WAITIFAKI WA ISRAEL WAMEITAJA HIZBULLAH KUWA KUNDI LA KIGAIDI.



Kamanda mwandamizi wa kijeshi nchini Iran amesema waitifaki wa utawala haramu wa Israel ndio wallioitaja harakati ya muqawama ya Hizbullah kuwa kundi la kigaidi.
Brigadier Jenerali Yadollah Javani, mshauri wa mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC amesema wale ambao wameibua mgogoro Syria na wanaounga mkono utawala wa Kizyauni wa Israel ndio walioitaja harakati ya mapambano ya Hizbullah kuwa kundi la kigaidi.
Javani amesema hatua ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ya kuituhumu Hezbollah ni hatua ya kujidhuru na ni kosa la kistratijia litakalolipotezea itibari baraza hilo.
Amesisitiza kuwa Hzibullah ni harakati mashuhuri ambayo iliundwa kwa ajili ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel, kulinda ardhi ya Lebanon na kutetea haki za Waislamu.
Kamanda huyo wa kijeshi nchini Iran amesema hatua ya tawala za Kifalme katika Ghuba ya Uajemi kuitaja Hizbullah kuwa kundi la kigaidi ni ishara kuwa nchi hizo za Kiarabu zinafuata nyayo za Wazayuni kwa lengo la kutekeleza matakwa ya Marekani.
Brigadier Jenerali Yadollah Javani amesema Hizbullah ni harakati inayoheshimika katika ulimwengu wa Kiislamu na kwamba ina nafasi ya kipekee miongoni mwa mataifa ya Waislamu na Waarabu.


'INAAIBISHA NCHI ZA KIISLAMU KUWA NA UKURUBA NA UTAWALA WA KIZAYUNI'

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema "inaaibisha" nchi za Kiislamu kuwa na ukuruba na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika mji mkuu wa Indonesia hii leo mwishoni mwa kikao cha dharura cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Dakta Muhammad Javad Zarif amesema: "katika zama ambapo kwa mara ya kwanza utawala wa Kizayuni unashambuliwa vikali katika Ulimwengu wa Magharibi, sambamba na jumuiya zisizo za kiserikali za nchi za Magharibi kuchukua msimamo dhidi ya utawala huo, inaaibisha kwa baadhi ya nchi za Kiislamu kuwa na ukuruba na utawala huo na hivyo kufifisha mashambulio ya Magharibi dhidi ya utawala wa Kizayuni".
Akizungumzia ajenda za kikao cha Jakarta, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "katika kikao hicho, mbali na kuchunguza jinai za utawala wa Kizayuni, tumesisitiza kuwa jinai hizo zinakinzana na sheria za kimataifa; hivyo tumelitaka Baraza la Usalama lichukue hatua kuhusiana na suala hilo."
"Moja ya maudhui kuu iliyotukutanisha pamoja ni suala la uyahudishaji wa mji wa Baitul Muqaddas na vilevile eneo la msikiti wa Al-Aqsa", amesema Zarif.
Mapema alipohutubia kikao cha dharura cha OIC, Zarif alisema Iran inasisitiza kutimiza ahadi zake kuhusiana na Palestina. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifafanua kuwa:"Pamoja na Iran kujua kwamba mashinikizo mbalimbali yaliyoikabili katika miongo ya karibuni yametokana na uungaji mkono wake kwa malengo matukufu ya Palestina lakini itaendelea kutekeleza sera hizo".
Zarif aidha amelikosoa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutotekeleza majukumu yake kulingana na Hati ya umoja huo kwa sababu kadhaa hususan siasa za moja ya nchi wanachama wa kudumu wa baraza hilo na hivyo kuruhusu utawala wa Kizayuni uendelee kutishia amani na usalama wa kimataifa.
Aidha ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kuweka kando tofauti zao na kuchukua hatua za kivitendo ili kukomesha madhihirisho yote ya kukaliwa kwa mabavu Palestina ikiwemo kuzuia hatua haramu za utawala ghasibu wa Israel za kutaka kuubadilisha utambulisho wa mji wa Quds unaoukalia kwa mabavu.
Kikao cha tano cha dharura cha viongozi wa nchi wanachama wa OIC kilichotanguliwa na cha mawaziri wa mambo ya nje hapo jana, kimefanyika leo katika mji mkuu wa Indonesia, Jakarta kikihudhuriwa na viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa nchi 57 wanachama.
Kikao hicho kimeitishwa kutokana na hali ya kutia wasiwasi ya Palestina na mji mtukufu wa Baitul Muqaddas.../ (irib)