju ‘l-Balagha” na kusambazwa mkono mwa mkono. Wanafunzi vijana wanamapinduzi wa kidini ambao walikuwa wakisoma kwa Ayatullah Khamenei darsa juu ya ukweli na mapambano, walikuwa wakielekea kwenye miji ya mbali na karibu ya Iran kuziamsha fikra za wananchi kwa kuwaelimisha juu ya masuala hayo na kutayarisha mazingira kwa ajili ya mapinduzi makubwa ya Kiislamu.

Kwa sababu ya harakati hizo, mnamo mwezi Disemba mwaka 1974, Savak walivamia nyumba ya Ayatullah Khamenei huko Mashhad wakamtia nguvuni na kukamata pia kumbukumbu na maandishi yake mengi. Hiyo ilikuwa ni mara yake ya sita kutiwa nguvuni na kukabiliwa na hali mbaya zaidi. Aliendelea kuwekwa kwenye jela ya makao makuu ya polisi hadi msimu wa mapukutiko wa mwaka 1975 . Katika kipindi hicho cha kuweko korokoroni aliwekwa kwenye seli yenye hali mbaya mno. Mateso na shida alizozipata katika wakati huo alipotiwa nguvuni kwa mara ya sita, ni kama anavyoeleza mwenyewe kwamba: “Wanaoweza kuyaelewa hasa ni wale tu waliowahi kufikwa na hali hiyo.” Baada ya kutolewa jela, alirejea kwenye mji mtakatifu wa Mashhad na kuendelea na ratiba zake zilezile za utafiti wa kielimu na harakati za kimapinduzi. Hata hivyo hakupewa fursa tena ya kuendesha darsa zake kama ilivyokuwa zamani.


 • UHAMISHONI:-

Mwishoni mwa mwaka 1977, utawala wa kinyama wa Kipahlavi ulimtia nguvuni Ayatullah Khamenei na kumpeleka uhamishoni kwa muda wa miaka mitatu huko kwenye mji wa Iranshahr. Katikati ya mwaka 1978 wakati harakati za mapambano ya wananchi Waislamu na wanamapinduzi wa Iran zilipokuwa zimepamba moto, Ayatullah Khamenei aliachiwa huru huko uhamishoni na hivyo kurejea mjini Mashhad ambako alijiunga kwenye safu ya mbele ya mapambano ya wananchi dhidi ya utawala katili wa Kipahlavi. Mwishowe, baada ya miaka 15 ya mapambano ya kishujaa, jihadi na subra katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kuvumilia kila aina ya taabu, shida na machungu, aliyashuhudia matunda ya mapambano hayo, ambayo yalikuwa ni ushindi wa mapinduzi makubwa ya Kiislamu ya Iran na kuanguka kiidhilali kwa utawala wa kidhalimu wa Kipahlavi na kusimamishwa utawala wa Kiislamu katika ardhi ya Iran.


 • KARIBU NA USHINDI WA MAPINDUZI.

Wakati ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulipokuwa unakaribia, kabla ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) kurejea nchini kutoka Paris (Ufaransa), kiongozi huyo aliunda Baraza la Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran lililoshirikisha shakhsia wanamapambano kama vile Shahid Mutahhari, Shahid Beheshti, Hashemi Rafsanjani na wengineo. Kwa amri ya Imam Khomeini, Ayatullah Khamenei akawa ni miongoni mwa wajumbe wa baraza hilo. Ujumbe wa Imam Khomeini wa kumteua kuwa mjumbe wa baraza hilo alifikishiwa Ayatullah Khamenei na Shahid Mutahari (r.a), na baada ya kupokea ujumbe huo wa kiongozi mkuu wa Mapinduzi aliondoka Mashhad na kuelekea Tehran.

********

Baada ya ushindi wa mapinduzi ya kiislamu, Ayatullah Khamenei aliendelea kwa hamu, shauku na raghba kubwa na harakati za Kiislamu na kubeba majukumu mbalimbali ili kuhakikisha malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu yanafikiwa; majukumu ambayo kila moja na katika wakati wake lilikuwa na athari ya kipekee na umuhimu mkubwa mno. Majukumu na nyadhifa hizo katika mfumo wa jamhuri ya Kiislamu ya Iran tunazitaja hapa kwa muhtasari:

• Kuasisi Chama cha Jamhuri ya Kiislamu (Hizb-e Jamhoriy-e Islami) mnamo mwezi Machi mwaka 1979 kwa ushirikiano wa wanazuoni wanamapambano wenzake kama vile Shahid Beheshti, Shahid Bahonar, Hashemi Rafsanjani, n.k.
• Naibu Waziri wa Ulinzi, mwaka 1980.
• Msimamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah), mwaka 1980.
• Imam wa Sala ya Ijumaa ya Tehran, mwaka 1980.
• Mwakilishi wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) katika Baraza Kuu la Ulinzi, mwaka 1981.
• Mbunge wa wananchi wa Tehran katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), mwaka 1980.
• Mnamo mwezi Septemba mwaka 1980 pale vilipoanza vita ilivyotwishwa Iran na Iraq, aa jeshi la Saddam kushambulia mipaka ya Iran kwa uchochezi na misaada ya silaha ya madola makubwa na ya kishetani yakiwemo ya Marekani na Urusi ya zamani, Ayatullah Khamenei akiwa amevalia sare za kijeshi alijiunga kwenye medani za vita vya kujitetea kutakatifu.
• Tarehe 27 Juni mwaka 1981 alijeruhiwa vibaya katika jaribio la kutaka kumuua lililofanywa na wanafiki kwa kutega bomu wakati akihutubia ndani ya msikiti wa Abu Dharr mjini Tehran
• Kufuatia kuuawa shahidi Muhammad Ali Rajai, Rais wa pili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mnamo mwezi Septemba mwaka 1981, Ayatullah Khamenei alichaguliwa kwa kura zaidi ya milioni kumi na sita na kupewa hukumu ya kuidhinishwa rasmi kuwa Rais na Imam Khomeini (quddisa sirruh). Alichaguliwa tena kwa mara ya pili kuwa Rais na kushika wadhifa huo kutoka mwaka 1985 hadi mwaka 1989.
• Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Utamaduni, mwaka 1981.
• Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo (wa Kiislamu), mwaka 1987.
• Mwenyekiti wa Baraza la Kuipitia Upya Katiba, mwaka 1989.
• Mnamo tarehe 4 Juni mwaka 1989, na kufuatia kuaga dunia Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini (quddisa sirruh), Ayatullah Khamenei alichaguliwa na Baraza la Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi, kuwa Kiongozi Mkuu na Fakihi Mtawala. Uteuzi huo ulikuwa sahihi na wenye baraka kwani baada ya kuaga dunia Imam Khomeini, Ayatullah Khamenei ameweza kwa mafanikio makubwa kuuongoza Umma wa Kiislamu wa Iran bali pia Umma wa Kiislamu duniani.

