AYATULLAH YAZDI, MKUU WA BARAZA LA WATAALAMU IRAN.

Ayatullah Mohammad Yazdi amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Mwanazuoni huyo ambaye alikuwa mkuu wa vyombo vya mahakama vya Iran kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 amechaguliwa kuongoza baraza hilo leo Jumanne kwa kupata kura 47 kati ya 73. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran Ayatullah Ali Akbar Hashemi Rafsanjani pia aliwania uenyekiti huo na kupata kura 24 huku kura mbili zikibatilishwa.
Kura hiyo imepigwa baada ya kuaga dunia mwenyekiti wa zamani wa baraza hilo, Ayatullah Mohammad-Reza Mahdavi Kani miezi mitano iliyopita. Baraza la Wataalamu humchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Wajumbe wote 86 wa baraza hilo huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi na huhudumu kwa muhula wa miaka minane. Baraza hilo huitisha kikao mara mbili kwa mwaka na kumteua mwenyekiti mpya.
Kikao hicho cha leo pia kimehutubiwa na waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ambaye amewasilisha ripoti kuhusu mkondo wa mazungumzo ya nyuklia na nchi za 5+1. Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/…/47260-ayatullah-yazdi,-mwenyekit…