SERIKALI YA IRAN HAITOSAINI MAKUBALIANO YOYOTE NA NCHI ZA MAGHARIBI.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo kuwa serikali yake haitosaini makubaliano yoyote ya nyuklia na nchi za Magharibi iwapo makubaliano hayo yatalazimisha kupekuliwa vituo vya kijeshi na vya kisayansi hapa nchini. Akiashiria kauli ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, Rais Rouhani amesema vituo vya kisayansi, wanasayansi wa nyuklia pamoja na vituo vya kijeshi ni mstari mwekundu kwenye mazungumzo yanayoendelea ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1. Hapo jana Jumatano, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kwamba, Wamagharibi wameanza kutoa masharti mapya ya kutaka waruhusiwe kufanya uchunguzi kwenye kambi za kijeshi na zile za kisayansi chini ya makubaliano ya mwisho ya nyuklia na kusisitiza kwamba suala hilo kamwe halitokubaliwa na Iran.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imesema hakuna makubaliano yoyote yatakayosainiwa na Iran hadi pale matakwa yake yote yatakapotekelezwa ikiwa ni pamoja na kuondolewa vikwazo vyote vya Wamagharibi kwa wakati mmoja.


MAREKANI INASHIRIKIANA NA ISRAEL KUTENDA JINAI PALESTINA.
Naibu Spika wa Bunge la Palestina amesema kuwa, Marekani inashirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya jinai dhidi ya Wapaletina.
Kituo cha Upashaji Habari za Palestina kimemnukuu Bw. Ahmad Bahar akililaumu Baraza la Congress la Marekani kwa kupasisha muswada wa kuuzatiti kwa silaha utawala wa Kizayuni ikiwa ni pamoja na kuupa utawala huo katili, silaha kali zenye thamani ya dola bilioni mbili za Kimarekani.
Amesema hatua hiyo ya Baraza la Congress la Marekani ni kushiriki moja kwa moja katika jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.
Ameongeza kuwa misaada ya silaha ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni ambazo zinajumuisha maelfu ya mabomu ya kuharibia mahandaki na ngome za kivita kuna maana ya kuuliwa shahidi na kujeruhiwa mamia ya wananchi wasio na hatia, wa Palestina. 

MAREKANI INATAKA KULIPIZA KISASI KUPITIA MAZUNGUMZO.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa mjini Tehran amesema kuwa, Marekani inatafuta njia ya kulipiza kisasi dhidi ya taifa la Iran kupitia mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea kati ya taifa hili na kundi la 5+1. Ayatullah Ahmad Jannati amesema hayo leo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Sala ya Ijumaa na kubainisha kwamba, kwa miaka mingi Marekani imepata pigo kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu na Uislamu na sasa inatafuta njia ya kulipiza kisasi katika mazungumzo ya nyuklia. Ayatullah Jannati amesema, ni kuwa na fikra finyu endapo mtu atadhani kwamba, kufikiwa makubaliano ya nyuklia kutahitimisha njama za maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Jannati amesema kuwa, kumuamini Mwenyezi Mungu, kuwa na imani na wananchi na kuendeleza njia ya Uislamu ni misingi mikuu mitatu muhimu katika mazungumzo na madola ya Magharibi ambayo inapaswa kuzingatiwa na timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran. Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesisitza kuwa, kuwa na matumaini na Marekani katika mazungumzo ya nyuklia ni kuwa na ndoto za alinacha na kuongeza kuwa, adui anataka kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isalimu amri, lakini hafahamu kwamba, wananchi wa taifa hili la Kiislamu wamejifunza vyema somo la nguvu, muqawama na ushujaa wa Imam Hussein AS, Imam wa tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

MAUAJI YA KIONGOZI WA KIISLAMU UGANDA YALAANIWA.
Watu mbalimbali waliotoa maoni yao wamelaani vikali kuuliwa kiongozi mwengine wa Kiislamu nchini Uganda.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, wananchi wa rika, dini na madhehebu tofauti nchini Uganda wamelaani vikali kuuliwa kwa kupigwa risasi kifuani, Imam wa Msikiti wa Bilal katika Wilaya ya Mbale, Sheikh Abdul Rashid Wafula (47). Wananchi wa Uganda wameilaumu serikali na hasa jeshi la polisi kwa kushindwa kuwalinda viongozi hao wa Kiislamu na kutosheka tu na kusema watu wasiojulikana ndio waliotenda jinai hiyo. Hata hivyo tayari jeshi la polisi nchini Uganda limetangaza kutiwa mbaroni watu kadhaa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Imam huyo wa Msikiti wa Bilal katika kitongoji cha Kireka, mjini Nakaloke, Wilayani Mbale, alipigwa risasi na watu wasiojulikana Alkhamisi usiku, nje ya nyumba yake. Mwezi Disemba mwaka jana pia, Sheikh Abdul Qadir Sudi Muwaya mkuu wa Taasisi ya Kiislamu ya Ahlul Bait (ABIF) katika Wilaya ya Mayuge nchini Uganda aliuawa kwa kupigwa risasi katika mazingira ya kutatanisha. Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda (UMSC) jana lilitoa taarifa na kulaani vikali mauaji ya Sheikh Wafula likimtaja sheikh huyo kwamba alikuwa hajui kuchoka na alikuwa akiwatumikia Waislamu wa rika na madhehebu yote kwa ikhlasi na kwa njia tofauti. Chanzo cha habari:http://kiswahili.irib.ir/…/48976-mauaji-ya-kiongozi-wa-kiis…