• UANDISHI NA UTAFITI:-

1. Nadharia Jumla ya Fikra za Kiislamu katika ya Quran
2. Katika Kina cha Sala
3. Mazungumzo kuhusu Subira
4. Vitabu Vinne Vikuu katika Elimu ya Rijali
5. Utawala (Wilayat)
6. Ripoti Kuhusu Historia na Hali ya Sasa ya Hawza ya Mashhad
7. Wasifu wa Maimamu wa Kishia (Hakijachapishwa)
8. Viongozi Wakweli
9. Umoja na Uundaji Vyama
10. Sanaa kwa Mtazamo wa Ayatullah Khamenei
11. Ufahamu Sahihi wa Dini
12. Nafasi ya Mapambano Katika Maisha ya Maimamu AS
13. Roho ya Tawhidi: Kutomwabudu Asiyekuwa Allah
14. Haja ya Kurejea kwenye Qur’ani
15. Sira ya Imam Sajjad AS
16. Imam Ridha AS na Urithi wa Ukhalifa
17. Hujuma za Kiutamaduni (Mkusanyiko wa Ujumbe na Hotuba za Kiongozi Muadhamu)
18. Hadithi ya Wilayat (Mkusanyiko wa Ujumbe na Hotuba zake ambazo hadi sasa zimeshachapishwa katika juzuu 9), n.k.

• TARJUMA:-

1. Suluhu ya Imam Hasan AS, kimeandikwa na Radhi Aal Yasin
2. Mustakabali katika Ulimwengu wa Uislamu, kimeandikwa na Sayyid Qutb
3. Waislamu Katika Harakati za Ukombozi wa India, kimeandikwa na Abdul Mun’im Namri Nasri
4. Hati ya Mashtaka Dhidi ya Ustaarabu wa Magharibi, kimeandikwa na Sayyid Qutb.


NCHI ZINAZOJITAKIA MAKUU ZIMEZUIA UTATUZI WA KADHIA YA NYUKLIA YA IRAN.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema nchi chache zinazojitakia makuu zinazuia utatuzi wa kadhia ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumatano wakati alipokutana na mkuu na maafisa wa ngazi za juu wa Vyombo vya Mahakama. Mkutano huo umefanyika kwa mnasaba wa kuwadia kumbukumbu ya kuuawa shahidi Ayatullah Muhammad Beheshti na makada 72 wa Mapinduzi ya Kiislamu Juni 28 mwaka 1981 ambayo huadhimishwa kama Siku ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran.

Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu ameashiria hati iliyotiwa saini na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA ambapo wakala huo unakiri kuwa hakuna tatizo katika shughuli za kuzalisha nishati ya nyuklia za Iran na kwamba faili la nyuklia la Iran linapaswa kufungwa. Amesema punde baada ya kutiwa saini hati hiyo Marekani iliibua masuala mapya ili kutumia kadhia ya nyuklia kama njia ya kuitisha na kuishinikiza Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia uchochezi wa Wazayuni katika kadhia ya nyuklia ya Iran na kusema, 'katika kadhia ya nyuklia, Jamhuri ya Kiislamu inaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria, kwa uwazi na kwa mtazamo wa dalili na ina mantiki yenye nguvu lakini malengo ya maadui ni kuendeleza mashinikizo, kulichosha taifa na kubadilisha mfumo wa utawala hapa nchini na kwa msingi huo hawataruhusu kadhia hii itatuliwe. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, kwa Wamagharibi shughuli za nyuklia, haki za binaadamu na demokrasia ni vitu visivyo na maana na kile wanachofuata ni kuzuia ustawi wa taifa na kueneza tena ubeberu wao nchini Iran lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uwezo, uhuru kamili, kutegema wananchi na kutawakali kwa Allah, imesimama kidete na italinda maslahi yake.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amepongeza hamasa  adhimu na ya hakika ya taifa erevu na lenye uono wa mbali la Iran katika uchaguzi wa Juni 14. Ameongeza kuwa siri ya kushiriki  kwa wingi taifa katika uchaguzi wa mwaka huu ni imani na mapenzi yao kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, imani kwa wasimamizi wa uchaguzi na matumaini ya taifa kuhusu ustawi wa Iran. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa kuna udharura wa kumsaidia rais-mteule na kuongeza kuwa, njama za maadui zimefeli katika pande zote. Aidha amesifu hatua ya wagombea wote kumpongeza rais-mteule na kusema jambo hilo linaashiria utiifu wao kwa sheria pamoja na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kiongozi Muadhamu amesema pamoja na kuwa serikali inayoondoka ina udhaifu lakini pia ina nukta za nguvu na hivyo wagombea urais pamoja na kuashiria nukta za udhaifu wangepaswa pia kutaja mafanikio yaliyopatikana hasa katika ustawi wa miundo msingi.

KIONGOZI MUADHIMU ASISITIZA UMOJA WA WAISLAMU.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema koo na ulimi wa wale wanaotoa wito wa umoja miongoni mwa Waislamu ni koo ya Mwenyezi Mungu na koo na ulimi unaoibua  uhasama miongoni mwa Waislamu na madhehebu za Kiislamu ni ulimi wa shetani.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei aliyasema hayo Jumamosi wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na maustadh, maqarii na mahafidh wa Qur'ani Tukufu walioshiriki kwenye Mashindano ya 30 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaliyofanyika hapa mjini Tehran. Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amesema moja kati ya maamrisho muhimu ya Qur'ani Tukufu kwa Waislamu ni kuwataka wadumishe umoja na mashikamano. Ameongeza kuwa kujifundisha maarifa ya Qur'ani ni jambo ambalo huandaa mazingira ya kufikia usalama, amani, heshima na kuimarika zaidi maisha ya Waislamu katika kivuli cha mafundisho ya Qur'ani Tukufu. Kiongozi Muadhamu pia amesisitiza ulazima wa Waislamu kujikurubisha na kuifahamu zaidi Qur'ani Tukufu pamoja na maarifa yake yenye kuleta saada. Ameongeza kuwa kati ya maamurisho ya Qur'ani ni kuwataka Waislamu washikamane kwa kamba ya Mwenyezi Mungu na wasifarakiane. Amesema mkabala ya hilo ni njama na mbinu za mabeberu za kuibua hitilafu katika Umma wa Kiislamu na kushadidisha taasubi za kimadhehebu. Kiongozi Muadhamu ameashiria namna baadhi ya tawala na serikali za nchi za Kiislamu zilivyohadaiwa na kuingia katika mtego wa adui na kusema umoja na mshikamano wa Waislamu ni faradhi ya dharura. Kiongozi Muadhamu amesema utawala wa Kizayuni ndio unaofaidika na umwagikaji damu na hitilafu katika umma wa Kiislamu. Ayatullah Khamenei pia ameashiria wimbi la chuki dhidi ya Uislamu linaloongozwa na nchi za Magharibi na kusema adui wa Kimagharibi amewaelekezea Waislamu upanga na hivyo Umma wa Kiislamu unapaswa kujiimarisha ili kukabiliana na hali hiyo.

