'TUNGELISUBIRI WAARABU, LEO ISRAEL INGELIKUWA LEBANON'



Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, lau kama tungelikaa na kusubiri stratijia na mikakati ya Umoja wa Waarabu, basi leo hii Israel ingelikuwa iko nchini Lebanon.
Sayyid Hassan Nasrullah amesema hayo leo katika tamasha la kumuenzi shahid Ali Fayyadh (Alhaj Alaa) na kubainisha kuwa, lau usingelikuwepo muqawama wa Waislamu wa Kishia basi leo hii Lebanon ingelikuwa inatawaliwa na Israel, kungelikuwa na makoloni huko Lebanon na vijana wa Kilebanoni wangelikuwa wamejaa kwenye jela za Wazayuni hivi sasa.
Amesisitiza kuwa, chaguo letu kwa ajili ya kukomboa ardhi yetu lilikuwa ni muqawama na litaendelea kuwa muqawama na lau tungelikaa kimya basi ardhi yote ya Lebanon ingelikuwa sawa na ya mashamba ya Shaba'a yanayoendelea kukaliwa kwa mabavu na Israel.
Amesema, hapa ndipo inapoonekana faida na umuhimu wa uungaji mkono wa Syria na Iran kwa muqawama wa wananchi wa Lebanon.
Sayyid Hassan Nasrullah ameendelea kusema: Wale wanaotutuhumu kuwa muqawama wetu ni wa kimadhehebu, wanapaswa kujiuliza, tulipowaunga mkono Waislamu wa Bosnia, tuliwaunga mkono kwa kuwa ni Mashia? Waislamu wa Bosnia ni Ahlusunna Waljamaa, lakini tuliwaunga mkono.
Vile vile amehoji akisema, tawala za Waarabu zimefanya nini tangu mwaka 1967 hadi leo, je, zimeikomboa Masjidul Aqsa, Kibla cha Kwanza cha Waislamu kutoka katika makucha ya Wazayuni?



'KUITAJA HIZBULLAH KUWA NI KUNDI LA KIGAIDI NI NJAMA YA SAUDIA'
Mkuu wa Kamati ya Intifadha ya Quds nchini Iran amesema kuwa kuiita Hizbullah ya Lebanon kuwa ni kundi la kigaidi ni njama iliyobuniwa na Saudi Arabia na Wazayuni kwa amri ya viongozi wa Israel.
Kamanda Ramadhan Sharif ambaye alikuwa akijibu hatua ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kiarabu wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (PGCC) walioiweka harakati ya Hizbullah kwenye orodha ya magaidi amesema kuwa, hatua hiyo imechukuliwa baada ya safari iliyofanywa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al Jubair huko Tel Aviv na mazungumzo yake na viongozi wa Israel.
Ramadhan Sharif amesema kuwa kuiweka Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi ni kuuvunjia heshima Umma wa Kiislamu na kwamba wale waliotia saini taarifa hiyo ya baraza la PGCC na kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu watatengwa na kuchukiwa na Waislamu.
Mkuu wa Kamati ya Mapambano ya Intifadha ya Quds tukufu huko Palestina amesema Hizbullah ya Lebanon ni mlinzi wa Umma wa Kiislamu na watu wa Lebanon na inaandamwa na wale ambao hadi sasa hawajachukua hatua yoyote ya kuitetea Palestina mbele ya uvamizi wa Israel. Ameongeza kuwa hatua hiyo haitakuwa na taathira yoyote katika azma imara ya Hizbullah na kwamba njama za Marekani, Wazayuni wa Israel na washirika wao zitagonga ukuta.  (irib)