SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMAH (A.S):


Bismillah Arrahman Ar-rahim:
Assalaam alaikum Ndugu Waislam:

Hazrat Fatimah (a.s) alikuwa binti wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) Nabii wa Uislamu kutoka kwa mke wake wa Kwanza Bi Khadijah bint Khuwaylid.
Waislaam wote humuona Sayyidat Fatimah (a.s) kama mfano bora kwa wanaume na wanawake.
Alipenda ibada,alipenda watu wote,na zaidi alipenda kuwasaidia masikini na kamwe hakuridhika jirani yake alale kwa njaa,aliona ni bora ampatie kila alichonacho maskini au jirani yake ale na huku yeye akishinda na njaa au kulalia maji tu.
Familia hii ilikuwa familia bora sana ambayo inakosa mfano wake,iliwalisha masikini kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu (s.w) pasina kuhitajia malipo wala shukran.Allah anasifu kitendo hicho katika Qur'an Tukufu kwa kusema:"Hakika sisi tunakulisheni (chakula) kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu (s.w) hatutaki -kutoka kwenu- malipo wala shukrani".
(Tazama: Suuratul-Insaani: Aya ya 9.)

Haya ndio maneno yaliyokuwa yakisemwa na Bi Fatimah (s.a) na Familia yake tukufu (a.s). Bi Fatimah (s.a) amekusanya sifa bora na nyingi sana katika kila sekta kiasi kwamba tutahitaji karatasi za kutosha na kalamu za kutosha na muda wa kutosha ili kuweza kuzitaja na pasina kuzimaliza.
Historia ya kiislaam inamtambua Bibi huyu kama Mwanamke mwenye Elimu pana kuliko wanawake wote wa zama,mwenye uchamungu,mwenye zuhdi,mpole mwenye huruma,mwenye kumtii mume wake,Mama bora na sifa nyingine nyingi.
Bi Fatimah (s.a) ,Mtume (s.a.w.w) alipenda sana ambapo mara kwa mara alinukuliwa akisema:
"Fatima anatokana na mimi(yaani ni sehemu ya nyama yangu) atakaye muudhi (atakuwa) ameniudhi mimi" .
(Tazama: Sahihi Bukhari: Juzu 4 ukurasa wa 210).
Hadithi hii tukufu tukiitafakari na kuizingatia,tutaikuta ni hadithi ambayo inataka kutueleza au inatueleza kwamba Fatimah (s.a) ni sehemu ya wujud wa Mtume (s.a.w.w).Na ndio maana Mtume (s.a.w.w) akasisitiza zaidi kwa kusema:
"Kinanitia wasi wasi kinachomtia wasi wasi (Fatima),na kinaniudhi kinachomuudhi (Fatima)". (Tazama Sahihi Bukhari:Juzu ya 4:Ukurasa wa 210).
Hivyo Ghadabu za Bi Fatimah (s.a) kwa mujibu wa hadithi hii Uislam unazitambua kuwa ni Ghadhabu za Mtume (s.a.w.w), na ghadamu za Mtume (s.a.w.w) ni ghadhabu za Mwenyeezi Mungu (s.w), na hivyo hivyo kinyume chake.
((Tazama: Al-mustadrak ala-sw-swahiyhayn, juzi 3, ukurasa wa 154.))
Bibi Fatimah (s.a) baada ya maisha ya baba yake hakubahatika kuishi tena maisha ya furaha, alisongwa sana na maudhi, manyanyaso na vitendo vya dhulma kutoka kwa wale ambao historia ya kiislaam imewatambua kwa uovu uliopindukia.
Kutokana na maudhi hayo yaliyoambatana na kudhulumiwa urithi wake na kuchomewa nyumba yake moto, Bi Fatimah (s.w) alifikia hatua ya kutamani mauti na kuachana na maisha haya ya dunia, akiwa katika kaburi tukufu la Mtume (s.a.w.w) alisikika akimuomba Mola wake akisema:
"Ewe Mola wangu! Nakuomba uharakishe kifo changu",
Pia alisikika akiyasema maneno haya yafuatayo:
صُبَّتْ عليَّ مصائبٌ لو أَنَّها صَُّبَّتْ على الأيام صرنا لَيالياً
"Mvua ya mabaya iliyoninyeshea baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w),laiti kama mvua hiyo ingeliukumba mchana, basi ungelibadilika na kuwa usiku".

(Tazama: Biharul-anwaar: Juzu ya 43, ukurasa wa 177, na Juzu ya 79, ukurasa wa 106.)
Hakika huzuni ya Bi Fatimah (s.a) ilikuwa haina mfano na niya milele.
Alidumu katika huzuni tangu baba yake kufariki, muda wote alionekana akimtetea Amirul Muuminina, Ali bin Abi Talib (a.s) dhidi ya wale walioamua kumdhulumu na kumfanyia uadui, akiwa katika hali ya kumhamia Mume wake Ali (a.s), ndipo alipojeruhiwa na watu hao, ambapo tukio hilo hatimae likasababisha mauti yake ya kishahidi miezi michache baada ya baba yake.
Bi Fatimah (s.a) alimuusia Mumewe Amirul-Muuminina , Ali bin Abi Talib (s.a) amuoshe na kumvalisha sanda usiku, pamoja na kumswalia na kumzika usiku,pia akamtaka asimjulishe yeyote.
Imam Ali (a.s) alitekeleza wasia huo na kumzika katika sehemu ya Ardhi tukufu inayoitwa Jannat al-Baqi' , Katika mji Mtukufu wa Madina lilipo kaburi tukufu la Imam Hasan bin Ali bin Abi Talib (a.s).
Na eneo halisi la kaburi la Bi Fatimah (s.a) halijulikani kwa watu wengi bali kwa watu wote.Hakika huu nao ni msiba wa aina yake ulioingiza huzuni katika nyoyo za waislaam walio wengi tangu zama hizo hadi leo hii.
Wapenzi wa Fatimah (s.a) na Ahlul-Bayt (a.s) kwa ujumla kamwe hawakusahau na hawatasahu msiba huu mkubwa ulioambatana na dhulma kubwa kwa binti pekee ya Mtume (s.a.w.w) Nabii wa Uislaam.
Wafuasi na wapenzi wa Ahlul Bayt (a.s) kila mara huonekana katika mavazi maalum yanayoashiria kuomboleza na kukumbuka kifo hiki cha kishahidi,huku wakikusanyika katika majlisi na vikao mbali mbali kwa lengo la kukumbushana kunako maisha ya Bi Fatimah (s.a) na shahada yake.Na daima husikika wakitamka kauli hii:
"Kamwe hatutakusahau,na hatutaisahau dhulma iliyojiri kwako", na ikiwa tutakuwa ni wenye kusahau,basi tutasahau yote lakini "si ule moyo uliojaa huzuni,na mwili uliojaa maumivu,na kaburi lisilojulikana lilipo..." Mpaka atakapo hukumu Mwenyeezi Mungu, Naye ni mbora wa wenye kuhukumu."
(Tazama: Suuratul-Yunus: Aya ya 10)

*و سيعلم الذين ظلموا أيّ منقلب ينقلبون*
Washukran.
Na Sheikh Taqee.