AYATULLAHIL UDHMA KHAMENEI: WAIRAN WANAJIAMINI.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehutubia hadhara kubwa ya wananchi na wageni kutoka mataifa mbalimbali waliokuja hapa nchini kushiriki kwenye maadhimisho ya kukumbuka kutimia miaka 24 tokea alipofariki dunia Imam Khomeini MA na kusema kuwa, kujiamini na ushujaa ndio siri ya mafanikio ya wananchi wa Iran.  Ayatullahil Udhma Ali Khamenei amesema kuwa, maadui waliwaelezea wananchi  wa Iran  kuwa ni watu wasio na uwezo  kwani wako nyuma miaka 100 kwenye medani za kisiasa, kielimu na kiuchumi lakini Imam Khomeini aliwaambia wananchi wa Iran kuwa munaweza kupiga hatua kubwa kwenye medani hizo mtakapokuwa mumejenga moyo wa ushujaa na kujiamini. Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, pamoja na kuwepo njama zote za maadui lakini wananchi wa Iran wameweza kupata ushindi kwenye medani zote, na  hivi sasa Iran iko huru na wala haitegemei madola ya kibeberu. Ayatullah  Khamenei amesema hivi sasa Iran ni moja kati ya nchi zilizopiga hatua kielimu duniani na kusisitiza kwamba Kituo cha Utafiti Duniani kimetangaza kuwa, ukuaji wa kielimu nchini ni mkubwa na hadi kufikia mwaka 2017 Iran itashika nafasi ya nne kielimu duniani. Kuhusiana na uchaguzi wa rais hapa nchini, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, uchaguzi ni dhihirisho la hamasa ya kisiasa ya wananchi na kusisitiza kuwa, wananchi wa Iran daima wako mstari wa mbele katika uwanja wa kulinda thamani za mapinduzi.

WANANCHI WATATHIBITISHA MAFANIKIO YA MFUMO.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kujitokeza kwa wingi na kwa shauku taifa la Iran katika uchaguzi wa Juni 14 mwaka huu kutaonesha mafanikio makubwa ya Mapinduzi na mfumo wa Kiislamu wa Iran. Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo leo katika sherehe za kuhitimu wanafunzi wa chuo kikuu cha kijeshi cha Imam Hussein (A.S) hapa mjini Tehran. Huku akiwahusia wananchi kuzingatia nara na ilani za uchaguzi za wagombea ili kutambua na kumchagua yule anayefaa, Ayatullah Khamenei amesema, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mustakbali wa nchi na taifa la Iran utakuwa wazi, wenye izza na mfano kwa wote. Pia amewausia wagombea wa duru ya 11 ya uchaguzi wa rais wa Iran kujiepusha na kampeni za uharibufu na pia kuzingatia maadili.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kuhudhuria kwa wingi wananchi katika vituo vya kupigia kura kunakodhihirisha ushiriki mkubwa wa taifa la Iran katika matukio mbalimbali ya nchi, bila shaka kutaandaa mazingira ya kuipatia izza na kinga serikali kimataifa, kuwafurahisha marafiki na kuwachukiza maadui wa Iran. 

WAIRAN WATAVUNJA NJAMA ZA MAADUI KATIKA UCHAGUZI.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, 'katika kufikia malengo yao na kuvunja njama za maadui, wananchi wa Iran watajitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao wa rais na kumchagua mgombea aliye bora ili aweze kuchukua jukumu zito la kusimamia ustawi na ezza ya taifa.'

Ayatullahil Udhma Sayyed Ali Khamenei ameyasema hayo Jumatano ya leo mjini Tehran alipokutana na maelfu ya watu kutoka matabaka mbali mbali ya jamii. Ameongozea kuwa uchaguzi wa rais utakaofanyika Juni 14 ni mtihani mwingine wenye fakhari kwa taifa la Iran. Amebainisha malengo yanayokinzana ya taifa la Iran na maadui katika uchaguzi ujao na kusema: 'katika uchaguzi huo mtu mmoja atachaguliwa kwa kura za taifa kusimamia masuala muhimu ya nchi kwa muda wa miaka minne.' Amesema  baadhi ya maamuzi sahihi au yasiyo sahihi ya rais yanaweza kuwa na taathira kwa miaka mingi na kwa hivyo ukweli huu unaashiria kuwa uchaguzi wa rais ni muhimu sana. Kiongozi Muadhamu amefafanua kuhusu umuhimu wa uchaguzi ujao kwa kusema: 'Pamoja na kuwa umesalia takribani mwezi mmoja kabla ya uchaguzi, kadhia hii imebadilika na kuwa suala muhimu la kimataifa. Majopo ya kifikra duniani na maadui wa Iran wanafuatilia kwa karibu hata utangulizi wa uchaguzi huu.'

Ayatullahil Udhma Sayyed Ali Khamenei amesisitiza kuwa watu wa Iran wanataka kumchagua mtu bora zaidi kwa ajili ya kuliwezesha taifa listawi kwa kasi katika uga wa kimaada na kimaanawi ili mbali na kutatua matatizo yaliyopo na kuleta maisha bora, ezza na uhuru wa Iran uweze kudumishwa katika fremu ya 'shauku na matumaini ya wananchi.'' Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema kuwa, maadui wanataka kupoza joto la uchaguzi na kuona mtu dhaifu akichaguliwa, ambaye ataifanya Iran iwe tegemezi, dhaifu,  ibaki nyuma katika nyuga mbali mbali na iende sambamba na sera za madola ya kigeni. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa awali maadui walitaka kuhakikisha kuwa uchaguzi haufanyiki lakini sasa baada ya kuona wamefali katika hilo wanataka kuvunja motisha wa wananchi ili wasishiriki katika uchaguzi. Ayatullahil Udhma Khamenei amesema mtandao mkubwa wa vyombo vya habari vya Kizayuni vinajaribu kuonyesha kuwa eti kuna mgogoro nchini Iran na kukuza kupita kiasi matatizo sambamba na kuchochea hisia za kutokuwa na matumaini kuhusu utatuzi wa matatizo na kuonyesha mustakabali wenye kiza. Kiongozi Muadhamu amesema mbinu hizo zimekuwa zikitumiwa na mitandao mikubwa ya habari yenye kueneza uongo na upotofu kwa lengo la kuzima joto la uchaguzi wa Iran.
 

