Sera za mabavu na ukandamizaji za
watawala wa Yemen katika kukabiliana na malalamiko ya wananchi
yanayodhihirishwa kwa njia za amani zimekabiliwa na radiamali za
upinzani za harakati, vyama na shakhsia mbalimbali wa nchi hiyo. Msemaji
wa harakati ya Ansarullah ametangaza kuwa Mahauthi hawatoruhusu
serikali ya Yemen imwage tena damu za wapinzani wanaoandamana kwa amani.
Kufuatia mashambulio ya kinyama yaliyofanywa na vikosi vya usalama vya
Yemen dhidi ya wapinzani karibu na jengo la ofisi ya Waziri Mkuu,
msemaji wa Ansarullah Muhammad Abdussalam, amesema serikali ya Yemen
ndio msababishaji mkuu wa maafa hayo na kubainisha kuwa serikali hiyo
haitaki kusikiliza sauti ya malalamiko yanayotolewa kwa njia za amani
kwa sababu imeamua kusikiliza na kufuata amri kutoka nje ya nchi.
Msemaji wa Ansarullah amesisitiza kwa mara nyengine juu ya ulazima wa
kuendelezwa harakati ya malalamiko ya wananchi hadi kuhakikisha matakwa
ya wananchi hao yanatekelezwa. Inafaa kuashiria hapa kuwa juzi Jumanne
vikosi vya usalama na jeshi vikiandamana na watu waliobeba silaha
walioziba nyuso zao waliyashambulia maandamano ya amani ya wananchi
katika mji mkuu wa Yemen, Sana’a, wakawafyatulia risasi wananchi hao
ambao hawakuwa na lengo jengine ghairi ya kufunga mahema yao mbele ya
jengo la ofisi ya Waziri Mkuu na kukusanyika hapo hadi matakwa yao
yatakapotekelezwa. Matokeo ya mashambulio hayo ya vikosi vya serikali
yalikuwa ni kuuawa raia kumi na kujeruhiwa makumi ya wengine. Takwa kuu
la wananchi wanamapinduzi wa Yemen ni kuondolewa serikali mbovu iliyopo
na kuundwa serikali mpya yenye uwezo wa kuihudumia nchi kulingana na
misingi ya makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya kitaifa na
kuutatua mgogoro na hali mbaya ya kiuchumi inayotawala nchini humo.
Kwa mujibu wa Hassan As Sa’adi, mjumbe
wa baraza la kisiasa la harakati ya Ansarullah ya Yemen, baadhi ya
madola ya kigeni ambayo yana hofu ya kuwepo demokrasia nchini Yemen
yanaishinikiza serikali ya Sana’a iwakandamize vikali wapinzani ili
serikali hiyo isiweze kulegeza kamba katika msimamo wake. As Sa’adi
mbali na kusisitiza kwamba matokeo mabaya yanawangojea watawala wa Yemen
amefichua pia kuwa watu wa karibu na makundi ya kitakfiri na al Qaeda
wamekuwa wakihudumu kwenye vikosi vya usalama vya nchi hiyo. Ali Al
Bukhaiti, mjumbe mwengine wa baraza la kisiasa la harakati ya
Ansarullah, naye pia amesisitiza kwamba harakati ya Mahuthi itaendelea
kufanya mikusanyiko zaidi ya upinzani katika mji mkuu na kandoni mwa
majengo ya wizara hadi kuhakikisha serikali inang’atuka madarakani.
Jumuiya ya Maulamaa wa Yemen nayo pia imetoa taarifa ya kulaani
mashambulio ya siku ya Jumanne dhidi ya wafuasi wa harakati ya
Ansarullah waliokuwa wamekusanyika kwa amani katika barabara ya al Matar
na kueleza kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ndiyo inayobeba dhima ya
damu iliyomwagwa ya raia wasio na hatia. Muhammad al Maqalih, mjumbe wa
kamati kuu ya chama cha Kisoshalisti cha Yemen yeye amesema kuhusiana na
matukio yaliyojiri mjini Sana’a na mashambulio ya vikosi vya usalama
dhidi ya raia, kwamba kilichotokea katika mji mkuu huo wa nchi hiyo ni
mauaji ya halaiki kwa maana yake halisi na kwamba rais ndiye anayebeba
dhima hiyo. Hayo yanajiri katika hali ambayo vitendo vya mabavu vya
serikali ya Yemen dhidi ya harakati za amani za wapinzani vimelalamikiwa
na duru za kidiplomasia pia ambapo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza wasiwasi alionao kutokana na
utumiaji nguvu na mabavu wa vikosi vya usalama vya Yemen dhidi ya
malalamiko ya wananchi. Bi Marzie Afkham aliyasema hayo jana na kuitaka
serikali, vyama vya siasa na makundi mbalimbali ya Yemen wajidhibiti
katika uchukuaji hatua; na akaongeza kwa kusema utatuzi wa masuala
yaliyopo utapatikana kwa njia ya mazungumzo tu; na kwa kupitia mchakato
wa kisiasa na wa njia za amani utakaoshirikisha vyama, makundi na
harakati zote za kisiasa na kijamii za Yemen ndipo itawezekana kurejesha
uthabiti, amani na utulivu nchini humo…/