NINI MAANA YA HARAKATI NA NANI MWANAHARAKATI.?


Katika miaka ya hivi karibuni neno mwanaharakati limeshika kasi sana miongoni mwa vijana wa Kiislamu. Kila kijana wa kiislamu anataka kuitwa kwa jina hilo bila kutambua yeye ni wanaharakati gani na harakati zake zinalengo nini.
Msiba mkubwa zaidi ni pale unapomtaza huyo anayeitwa kiongozi wa hizo harakati na kumkuta ni mtu ambaye hana sifa ya uana harakati wala yeye mwenyewe hajitambui achilia kuutambua Uislamu wake. Kuna baadhi wana dhana kwamba ili uhesabike kuwa mwanaharakati lazima ujiunge na chama fulani cha kiasiasa.
Baadhi yetu tunadhani maana ya harakati ni kuwa na maneno makali na kutokuwa na adabu. Lakini wengine wanafikiri mwanaharakati ni mtu jasiri wa kupambana na viongozi wa Serikali, kuandamana, kuteka misikiti na kukufurisha Waislamu wasiofuata itikadi yake na kutangaza chuki na uadui kwa watu wa dini na madhehebu yasiyokuwa ya Kiislamu.
Lakini kabla ya kwenda mbali, turudi kwenye mada ya msingi. Nayo ni  ‘’nini maana ya harakati na nani mwanaharakati?’’ Je! harakati hulenga nini na kuanza wakati gani na kwa sababu gani? Tunaweza kueleza harakati zinazotambulika na dini ya Kiislamu kwa kuanza na kauli ya Mwenyezi Mungu (SW) akisema ndani Qur’ani tukufu kuwa:
 “Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa jamii (kaumu) mpaka wao wenyewe (wanajamii) wabadili yaliyomo ndani ya nafsi zao”.  (Ku 31:11)

Aya hiyo inasimamisha msingi wa harakati. Kwa mujibu wa aya hiyo harakati ni mapinduzi yanayolengwa kufanywa na jamii dhidi ya mfumo unaotawala au uliozoeleka ili kuleta mabadiliko yanayohitajika katika jamii. Ukipenda unaweza kuyaita mapinduzi au mabadiliko yanaweza kuhitajika katika nyanja zinazogusa uhai wa jamii kama vile kilimo, uchumi, siasa, utawala n.k.
  Aya tuliyoisoma inasema mabadiliko hayawezi kutokea kama miujiza. Ni lazima yaletwe na wanajamii wenyewe, na hatua ya kwanza kabisa ni watu kujenga chuki dhidi ya mfumo mbaya unaowakera. Hatua ya pili ni kufanya azma ya kuubadili mfumo huo ili kuleta mfumo ulio bora zaidi.
 Hatua ya tatu ni elimu ya ujuzi wa manufaa au madhara yatokanayo na juhudi za kutafuta mabadiliko hayo na njia za kufikia azma hiyo. Maana ni vigumu kuleta mabadiliko yasiyokuwa na gharama. Kusaka mabadiliko yatakayoondoa mfumo uliopo ni sawa sawa na wapigania uhuru katika mataifa yao ambao kuyaweka rehani maisha yao na kuingia katika hatari kwa faida na jamii.
 Aidha harakati ni sawa na jihadi ambayo ni njia ya kujitoa muhanga kwa faida ya umma, na hivyo hivyo katika kuleta mapinduzi ya kijamii dhidi ya mfumo wa kidhalimu, lazima wapatikane watu watakaojitolea uhai wao kwa shabaha ya kuutokomeza udhalimu na mfano mzuri ni namna alivyojitolea Mzee Mandela kwa faida ya jamii yake.
Kufahamu na kutambua shabaha ya harakati zozote zile, kunalazimisha kwanza kuwa na ujuzi wa kutosha juu ya mazingira ya hakika yaliyopelekea kuwepo haja ya kudai mabadiliko. Mdai mabadiliko (mwanaharakati) kwa ujumla, anatakiwa afahamu malengo na natija iliyokusudiwa kupatikana katika harakati hizo.
Lazima awe na imani kamili  juu ya anachokipigania kuwa ni haki, imani ambayo itamfikisha katika kiwango cha kumridhisha na kumfanya kuwa na yakini na kuondoa shaka kabisa. Kujitambulisha kuwa mwanaharakati wa Kiislamu, kunahitaji ujuzi kamili wa malengo yaliyokusudiwa, na kisha kujiridhisha wewe mwenyewe na malengo hayo. Lazima mwanaharakati kwanza awe na ujuzi wa dini yake, ashiriki katika ibada na kuyakataa maasi kwa juhudi zake zote.
Kubwa kuliko yote ni kuwa tayari kuyatumikia malengo yenyewe na kubeba dhamana ya matokeo yake yakiwa mazuri au mabaya. Linalojulikana zaidi ni kuwa, kudai haki daima ni mapambano, maana madhalimu siku zote hawako tayari kutoa haki kwa hiyari, mwana falsafa mmoja alipata kusema. “Haki haiombwi, huchukuliwa”.