 MWANAMKE AANGALIWE KWA JINSIA YAKE.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa mtazamo sahihi juu ya mwanamke ni ule unaozingatia jinsia yake na thamani zinazomtukuza. Ayatullahil Udhma Seyyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo kwa mnasaba wa kuwadia mwezi mtukufu wa Rajab mbele ya hadhara ya mamia ya wanawake wanaoshughulika katika sekta za vyuo vikuu, vyuo vikuu vya kidini, masuala ya familia na wanawake, taasisi za utendaji, masuala ya Qur’ani, vyombo vya habari na jumuiya za wananchi. Amesema “kuimarisha taasisi ya familia” na “kumheshimu na kumuenzi mwanamke katika mazingira ya nyumbani” ni masuala mawili muhimu na ya dharura yanayohitajiwa na jamii. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa wanawake wanaharakati na wafanisi katika harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu wanapaswa kujitokeza kwa wingi zaidi na kwa uwazi zaidi katika uga wa kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Huku akisisitiza kwamba hakuna mushkeli wowote kwa wanawake kufanya kazi na kushika nyadhifa za utendaji, Ayatullah Khamenei amesema suala lenye mushkeli na ambalo kwa hakika ni kuendeleza mtazamo wa Kimagharibi ni kujivunia kuwa ni idadi kubwa ya wanawake wafanyakazi katika nyadhifa za utendaji. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua kama ninavyonukuu:”Ni mtazamo potofu na kwa kweli ni kusalimu amri mbele ya mtazamo wa Kimagharibi kwa sisi kujivunia kuwepo wanawake wengi katika nyadhifa za utendaji. Kinachopasa kujivunia ni kuwepo idadi kubwa ya wanawake wanafikra, mujahidina na wanaharakati wa kiutamaduni na kisiasa”. Ayatullah Khamenei ameashiria jinsi Uislamu ulivyo na mtazamo sawa kwa mwanamke na mwanamme kwa mtazamo wa kiutu na kusisitiza kwamba kwa mtazamo wa Uislamu, kila mmoja kati ya mwanamke na mwanamme kwa upande wa maumbile ana hali zake maalumu, lakini kwa upande wa haki za kiutu na kijamii na thamani za kimaanawi na katika kufikia kwenye ukamilifu wa kimaanawi hakuna tofauti yoyote baina yao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema heshima ya mwanamke, izza ya mwanamke na uwezo wa kimaumbile na kiutendaji wa mwanamke ni miongoni mwa sifa maalumu za mtazamo wa Uislamu juu ya mwanamke na huku akiashiria kujitokeza kwa wingi na kwenye uzito mkubwa wanawake wakati wa harakati wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na katika vipindi tofauti baada ya Mapinduzi alisema, wanawake wanaharakati, wenye ufanisi, wajuzi, waandishi na wanafikra katika harakati ya ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wanapaswa kujitokeza katika medani kwa uwazi zaidi na kwa uzito mkubwa zaidi.


 SEKTA YA ELIMU NI MUHIMU KATIKA USTAWI WA IRAN.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kuendelea mkondo wa kasi wa ustawi wa Iran katika nyanja mbali mbali ni jambo linalohitajia harakati ya kuibua hamasa ya kisiasa na kiuchumi na katika hili sekta ya elimu ina nafasi muhimu. Ayatullahil Udhma Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumatano mjini Tehran alipokutana na maelfu ya waalimu kutoka kote nchini. Amesema sekta ya elimu ni muhimu sana na ni muundo msingi mkuu katika kujenga jamii iliyostawi, yenye msingi wa kibinaadamu na mfumo wa Kiislamu wa maisha. Katika mkutano huo uliofanyika kwa mnasaba wa 'Wiki ya Kumuenzi Mwalimu' nchini Iran, Ayatullah Khameni amemkumbuka na kumuenzi Ayatullah Shaheed Ustad Mutahhari, waalimu pamoja na wanafunzi mashahidi. Kiongozi Muadhamu alisema nafasi na hadhi ya kazi ya ualimu katika jamii ya Kiislamu ni ya juu sana na kwamba inatafuatiana na kazi zingine zote. Kiongozi Muadhamu amesema kupatikana hamasa ni jambo linalohitajia nishati na kupewa nafasi watu wote wakiwemo waalimu na wanafunzi. Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa nchi na taifa kubwa la Iran, kwa kuzingatia malengo yake ya juu, linahitajia hamasa na harakati kubwa katika setka zote. Huku akiashiria ustawi wa ajabu wa taifa la Iran katika miongo mitatu iliyopita hasa ustawi wa kielimu, Kiongozi Mudhamu amesema, 'ustawi wa kielimu wa Iran ni mkubwa kiasi kwamba taasisi za kimataifa hazina budi ila kukiri ukweli huo.


 MAADUI WANACHOCHEA UADUI BAINA YA WAISLAMU.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa, maadui wanataka kuwasha moto wa uadui kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni kwa kuvunjia heshima haramu tukufu ya swahaba wa Mtume SAW nchini Syria.

Akiwahutubia hii leo maafisa wanaoshughulikia uchaguzi wa duru ya 14 wa rais hapa nchini, Ayatullah Khamenei ametoa wito wa kuendelea kulaaniwa kitendo cha kuvunjiwa heshima kaburi tukufu la Sahaba wa Mtume Muhammad (SAW) Hujr bin Adi (R.A)

Ayatullah Khamenei ametahadharisha kwamba, vitendo kama hivyo vitaendelea iwapo maulamaa wa Kiislamu na shakhsia wa kisiasa watashindwa kuvikemea na kuvilaani.

Katika upande mwingine Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kujitokeza kwa wingi wananchi katika duru hii ya uchaguzi wa rais hapa nchini Iran kutaupa iitibari uchaguzi na kudhamini maendeleo na ustawi wa taifa.


 UISLAMU UNALINDA HAKI ZA WANAWAKE.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, mtazamo wa Uislamu na Qur'ani kwa haki za kijamii na mtu binafsi za mwanaume na mwanamke ndio mtazamo wa kimantiki, matini na kielimu zaidi.

Ayatullahil Udhma Sayyed Ali Khamenei ameyasema hayo siku ya Jumatano mjini Tehran alipokutana na malenga na wasomaji tungo za kumsifu Mtume na Ahul Bayt Watukufu AS, sambamba na kuadhimisha siku ya maulidi na kuzaliwa Bibi Fatima Zahra SA na vile vile kukumbuka kuzaliwa Imam Ruhullah Khomeini MA siku ambayo inatambuliwa kama Siku ya Mwanamke hapa Iran. Kiongozi Muadhamu amesisitiza juu ya udharura wa kuenzi nafasi ya mwanamke na kusema, mbele ya Allah SWT hakuna tafauti kati ya mwanaume na mwanamke katika mkondo wa umaanawi na haki za kijamii na mtu binafsi. Amesema kuamiliana na mwanamke kunapaswa kuandamana na heshima pamoja na adabu.

