"NJAMA ZA MAREKANI, ISRAEL NA DAESH ZIMESHINDWA"



Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa, Marekani kwa kushirikiana na nchi nyingine za eneo la Mashariki ya Kati ndizo zilizounda kundi la kigaidi la Daesh na kulipeleka nchini Syria. Sheikh Naeem Qassim amesema kuwa, njama za Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na kundi la kigaidi la Daesh za kutaka kuiangusha serikali ya Rais Bashar Assad wa Syria zimegonga mwamba. Ameongeza kuwa, uhusiano wa Hizbullah na  Hamas bado ni imara na kusisitiza kwamba harakati hizo mbili daima zimekuwa zikielekeza nguvu zao dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amepuuza matamshi yanayotolewa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu kwamba, mapambano ya Wapalestina dhidi ya Wazayuni yamesambaratika. Sheikh Naeem Qassim amesema kuwa, vita vya Ghaza vimetoa funzo na somo zuri kwa  adui Mzayuni na kusisitiza kwamba kwa mara ya kwanza kabisa Netanyahu amekiri wazi juu ya kuwepo utulivu mkabala wa utulivu na usitishaji vita mkabala wa usitishaji vita. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwa, Netanyahu ameonyesha wazi kushindwa kwenye vita vya Ghaza, pale alipotoa madai kwamba Iran inashiriki kwenye vita hivyo.