Harakati huanzishwa na wanyonge
Mwanafalsafa wa kiajemi Murtadha Mutahhari, akielezea nadharia hii katika mojawapo ya matoleo yake anasema, kuna nadharia mbili zitolewazo kuhusu harakati zozote duniani. Nadharia ya kwanza inasema, mabadiliko yoyote ya kijamii yanayotokea, yana msingi na asili moja ingawa miundo yake ya wazi huonekana kuhitilafiana.
Wanaoamini nadharia hii, wana dhana kwamba msingi na roho inayopelekea kutokea harakati zote ni uchumi na maada. Harakati za kijamii ni mithili ya ugonjwa unaojitokeza kwa dalili tofauti, anasema Mutahhari, lakini Daktari hutambua kuwa dalili zote hizo zinaonyesha chanzo cha tatizo au ugonjwa mmoja.
 Hivyo hivyo, katika harakati mwishowe hubainika wazi kuwa hufanywa na kundi la wanyonge wenye hisia ya kukosa haki, kudhulumiwa na kukandamizwa dhidi ya tabaka la juu hata kama hapo awali taswira hiyo itakuwa haikujitokeza au kugundulika wazi.
Wanaoaminini nadharia ya pili, wanatofautiana na wafuasi wa ile nadharia ya kwanza. Wao wanatakidi kwamba, umaada, yaani maumbile, dunia na mahitaji yake, sio chanzo peke yake. Inayumkinika kabisa kuwa, baadhi ya misingi ya harakati zilizopelekea mapinduzi ya kijamii nyingine zilituama juu ya matatizo ya kiuchumi na kimaisha kulikosababishwa na tofauti ya kitabaka inayotawala katika jamii.
 Yaani tabaka la wanaojidhania kuwa wao ndio mabwana waheshimiwa, wenye haki ya kuishi na kutawala, na hivyo kushikilia maeneo yote ya utawala na uchumi kunakowapelekea kuishi maisha ya starehe na anasa, na tabaka la watawaliwa, raiya wa daraja la chini wenye kukandamizwa na ambao matumbo yao yamerudi mgongoni kwa njaa.
 Kwa mujibu wa wanaoamini nadharia ya pili, si lazima kilichosababisha harakati kiwe ni kugawika matabaka mawili ya kijamii na kiuchumi ya wenye shibe na njaa pekee, kwani huenda uasi unaweza kutokea kutokana na hisia ya utu tu na ukazusha patashika nguo kuchanika katika nchi.
Kuna nadharia nyingi juu ya sababu zinazoweza kupelekea kuzuka kwa harakati za kudai haki. Kuna uwezekano pia harakati zikawa na hisia za kibinadamu endapo zina msingi wa kupigania uhuru na msingi wa siasa, wala siyo zikiwa zina msingi wa uchumi pekee. Kwani inawezekana kuondoa njaa kwa kadri kubwa, lakini wakati huo huo watu wakawa hawana uhuru wa kuabudu, kuhubiri dini zao, uhuru wa kusema, uhuru wa kukosoa na uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe.
Tunajua kwamba mambo haya, hayana uhusiano na mambo ya kiuchumi. Lakini ni ukweli ulio wazi kuwa hakuna harakati zisizoweza kufungamanishwa na sababu hizo, zote kwa pamoja au baadhi yake.
Harakati zenye msingi wa Kidini
Ukiacha misingi miwili tuliyoitaja, harakati huweza pia kuwa na misingi ya kidini. Kwa mfano, ikiwa watu wenye kuamini dini fulani na kuyathamini kwa dhati mafundisho yake, wataona kwamba dini yao na itikadi yao inapigwa vita, inashambuliwa, kubezwa na kupuuzwa, na wao wenyewe wanapoteza haki zao fulani fulani za kiraia, kisiasa na kiutawala na kutengwa kwa sababu ya imani yao, basi hapana shaka watu hao watachukia na kuweka malalamiko mbele ya madhalimu wao kwa lengo la kupinga dhulma hiyo.
Endapo hatua hiyo haitozaa matunda na wakaendelea kudharauliwa, kupuuzwa na kunyanyaswa kwa kuwa hawana nguvu, kitakachofuatia itakuwa ni kuanzisha harakati zenye shabaha ya kupambana dhidi ya wakandamizaji ili kupata haki zao. Katika kipindi chote hicho si rahisi kwa dhalimu kuamka, kwa kuwa tabia ya udhalimu huambatana na kukosa hekima katika kufikia njia ya kutatua tatizo.
 Bali mara zote udhalimu huondokana na hali ya kukosa utu na hekima, na wakati wote kuamini kuwa njia ya kutatua tatizo lolote ni kutumia nyenzo, yaani ubabe kwa kuumia nguvu za utawala na nguvu za vyombo vya dola ili kukandamiza matakwa ya wanyonge.