Ayatullahil Udhma Khamenei amekosoa sera za Wamagharibi kuhusu masuala ya mwanamke na kuashiria jinsi mwanamke anavyotendewa dhulma katika ustaarabu wa kimaada wa Magharibi. Amesema muamala huo ni dhambi kubwa isiyoweza kusamehewa. Amesema natija ya muamala huo mbaya haiwezi kufidiwa. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mwelekeo wa ustaarabu wa kimagharibi kuhusu mwanamke umeandaa mazingira ya kumfanya mwanamke kuwa chombo cha kukidhi starehe za wanaume na kumvunjia heshima. Amesema mwanamke anatendewa vibaya katika utamaduni wa Magharibi na hilo linatajwa kuwa ni uhuru jambo ambalo limepelekea kuporomoka familia. Ameongeza kuwa wakati misingi ya familia inapotikisika, jambo hilo huathiri vibaya jamii yote na kwa hivyo ustaarabu wa Magharibi ambao una sheria khabithi kuhusu mwanamke, utaangamia.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameendelea kusema kuwa, leo kuchochea hisia na taasubi za kimadhehebu ni jambo lisilo sahihi na linalokiuka maslahi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kila nchi na kila ustaarabu unahitaji harakati ya kijihadi isiyo na kikomo kwa ajili ya maendeleo na hivyo malenga wana nafasi muhimu katika kueneza itikadi imara na matumaini.


 UISTIKBARI WATIWA WASIWASI NA MWAMKO WA KIISLAMU.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema leo katika kikao cha Kimataifa cha Maulamaa na Mwamko wa Kiislamu kilichoanza leo hapa Tehran kuwa kadhia ya mwamko wa Kiislamu ni suala kuu linalouhusu  umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa kile tunachokishuhudia hii leo na ambacho mwanadamu yoyote hawezi kukizuia ni hiki kuwa, Uislamu umekuwa na nafasi mashuhuri katika kuainisha  matukio ya ulimwengu. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mwamko wa Kiislamu sasa limekuwa jambo jipya katika dunia ya sasa, mwamko ambao ulikuwa mtupu baada ya kushindwa Ukomonisti na Uliberali.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa wasemaji wa mrengo Uistikbari ambao wanatiwa wasiwasi pia kwa kutaja neno mwamko wa Kiislamu , ni ukweli usiopingika hii ni kwa sababu ishara zake zinaweza kushuhudiwa katika  ulimwengu wa Kiislamu. Amesema taathira za mwamko wa Kiislamu ni kubwa mno na kwamba  kile kinachoweza kushuhudiwa hivi sasa kufuatia kujitokeza mwamko wa Kiislamu katika baadhi ya nchi za Kiafrika  ni dhihirisho la wazi la mustakbali wa nchi hizo unaotoa matumaini ya kufikiwa matarajio makubwa zaidi katika nchi hizo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni uzoefu wa gharama ya juu katika kukabiliana na madola ya kibeberu, matunda ambayo yameyayumbisha madola hayo.  Maulamaa na wasomi wa Kiislamu karibu ya 700 kutoka nchi za Kiislamu na zisizo na Kiislamu  na wa dini nyingine wanashiriki kwenye Kongamano la Kimataifa la Maulamaa na Mwamko wa Kiislamu ulioanza leo hapa Tehran kwa hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.



IRAN INAHITAJI RAIS SHUJAA NA ANAYECHUKIA UISTIKBARI.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, katika uga wa kimataifa taifa la Iran linahitajia Rais ambaye ni shujaa na mwenye kuuchukia uistikbari; amma katika uga wa ndani, taifa hili linahitaji Rais mwenye tadbiri, hekima na tabia njema. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo kwa mnasaba wa kukaribia maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaani Mei Mosi wakati alipohutubia maelfu ya wafanyakazi wa sekta ya uzalishaji na kundi la wafanyakazi bora kutoka pembe mbalimbali za nchi hii na kusisitiza kwamba, uchaguzi ni zoezi muhimu na ni uga wa kudhihirika nguvu za taifa  na kusisitiza kwamba, katika uga wa kimataifa Iran inahitajia Rais ambaye atasimama na kukabiliana na mabeberu na ambaye ni shujaa na mtu ambaye katika masuala ya ndani ana mipango, tadbiri, hekima, mwenye nara za kimantiki ambazo zinaendana na uhakika wa mambo na ambaye ana imani na uchumi wa kimuqawama.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, hamasa ya kisiasa ni mahudhurio ya wananchi yenye welewa katika uga wa kisiasa. Ayatulahil Udhma Khamenei amesema kuwa, watu wanaotaka kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wanapaswa kujitosa baada ya kufanya tathmini sahihi. 



MITAZAMO YA MAREKANI INAKINZANA KUHUSU MAUAJI YA WATU WASIO NA HATIA.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Marekani ina mtazamo unaokinzana kuhusu mauaji ya watu wasio na hatia.

Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo Jumatano ya leo mjini Tehran alipokutana na baadhi ya makamanda wa jeshi, wafanyakazi na wanachama wa vituo vya jeshi la kujitolea (Basij) na familia zao kwa mnasaba wa tarehe 18 Aprili ambayo ni Siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu ameashiria muamala unaokinzana wa Marekani na kusema: "Marekani na wale wengine wanaodai kutetea haki za binaadamu wananyamazia kimya mauaji ya watu wasio na hatia Pakistan, Afghanistan, Iraq na Syria lakini baada ya milipuko michache Wamarekani wanaibua rabsha duniani. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ameongeza kuwa kinyume na madai ya wakuu wa Marekani kuwa wanapinga silaha za mauaji ya umati lakini ndege zisizo na robani za nchi hiyo zinawaua kwa umati watoto, wanawake na watu wengine wasio na hatia Afghanistan na Pakistan na fauka ya hayo Marekani inawaunga mkono wazi wazi na  kwa siri magaidi wanaouwa raia wa Iraq na Syria.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kufuata mantiki ya Kiislamu, inapinga na inalaani milipuko na mauaji ya watu wasio na hatia iwe ni Boston, Marekani au Pakistan, Afghanistan, Iraq na Syria.

Ayatullahil Udhma Khamenei amesema kuwepo sera zinazokinzana, zisizo na mantiki, utumiaji mabavu na upuuzaji wa misingi ya ubinaadamu katika muamala wa nchi za Magharibi ni jambo ambalo litapelekea kusambaratika na kuangamia ustaarabu wa Magharibi.

