Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson ameuokosoa Utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi na kueleza kwamba sera hizo za Tel Aviv zinakinzana waziwazi na madai ya kutaka amani yanayotolewa na viongozi wa utawala huo. Akiashiria kutangazwa tarehe 29 Novemba kuwa Siku ya Mshikamano na Wapalestina na haja ya kufanywa jitihada zaidi na Jamii ya Kimataifa kwa ajili ya kutatua kadhia ya Palestina, Eliasson ameongeza kuwa matumaini na hisia ya kuwa na amani waliyonayo wananchi wa Palestina vimefikia kiwango cha chini kabisa. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameashiria kuongezeka ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa Wapalestina na walowezi hao na kueleza kwamba muelekeo huo na sera za aina hiyo zinazotekelezwa na Israel vimezidi kufuta matumaini ya kupatikana suluhu na amani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Aidha amesema japokuwa mnamo tarehe 29 Novemba mwaka uliopita wa 2014 Palestina ilikubaliwa kuwa nchi mtazamaji isiyo mwanachama katika Umoja wa Mataifa, na hadi sasa zaidi ya nchi 130 zimeitambua rasmi nchi ya Palestina huku bendera ya Palestina ikipepea kando ya bendera ya nchi nyengine wanachama wa umoja huo, lakini mafanikio yote hayo pamoja na hatua zilizopigwa kisiasa hazijaweza kuwa na taathira chanya kwa maisha ya watoto wa Kipalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza kutokana Israel kuendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kuendeleza ujenzi wa vitongoji katika ardhi hizo…/
KUMALIZIKA KIKAO CHA TEHRAN CHA NCHI ZINAZOUZA GESI KWA WINGI DUNIANI (GECF)
Kikao cha tatu cha viongozi wa nchi wanachama wa Jukwaa la Nchi Zinazouza Gesi Kwa Wingi Duniani (GECF) kilimalizika jana usiku hapa mjini Tehran kwa kutolewa taarifa maalumu. Kikao hicho cha Gesi cha Tehran kilianza siku ya Jumamosi kwa kuhudhuriwa na mawaziri wa nishati wa nchi 18 wanachama wa asili pamoja na wanachama watazamaji wa nchi zinazosafirisha gesi kwa wingi zaidi duniani. Katika kikao hicho cha mawaziri nchi wanachama zilifikia mwafaka juu ya rasimu ya taarifa ya pamoja ya kikao cha viongozi wakuu wa nchi hizo. Katika kikao cha viongozi kilichofanyika jana chini ya uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Dakta Hassan Rouhani na kuhudhuriwa pia na marais wa Russia, Iraq, Bolivia, Venezuela, Equatorial Guinea, Nigeria, Turkmenistan pamoja na Waziri Mkuu wa Algeria nchi washiriki zilikamilisha mazungumzo yao kwa kutoa taarifa maalumu. Katika taarifa yao hiyo nchi wanachama wa GECF zimesisitiza kuwa zinaunga mkono maslahi ya pamoja ya nchi wanachama kupitia utekelezaji wa sera na mikakati ya pamoja katika ngazi ya kimataifa kwa madhumuni ya kuongeza zaidi kiwango cha maslahi ya kijamii na kiuchumi yanayotokana na vyanzo vya gesi asilia. Kutokana na umuhimu wa kuwepo uratibu wa pamoja na ushirikiano kati ya nchi wauzaji na wanunuzi wa gesi, nchi wanchama wa Jukwaa la Nchi Zinazouza Gesi Kwa Wingi Duniani (GECF) zimetaka yafanyike mazungumzo ya maana zaidi na nchi wanunuzi wa gesi asilia kupitia taasisi na jumuiya za kieneo na kimataifa za nishati. Miongoni mwa masuala yaliyozingatiwa ni pamoja na mahitaji ya gesi asilia pamoja na kustawisha miundombinu kupitia utekelezaji wa sera zisizo za ubaguzi na upendeleo. Taarifa ya kikao cha Tehran imesisitiza pia juu ya umuhimu wa upangaji bei ya gesi asilia na vilevile kudhaminiwa usalama wa uwekezaji katika sekta ya gesi. Viongozi wa nchi wanachama wa GECF aidha wametaka kuimarishwa zaidi nafasi ya nchi hizo katika uga wa kimataifa wa nishati na kukubaliana juu ya kuanzisha taasisi ya utafiti wa gesi nchini Algeria. Kutokana na umuhimu wa kuzingatia utunzaji wa mazingira na umuhimu wa kutumia gesi asilia kama fueli safi kwa ajili ya hifadhi ya mazingira, kikao cha Tehran kimetoa ujumbe maalumu kwa kikao cha kimataifa cha mabadiliko ya tabianchi kinachojulikana kama COP 21 kilichopangwa kufanyika mjini Paris, Ufaransa. Katika ujumbe wao huo, nchi wanachama wa Jukwaa la Nchi Zinazouza Gesi Kwa Wingi Duniani zimetangaza kuwa ziko tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya COP 21. Udharura wa kuwepo ushirikiano huo kutokana na faida za gesi asilia umekipa umuhimu zaidi kimataifa kikao cha Tehran cha nchi wanachama wa GECF. Ni kwa sababu hiyo ndipo Rais Hassan Rouhani akakitaja kikao hicho kuwa ni tukio muhimu katika uga wa nishati. Akiwa mwenyekiti mpya wa mzunguko wa GECF, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya udharura wa kuandaliwa ramani ya njia kwa lengo la kulipatia nafasi zaidi jukwaa hilo katika kudhamini uhakika wa upatikanaji wa nishati duniani. Amesema miongoni mwa malengo ya kikao cha Tehran ni pamoja na kuwepo ushirikiano wa kubuni njia za kudhamini maslahi ya pamoja ya nchi wanachama zinazouza gesi kwa wingi zaidi duniani, kustawishwa ushirikiano katika nyanja mbalimbali zikiwemo za ugunduzi, uzalishaji na uuzaji wa gesi asilia, kuratibu sera zitakazowezesha kuongezwa mgao wa gesi asilia katika matumizi ya nishati duniani pamoja na kustawisha nafasi ya GECF katika uga wa kimataifa wa nishati…/
ZARIF: MAGAIDI WANALENGA KULICHAFUA JINA LA UISLAMU.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema magaidi na watu wenye misimamo mikali na ambao wanafanya maovu makubwa kwa jina la Uislamu wanalenga kuiharibia jina dini hiyo tukufu ya Mwenyezi Mungu. Waziri Zarif amesema hayo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Geoffrey Onyeama, hapa mjini Tehran. Waziri Onyeama ameandamana na ujumbe wa Rais Muhammadu Buhari ambaye amefika nchini kuhudhria mkutano wa kimataifa wa gesi uliowaleta pamoja marais na mawaziri wakuu kutoka nchi mbalimbali zinazounda Jukwaa la Nchi Zinazouza Gesi Kwa Wingi Duniani (GECF). Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Makundi ya kigaidi na kitakfiri kama vile Daesh na Boko Haram yanaendesha propaganda dhidi ya Uislamu kwa uungaji mkono wa Madola ya Magharibi. Waziri Zarif amesema kwa masikitiko makubwa pia baadhi ya nchi za Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati zinayaunga mkono makundi kama hayo ambayo yameleta fitina na mfarakano mkubwa miongoni mwa Waislamu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria kwa upande wake amesema nchi yake itashirikiana kwa karibu na Iran katika vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali. http://kiswahili.irib.ir/…/53156-zarif-magaidi-wanalenga-ku…