IDUL FITR KUADHIMISHWA JUMAMOSI NCHINI IRAN.

Kamati ya kuutafuta mwezi mwandamo katika Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imetangaza kuwa, Siku kuu ya Idul Fitr itaadhimishwa kesho nchini Iran na kwa msingi huo Ijumaa ya leo ni siku ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani nchini.
Ofisi hiyo imetoa taarifa na kusema kuwa, Alhamisi jioni mwezi mwandamo haukuonekana na kwa msingi huo Ijumaa hii ni siku ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kesho, ni Idul Fitr, Inshaallah.
Serikali ya Oman pia imetangaza kuwa mwezi haukuandama jana Alkhamisi na kwa hivyo Idul Fitr itaadhimishwa kesho nchini humo. Afghanistan na Morocco pia ni kati ya nchi ambazo Idul Fitr itaadhimishwa kesho. Pamoja na hayo baadhi ya nchi kama vile Syria, Saudi Arabia, Misri, Qatar na Indonesia zimetangaza Ijumaa ya leo kuwa ni Idul Fitr.
Nchini Kenya Kadhi Mkuu Sheikh Ahmed Muhdhar jana Alkhamisi pia alitangaza kuwa Waislamu nchini wataadhimisha Idul Fitr Siku ya Jumamosi. Akizungumza mjini Mombasa, amesema mwezi haukuandama eneo la pwani kama ambavyo pia haujaandama maeneo mengine ya Afrika Mashariki hasa Tanzania na Zanzibar.