Kiongozi Muadhamu ambaye pia ni Amri Jeshi Mkuu ameashiria mwelekeo tafauti wa vikosi vya kijeshi vya Iran ikilinganishwa na majeshi ya dunia na kusema, vikosi vya jeshi, Sepah na Basij vimeleta utamaduni na mwelekeo mpya duniani na sasa ni kigezo cha kuigwa katika kukabiliana na mwelekeo wa kikoloni na kibeberu katika majeshi mengi duniani. Ameongeza kuwa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni chanzo cha fakhari na ni jeshi la wananchi, la kielimu, kiitikadi na pia ni jeshi lenye ubunifu.

Kiongozi Muadhamu amesema mafanikio yote katika jeshi yamepatikana katika hali ambayo wanaolitakia mabaya taifa la Iran wamekataa kulipatia taifa hili hata suhula za kimsingi kabisa lakini kutokana na kuchanua vipawa, vijana wa taifa la Iran wameibua maajabu. Kiongozi Muadhamu ameashiria mwelekeo wa kibeberu katika vikosi vya kijeshi vya mrengo wa istikbari hasa Marekani na kusema kila sehemu majeshi hayo yanapofika huibuka ufisadi wa kimaadili, mashinikizo na mauaji ya watu.


HOTUBA YA KIONGOZI MUADHAMU KUHUSU UCHAGUZI NA KADHIA YA NYUKLIA YA IRAN.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutana na mkuu na viongozi waandamizi wa vyombo vya mahakama hapa nchini Iran, na kutoa hotuba muhimu kuhusiana na uchaguzi wa rais uliofanyika Juni 14  hapa nchini pamoja na misimamo ya madola ya kibeberu dhidi ya wananchi wa Iran kwa kisingizio cha kadhia ya nyuklia. Mkuu pamoja na viongozi waandamizi wa vyombo vya mahakama hapa nchini walikwenda kuonana na Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei jana Jumanne, wakati huu wa kuwadia siku lilipotokea shambulio la kigaidi tarehe 28 Juni 1981 mjini Tehran. Kikundi cha Munafiqin cha MKO kilitega bomu kwenye ofisi kuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu mjini Tehran, na kupelekea kuuawa shahidi Ayatullah Muhammad Husseini Beheshti, Mkuu wa Mahakama Kuu kwa wakati huo, na wafuasi wengine wasiopungua 72 wa Mapinduzi ya Kiislamu, wakiwemo mawaziri na wabunge. Akizungumzia kadhia hiyo mbele ya viongozi wa Vyombo vya Mahakama, Ayatullah Khemenei amesema kuwa, jinai hiyo ilionyesha wazi sura  halisi ya kundi la  kigaidi la MKO na washirika wake wa Kimagharibi mbele ya jamii ya wananchi wa Iran na kufuta kabisa uwezekano wa kufufuka tena kikundi hicho hapa nchini.  Kwenye sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliuelezea uchaguzi wa rais uliofanyika Juni 14 hapa nchini, kwamba ulikuwa wa hamasa kubwa kwa maana halisi ya neon, kwani hata Marekani na waitifaki wake walilazimika kuukubali ukweli huo. Viongozi na hata vyombo mbalimbali vya kupasha habari vya Marekani, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani kwa zaidi ya  mwaka mmoja nyuma, vilianza kufanya propaganda na njama kubwa za kuwashawishi  wananchi wa Iran wasijitokeze kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura. Nchi hizo za Magharibi zilikuwa zikiamini kwamba, propaganda hizo zingeweza kuwavunja moyo wananchi na hatimaye  kuwafanya waususie uchaguzi huo Amma kinyume na walivyofikiria viongozi wa Magharibi, uchaguzi wa rais hapa nchini umefanyika kwa uwazi kabisa na katika anga ya amani kikamilifu na wananchi wa Iran walionyesha hamasa kubwa ya kisiasa kwa kujitokeza kwa wingi mno kwenye uchaguzi huo kwa zaidi ya asimilia 72. Kinyume na matakwa ya viongozi wa Magharibi, baada ya kufanyika uchaguzi huo hakukujitokeza machafuko yoyote, bali  nyendo nzuri, za kiungwana na za kisheria zilizoonyeshwa na wagombea wengine walioshiriki kwenye uchaguzi huo, zilipelekea  kupatikana utulivu na furaha kwa wananchi wa Iran.  Nukta muhimu nyingine inayohusiana na uchaguzi wa Iran ilikuwa ni hii kwamba, hata wale watu  ambao si wafuasi wa  mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, walijitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura, na hiyo inaonyesha kuwa wananchi hao wana imani kamili na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na viongozi wake. Sehemu nyingine ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ilijikita kwenye shughuli za nyuklia za Iran zinazofanyika kwa malengo ya amani.  Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Marekani na waitifaki wake kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wametoa maazimio kadhaa yasiyo ya kisheria dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo amani. Kama alivyoelezea Kiongozi Muadhamu, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, umebainisha wazi kwenye hati ya maandishi kwamba, masuala ambayo yalikuwa kwenye miradi ya nyuklia ya Iran yameshatatuliwa. Iwapo Marekani na waitifaki wake wa Ulaya wangeliiangalia kadhia ya nyuklia ya Iran kwa mtazamo wa kitaalamu, basi faili la nyuklia la Iran lingelikuwa limeshafungwa kitambo nyuma. Uhakika wa mambo ni kwamba baadhi chache ya Magharibi, ambazo zinajipachika jina la jamii ya kimataifa zimeifanya kadhia ya nyuklia ya Iran kuwa kisingizio cha kushadidisha mashinikizo dhidi ya  mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Uzoefu katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja unaonyesha kuwa, madola ya kibeberu ya Magharibi yanaichukulia kadhia ya nyuklia ya Iran  pamoja na masuala ya  demokrasia na haki za binadamu, kama wenzo na kisingizo tu cha kuendeleza siasa zao za kiadui  na za kujitanua, dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran. Lakini nchi hizo za Magharibi zinapaswa kuelewa kwamba,  uadui, vita vya kisaikolojia, vitisho na vikwazo, kweli vinaweza kupunguza kasi ya maendeleo ya wananchi wa Iran, lakini kamwe haviwezi kusimamisha kikamilifu juhudi  na maendeleo za wananchi wa taifa hili kubwa.