Mwanzoni mwa kila harakati za namna hiyo ni madai ya haki  yatakayowekwa mbele ya wababe na si vinginevyo, huku watawala wakiendelea ukaidi kwa kutumia njia za mabavu kuwanyamanzisha wanyonge. Lakini kadri siku zinavyoendelea na haki haipatikani, na dhalimu kuzidisha vitendo vya ukatili, wanyongea nao  hugeuza mwelekeo.
 Badala ya kutishika na kurudi nyuma, wanaamua kujitoa mhanga maisha yao ili haki ipatikane. Wanafanya hivyo ili waweze kwa vyovyote vile kuhifadhi na kuyalinda mafundisho ya dini yao na utu wao. Hali ifikiapo kiwango hicho uasi hauwezi kuzuilika tena ila kwa kuporomoka udhalimu au kupatikana haki zinazodaiwa hata kama itachukua muda mrefu. Qur’ani tukufu inawahimiza wanyonge kutorudi nyuma:-
 “Na piganeni nao mpaka kusiwepo uonevu na dini iwe kwa ajili ya Allah tu”. (2:193).
Ni katika hatua kama hizo tunaweza kuyazungumzia mapinduzi makubwa yaliyoletwa na Mtume Muhammad (SAW), Mapinduzi makubwa ya Ufaransa, mapambano ya kudai haki ya heshima ya mwanadamu huko Afrika Kusini, mapambano ya kudai uhuru wa Taifa la Palestina, mgogoro wa Lebanon ulioishia kwa kuundwa katiba, mapinduzi ya mwaka 1979 ya  Iran.
Wananchi wa nchi hizo walijitoa mhanga ili kudai haki zao kama raia na binadamu zitambulike na kuheshimiwa, na kwamba wao hawakuumbwa na Mwenyezi Mungu ili kuwa raia wa daraja la pili la wanyonge wenye  kutawaliwa daima na kubaguliwa, kunyanyaswa  na kutengwa.
Harakati zinazofanywa na watu wenye nia na malengo kama hayo tuliyoyataja, hazina chanzo cha siasa na utawala, njaa au shibe, wala uhuru wa kisiasa. Lakini kwa kuwa hawapewi fursa ya kutekeleza malengo ya dini yao, huwajibika kuanzisha harakati.  Harakati hizo huenda zikafikia hatua ya kusababisha kuanguka kwa utawala wa kidhalimu, maana udhalimu ndicho kikwazo, na hapo yanakuwa yamefanyika mapinduzi.
Historia inashuhudia kuwa ni vigumu watawala kutoa haki za wanyonge, jambo ambalo huwafikisha katika hatua ya kufanya vitendo vya mauaji na ukatili kuwatisha watawaliwa. Vitendo vya ukatili vinaposhamiri huimarisha mioyo ya wanyonge kujitoa mhanga zaidi kuliko kutishika na mwishowe hapana njia ila kuangamia madhalimu na mfumo wao. Qur’ani tukufu katika sura ya 71 aya ya 28 inatoa hakikisho kuwa, mwisho wa madhalimu ni kuangamia ikisema:
 ‘’Wala usiwazidishie madhalimu ila maangamio’’
Ukiangalia kwa makini nadharia zote tulizozitaja, utaona kwamba sisi Waislamu tunaodai kuwa wanaharakati wa Kiislamu, bado tuna matatizo ya kuelewa harakati zetu zinalenga shabaha gani. Wengi miongoni mwetu tukitakiwa kujibu swali kwamba, nyinyi Waislamu wa Tanzania mna matatizo gani? Ni haki gani mnazodai? Na mnamdai nani haki hizo?
 Majibu ya maswali yote haya ni rahisi mno kuyajibu. Lakini lililo gumu zaidi ni kujua ni njia gani ya kufikia suluhu juu ya matatizo yote hayo. Ukweli wenyewe ni kuwa elimu ya kutosha inahitajika kwa Waislamu ili kwanza, kujua maana ya harakati na shabaha zake.
Haja ya elimu kwa umma ni kubwa sana lakini nalo lina changamoto ya msingi nayo ni hii kwamba, nani atoe elimu hiyo wakati sisi tunaojiweka mbele kama viongozi wa harakati hatuna hata elimu ya msingi juu jambo husika?  na baya zaidi tumejenga uadui na hasama na wale ambao wana sifa za kutuongoza?
Pili, tunahitaji kujua ni njia gani iliyo sahihi katika kufikia hatua ya kupata jawabu linalofaa. Ni vigumu mtu kupata ufumbuzi juu ya tatizo analolifikiria tu bila kulitambua kwa ukamilifu. Na ni vigumu zaidi kwa tatizo la kijamii linalohitaji nguvu za pamoja, kupata ufumbuzi katika kipindi ambacho jamii husika imo katika mfarakano na kutotambuana.
 Leo tuna viongozi wengi wa makundi yaliyozuka hivi haribuni, ambao hawana mlingano wowote mahala walipo, zaidi ya kuwachochea wafuasi wao kuwatukana, kuwazomea, kuwakejeli na kuwavunjia heshima viongozi na Masheikh wengine wanaotofautiana nao katika masuala ambayo si ya msingi. Imetolewa  na Sheikh Khalifa Khamis