SHEREHE YA KUKUMBUKA MAZAZI YA MTUKUFU MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W), YAMEFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM KATIKA VIWANJA VYA MNAZI MMOJA.

Waumini wa dini ya Kiislam wakiwa katika viwanja vya Mnazi mmoja, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukumbuka mazazi ya Mtukufu wa daraja Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Kuwakusanya watu kwa ajili ya sherehe ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni kuitukuza sifa zake ambazo zimesifiwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t). Nabii Isa (a.s) alimuomba Mwenyezi Mungu amteremshie meza ya chakula, na siku hiyo ya kuteremshwa meza ya chakula akaitaja kuwa ni sikukuu: "Ee Mwenyezi Mungu Mola wetu! tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu na kiwe ishara itokayo kwako, na turuzuku, kwani wewe ni mbora wa wanaoruzuku". 5:114.

Je. thamani ya kuwepo Mtume Mtukufu, ni ndogo kuliko meza ya chakula iliyotoka mbinguni ambayo Nabii Isa (a.s) ametangaza siku ya kuteremshwa chakula hicho kuwa ni sikukuu? Ikiwa kufanywa siku hiyo sikukuu ni kwa sababu chakula ilikuwa ni ishara ya Mwenyezi Mungu, Basi Je, Mtume Muhammad (s.a.w.w) si ishara kubwa kabisa ya Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu anamteremshia rehema Mtume, na Malaika wake wanamteremshia rehema Mtume, enyi mlioamini! Muombeni rehema (Mtume) na muombeni amani". 33:56 iliposemwa Aya hii, Maswahaba waliuliza Mtume: Watamuombeaje rehema? Mtume akawafundisha, semeni: Allahumma swali a'laa Muhammad wa Aali Muhammad. Hili ni muhimu sana kuliewa, kwa sababu, wako watu wengi wanapomuombea rehema Mtume husema: Swallallahu Alayhi wasallama. Hili ni kosa kubwa kabisa, kwa sababu Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) hakufundisha hivyo. Bali amesisitiza akisema: "Msiniombee rehema kwa kunikata, mkisema: Allahumma swali A'laa Muhammad, mna nyamaza, lakini semeni: Allahumma swali A'laa Muhammad wa Aali Muhammad.

Rejea: Naylul Awtaari J. 2 uk. 287, Sablus Salaami J. 1 uk. 326, Yanabiiul Mawadda J. 1 uk. 6