 IRAN HAITOSALIMU AMRI MBELE YA UBABE WA MAREKANI.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema maandamano ya kila mwaka ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni mithili ya dharba nzito inayowashukia maadui na wapinzani wa taifa la Iran na kusisitiza kwamba mwaka huu pia hivyo ndivyo ilivyokuwa. Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo asubuhi mbele ya umati mkubwa wa maelfu ya wananchi wa mkoa wa Azarbeijan waliokwenda kuonana naye kwa mnasaba wa kumbukumbu ya Februari 18 mwaka 1978 ya mapambano ya wananchi wa mji wa Tabriz. Sambamba na kuwashukuru tena wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kwa izza na adhama katika maandamano ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema ikiwa shukurani hizo zitatolewa tena na tena litakuwa ni jambo la sawa pia na kwamba inapasa kuonyesha taadhima mbele ya moyo wa hamasa na basira yaani uono wa mbali walionao wananchi wa Iran.

Katika hotuba yake hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha mwenendo na kauli zisizo za kimantiki za viongozi wa Marekani juu ya suala la kufanya mazungumzo na Iran mkabala na mwenendo wa kimantiki wa taifa na Mfumo wa Kiislamu juu ya suala hilo. Amesema viongozi wa Washington ni watu wasio na mantiki ambao kauli na vitendo vyao vinagongana na wana hulka ya ubabe na utumiaji mabavu. Ayatullah Khamenei amesema, kama walivyofanya baadhi ya watu, mategemeo ya Wamarekani ni kuona watu wengine pia wanasalimu amri mbele ya matakwa yao yasiyo ya kimantiki, ubabe na utumiaji wao wa mabavu, lakini taifa la Iran na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hautosalimu amri kwa sababu una mantiki, uwezo na nguvu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matamshi yaliyotolewa siku chache zilizopita na Rais wa Marekani kwamba nchi hiyo itahakikisha inaizuia Iran isiunde silaha za nyuklia na akasisitiza kwamba lau kama Iran ingekusudia kuunda silaha za nyuklia Marekani isingekuwa na uwezo katu wa kulizuia taifa la Iran lisifanye hivyo. Kuhusiana na madai ya viongozi wa Washington ya kuwa na nia njema ya kutaka kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Iran, Ayatullah Khamenei amesema kuacha Marekani ubabe, uadui na utumiaji mabavu, kuheshimu haki za taifa la Iran, kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Iran kama ilivyodhihirika kwa uwazi kabisa katika kuunga mkono kwake wafanya fitina za baada ya uchaguzi wa mwaka 2009 na kuacha kuchochea moto wa vita katika eneo ni miongoni mwa ishara ambazo kama zitajitokeza zinaweza kuwa dalili ya kuwa na nia njema viongozi wa Marekani.



HAKI YA NYUKLIA YA IRAN INAPASA KUTAMBULIWA.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Marekani na washirika wake wanapaswa kutambua haki ya Iran ya kunufaika na teknolojia ya atomiki kwa matumizi ya amani. Akiwahutubia wananchi wa mji mtukufu wa Mashhad, Ayatullah Ali Khamenei sambamba na kubainisha kuwa taifa la Iran linafuatilia haki yake ya kawaida tu ya kutumia nishati hiyo kwa malengo ya kiraia, amesema Marekani na washirika wake pia kama zilivyo nchi nyingi duniani wanapaswa kuitambua haki hiyo na kuikubali. Aidha amesisitiza kwamba Marekani haina nia ya kweli ya kutatua kadhia ya nyuklia ya Iran kupitia mazungumzo na kundi la 5+1 na kuongeza kuwa, mara kadhaa pande husika zimefikia mwafaka katika nukta za pamoja lakini Marekani kila mara imekuwa ikiweka pingamizi na kuzuia kupatikana mafanikio. Kiongozi Muadhamu aidha amesema, iwapo Wamarekani kweli wanataka kuondoa hitilafu zao na taifa la Iran kwa njia ya mazungumzo, basi wanapaswa kwanza kuacha uadui wao kwa taifa hili na kuthibitisha kwamba wana nia njema katika suala hilo. Ayatullah Khamenei pia ameashiria matamshi yanayotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kushambulia taasisi za nyuklia za Iran na kusema kuwa, Israel inajua na kama haijui inapaswa kutambua kwamba, iwapo itajaribu kufanya hivyo makombora ya Iran yataisawazisha na udongo miji ya Tel Aviv na Haifa.



MWAKA WA HAMASA YA KISIASA NA HAMASA YA KIUCHUMI.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutangaza mwaka mpya wa 1392 Hijria Shamsiya kuwa, 'Mwaka wa Hamasa ya Kisiasa na Hamasa ya Kiuchumi' kwa taifa la Iran.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei katika ujumbe wa Nowruz alioutoa kwa mnasaba wa kuanza mwaka 1392 Jumatano ya leo, ameashiria harakati ya kusonga mbele taifa la Iran mwaka uliopita hasa katika makabiliano ya kisiasa na kiuchumi na ulimwengu wa kiistikbari. Amesema uono wa mwaka 92 ni wa matumaini sambamba na ustawi, harakati  na ushiriki wa kijihadi wa taifa la Iran katika nyuga za kisiasa na kiuchumi. Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema kuwa ana matumaini kuwa kwa rehema zake Allah SWT, hamasa ya kiuchumi na hamasa ya kisiasa itaweza kufikiwa na wananchi pamoja na maafisa wa serikali  wenye kuupenda mfumo.

Kiongozi Muadhamu amesema kile ambacho kilijiri katika mwaka 1391 ambao umemalizika leo ni makabiliano ya wazi ya Iran na ulimwengu wa istikbari ambao ulidhirisha uhasama na uadui dhidi ya taifa la Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kiongozi Muadhamu amesema maadui wa Iran walitangaza kuwa wanataka kulilemaza taifa la Iran kupitia vikwazo lakini si tu kuwa hawakuweza bali kinyume na hilo, kwa taufiki na uwezo wake Allah SWT, taifa la Iran limeweza kupata mafanikio mengi sana. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei katika ujumbe wake wa Nowruz ameongeza kuwa, si tu kuwa maadui hawakuweza kuitenga Iran kieneo na kimataifa bali pia natija kinyume ya njama zao ilibainika pale kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamna na Siasa za Upande Wowote NAM waliposhiriki katika kikao kilichofanyika hapa mjini Tehran. Amesema kikao hicho kilionyesha kuwa Iran haijatengwa na kwamba dunia inaitazama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa heshima na taadhima. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa mwaka mpya wa 1392 Hijria Shamsiya ni mwaka wenye upeo wa matumaini na kwamba kwa taufiki ya Allah SWT na kwa hima ya taifa la Waislamu utakuwa mwaka wa ustawi na maendeleo ya taifa la Iran. Amesema hilo halimaanishi uhasama wa maadui utapungua bali linamaanisha kuwa taifa la Iran liko tayari kujitokeza katika kujenga mustakabali bora na wenye matumaini kwa taifa hili kwa kujitegemea, Insha Allah. Kuhusiana na uchaguzi ujao wa rais utakaofanyika mwezi Juni, Kiongozi Muadhamu amesema, Insha Allah watu wa Iran watajitokeza kwa wingi katika medani na kuweza kuainisha mustakabali mwema wa nchi na wao binafsi.



