SAUDIA YAAHIRISHA HUKUMU DHIDI YA SHEIKH NIMR



Mahakama maalumu mjini Riyadh, Saudi Arabia, leo imeahirisha hukumu dhidi ya Sheikh Nimr Baqir an Nimr ambaye anaendelea kushikiliwa katika korokoro za utawala wa Aal Saud kwa miaka miwili sasa. Habari zinasema kuwa, mahakama hiyo imeahirisha hukumu ya Sheikh Nimr Baqir an Nimr hadi mwishoni mwa mwezi huu baada ya kufanya kikao na kujadili tuhuma zinazomkabili Sheikh Nimr. Hii ni baada ya kutolewa onyo kutoka kwa viongozi wa kidini wakiwemo maraajii wa Kiislamu katika nchi tofauti wakiuonya utawala wa nchi hiyo ya kifalme kuhusu uwezekano wa kumuhukumu adhabu ya kifo mwanachuoni huyo. Mbali na maulamaa wa Kiislamu, nchi kadhaa za Kiarabu na asasi za kutetea haki za binaadamu nazo zilikuwa zimeonya kuwa huku kama hiyo itazusha hasira ndani ya nchi hiyo. Duru za habari nchini Iraq zimetangaza kuwa Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Sistani amemtaka rais wa nchi hiyo Fuad Masum, kuchukua hatua za haraka za kuzuia hukumu ya adhabu ya kifo inayoweza kutolewa na mahakama ya Saudia dhidi ya shakhsia huyo wa kidini. Hii ni katika hali ambayo Ayatullah Naser Makarim Shirazi, mmoja wa wanavyuoni wakubwa wa Kiislamu na marjaa wa kidini wa mjini Qum hapa Iran alikuwa ametangaza kuwa, kutolewa adhabu ya kifo dhidi ya Sheikh Nimr Baqir an Nimr, kutajeruhi nyoyo za Waislamu wa Kishia kote ulimwenguni na kutakuwa na matokeo mabaya sana. Marjaa huyo ameuusia utawala wa Aal Saud kusikiliza matakwa ya wananchi wa nchi hiyo badala ya kutumia mabavu katika kuzima madai yao.