NUSAIBA: "MIMI SI MUISLAMU SHIA, MIMI NI MUISLAMU."

Bintiye Sheikh Zakzaky
Mimi si Muislamu Shia,Mimi ni Muislam.
Bi. Nusaiba Zakzaky bintiye Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky ametoa taarifa akibainisha hali ya Waislamu nchini Nigeria na kusema, serikali ya nchi hiyo inawakandamiza Waislamu wa madhehebu zote.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, katika taarifa iliyosambwaza kupitia tovuti ya 'Islamic Movement of Nigeria', Bi. Nusaiba Zazaki amesema:
"Mimi si Muislamu Shia. Mimi ni Muislamu na wala situmii neno lingine ila Mwislamu. Sisi Waislamu hatupaswi kukubali kutumia majina kama Mwislamu Shia, Mwislamu Sunni, Muislamu Mnigeria, Muislamu Mmarekani, Muislamu wa kisasa, Muislamu mwenye misimamo ya wastani na kadhalika.
Inasikitisha sana kuona namna baadhi ya ndugu zetu wanavyotaja yale yaliyojiri Zaria kuwa ni mauaji ya Mashia kana kwamba hawa watu (serikali na jeshi la Nigeria) wametushambulia kwa sababu tu sisi tunafuata madhehebu ya Shia. Kuna wengine pia wanafuata hayo madhehebu lakini hawashambuliwi. Wakati harakati ya Kiislamu Nigeria ilipoanza, wengi katika harakati hii walikuwa Masuni na serikali iliwashambulia wakati huo kama ambavyo inatushambulia hivi sasa.
Serikali wakati huo pia iliwafunga jela na iliwatazama kama tishio kwa ufisadi na udhalimu ulioko katika utawala. Kwa nini? Kwa sababu tunataka kusitisha udhalimu wa serikali kwa Wanigeria.
Iwapo tutakuwa na msimamo sawa na watu wengi nchini ambao hawasemi chochote kuhusu ufisadi na udhalimu, sote tutakumbwa na matatizo na kisha tutaishi kwa "amani", kama unavyoweza kuishi katika nchi ambayo hauna haki zozozte hata haki za kimsingi za binadamu.
Baba yangu (Sheikh Zakzaky) hakujitambulisha kama kiongozi wa madhehebu maalumu wala hakuitambulisha Harakati ya Kiislamu kama madhehebu. Ajenda kuu ya Harakati ya Kiislamu imekuwa ni kupigania na kutetea uadilifu katika mfumo ambao tunalazimishwa kuishi ndani yake katika nchi hii.
Kila mtu kutoka sehemu yoyote, hata wasio kuwa Waislamu wanakaribishwa kujiunga na mapambano yetu. Kwa vyovyote vile, hata tukiwa tunaegemea au kufuata madhehebu zilizopo, lengo letu kuu ni kutekeleza yale ambayo Mtume Muhammad SAW alitufundisha na kutuletea.
Tunakaribia kuadhimisha 'Wiki ya Umoja', hii ni wiki ambayo Waislamu kutoka matabaka yote hukutana kusherehekea nukta zetu za pamoja kuliko yale yenye kututenganisha. Usiruhusu yaliyojiri yapelekee usahau mafunzo yenye thamani ambayo tumejifunza katika 'Wiki ya Umoja' miaka iliyopita.
Wakati ndugu zangu watatu walipouawa mwaka jana, walikuwa katika maandamano ya kufungamana na Wapalestina, ambao aghalabu wanafuata madhehebu ya Sunni. Kwa hivyo hawakuuawa kwa sababu wanafuata madhehebu ya Shia, bali waliuawa kwa sababu walikuwa wakiwatetea watu waliodhulumiwa. Wakuu wa serikali ya Nigeria walihisi hatari kwa sababu wao wenyewe ni madhalimu.
Hakuna sababu nyingine inayoweza kuhalalisha kuwapiga risasi na kuwaua watu waliokuwa wakiandamana kwa amani na kuwaacha watokwe na damu kwa muda mrefu hadi wafariki dunia.
Mauaji (ya Zaria) si ya Mashia.
Ni mauaji ya wanadamu. Kila mtu duniani anapaswa kukasirishwa na mauaji hayo wakiwemo wasio kuwa Waislamu hasa Wanigeria. Iwapo serikali au wanajeshi waliokula kiapo kulinda usalama wako watatekeleza mauaji dhidi yako kwa sababu ndogo sana kama vile kufunga barabara na kisha kusambaza video ambayo wanasema inahalalisha mauaji ya mamia bali maelfu ya watu, ni nini kingine hawawezi kufanya kukuua. Iwapo hausimami na kuzungumza dhidi ya jinai kama hii, siku moja nawe pia utakumbwa na hali kama hii na wakati huo ni nani atakayekutetea"?
Na. Nusaibah Ibrahim El Zakzaky
Ikumbukwe kuwa, kwa kutoa tuhuma kwamba Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ilikula njama ya kutaka kumuua kamanda wa jeshi na kufunga njia kwa ajili ya shughuli za mijumuiko ya harakati hiyo, tarehe 12 Desemba, jeshi la Nigeria liliishambulia ukumbi wa Kiislamu wa Husainiyyah Baqiyyatullah katika mji wa Zaria kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuuawa Waislamu kadhaa. Siku iliyofuata jeshi hilo lilihujumu nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na kuwaua Waislamu zaidi ya elfu moja.
Sheikh Ibrahim Zakzaky alikamatwa na jeshi la Nigeria akiwa tayari amesapgiwa risasi nne na anatazamiwa kufikishwa mahakamani. Jeshi la Nigeria limechoma miili ya baadhi ya iliyowaua na kuwazika wengine katika makaburi ya umati ili kujaribu kuficha jinai la askari wake. Aidha jeshi hilo limebomoa kikamilifu ukumbi wa Kiislamu wa Husainiyyah Baqiyyatullah na majengo yote ya karibu.
Imearifiwa kuwa Sheikh Zakzaky ana watoto tisa ambapo sita kati yao wa kiume wameuawa shahidi na jeshi la Nigeria. Watatu waliuawa mwaka jana katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na wengine watatu wameuawa shahidi mwezi huu wa Desemba kufuatia mauaji ya umati yaliyotekelezaji na jeshi hilo hilo la Nigeria mjini Zaria.