WANAWAKE WAISLAMU IRAN NI KIGEZO KIPYA.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema mwanamke Mwislamu Muirani ana nafasi ya kihistoria katika kuarifisha kigezo kipya cha mwanamke.

Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo katika ujumbe wake uliosomwa katika 'Kongamano la Mashahidi Elfu Saba Wanawake' ambalo limefanyika Jumatano mjini Tehran. Ameashiria mtazamo wa mwanamke katika mifumo ya Mashariki na Magharibi duniani ambapo mwanamke anatazamwa kama kitu cha pembeni au chombo cha kutumiwa kijinsia na mwanaume. Amesema nafasi ya mwanamke Muirani iliibua kigezo kipya katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu na Kujihami Kutakatifu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mwanamke Mwislamu Muirani ameweza kuthibitisha kuwa anaweza kudumisha utambulisho wake wa kike, kuwa afifu, kuzingatia hijabu na heshima sambamba na kushiriki katika uga wa kisiasa na kijamii na kupata mafanikio makubwa. Ayatullah Khamenei amesema maadamu wanawake katika Ulimwengu wa Kiislamu wanawachukulia kama vigezo bora wanawake wa mwanzoni mwa Uislamu kama vile Bibi Khadija AS na bintiye mtukufu Bibi Fatimatu Zahra SA na Zainab Kubra SA  basi njama zote za kale na mpya dhidi ya wanawake zitafeli na kushindwa.



UISLAMU UNAHIMIZA KUPANDA MITI.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja mimea na miti kuwa chimbuko la ustawi na Baraka kwa nchi zote na jamii ya mwanaadamu.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo Jumanne mjini Tehran kwa mnasaba wa ‘Wiki ya Mazingira na Kupanda Miti’. Baada ya kupanda miche miwili, Kiongozi Muadhamu amesema kuwa kulinda miti na kuzuia uharibifu wa miti ni kati ya mambo yaliyosisitizwa katika dini tukufu ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuhusu udharura wa kuwepo azma na irada imara ya kuzuia unyakuzi wa maeneo yenye misitu kando ya miji mikubwa. Amesema, malalamiko yake kwa wanaoshusika na masuala ya miti na upandaji miti ni kuwa mamia ya miti inakatwa katika maeneo ambayo haipaswi kukatwa. Kiongozi Muadhamu amesema kuharibiwa maeneo ya kijani katika vitongoji vya miji hasa misitu ni mambo ambayo yanamsababishia mwanaadamu matatizo mengi na hivyo wahusika wote nchini Iran wanapaswa kuchukua hatua za kuzuia uharibifu wa misitu. Wakati huo huo Rais Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran naye pia ameongeza shughuli ya kupanda miti katika Ikulu ya Rais mjini Tehran. Katika shughuli hiyo mabalozi na wawakilishi wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM wamepanda miti katika ‘Bustani ya NAM’ iliyoko kwenye viwanja vya Ikulu hapa mjini Tehran.



WAZAYUNI WANAZUSHA HITILAFU KATIKA UMMA WA KIISLAMU.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa matatizo mengi ya Umma wa Kiislamu ni matatizo ya kutwishwa na yaliyobuniwa na maadui wa Uislamu. Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan aliyeko safarini hapa nchini na kuongeza kuwa, kuhuishwa uwezo na vipawa vya kibinadamu, kimaumbile na kijiografia vya ulimwengu wa Kiislamu kunaweza kuwa na taathira kubwa katika kuondoa matatizo hayo.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa kuimarishwa na kupanuliwa zaidi uhusiano wa nchi za Kiislamu ni sababu ya pili muhimu inayoweza kusaidia juhudi za kutatua matatizo ya Waislamu. Ameongeza kuwa moja ya malengo ya Wazayuni na mabeberu wengine ni kuzusha hitilafu na mifarakano katika Umma wa Kiislamu.

Ameashiria uhusiano mzuri na wa kidugu uliopo kati ya Iran na Pakistan na akasema: "Tunaamini kwamba uhusiano wetu wa kiuchumi, kimiundombinu, kisiasa, kijamii na katika masuala ya usalama unapaswa kuimarishwa zaidi."

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa bomba la kusafirisha gesi kati ya Iran na Pakistan ni mfano mzuri wa ushirikiano wa Tehran na Islamabad. Ameashiria uadui na upinzani uliopo dhidi ya uhusiano mzuri wa nchi hizo mbili na akasema kuwa, kuna ulazima wa kuvuka upinzani huo kwa nguvu zote.

Amesema suala la kupata chanzo cha kuaminika na thabiti cha nishati lina umuhimu wa daraja la kwanza kwa nchi yoyote ikiwemo Pakistan na kuongeza kuwa, katika eneo hili Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi pekee yenye vyanzo vya kuaminika vya nishati na iko tayari kukidhi mahitaji ya Pakistan katika uwanja huo.

Ayatullah Ali Khamenei amekitaja kitendo cha kuzusha hitilafu za kimadhehebu nchini Pakistan kuwa ni vijidudumaradhi hatari kutoka nje ya nchi hiyo. Amesema kuwa mauaji yanayofanywa dhidi ya wafuasi wa madhehebu tofauti nchini Pakistan yanasikitisha mno na kuna udharura wa kukabiliana nayo ili yasivuruge umoja wa kitaifa wa Pakistan.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ana matumaini kwamba serikali ya Pakistan itatatua matatizo hayo na kuongeza kuwa, anatarajia kuwa serikali ya Rais Asif Ali Zardari itaimarisha umoja kati ya madhehebu na kaumu tofauti na kupata mafanikio katika masuala ya ustawi.

Kwa upande wake Rais Asif Zardari wa Pakistan ameeleza kufurahishwa kwake na kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na akasema kuwa anaamini kwamba uhusiano wa pande hizo mbili unapaswa kuimarishwa zaidi.

Rais wa Pakistan amesema kuwa njama za madola makubwa za kutaka kuzuia juhudi za kuimarishwa uhusiano wa Iran na Pakistan zimegonga mwamba kwa sababu mataifa hayo mawili yameelewa jinsi ya kukabiliana na maadui wa Uislamu.

Asif Zardari amesema kuwa maadui wanafanya njama za kuanzisha vita vya ndani nchini Pakistan na kuongeza kuwa serikali yake haitaruhusu njama hizo.