Jinai za muda mrefu za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza zinaendelea kuwaunganisha wapenda haki kote duniani na kwa sasa kunashuhudiwa wimbi jipya la muamko wa walimwengu wanaosisitiza kususiwa bidhaa za makampuni ya kizayuni kama njia moja ya kuutia adabu utawala huo bandia. Wananchi katika mji wa Belfast, Ireland ya Kaskazini, huku wakipiga nara za kulaani utawala wa Kizayuni wa Israel na kutetea uhuru wa Wapalestina, wamekusanya bidhaa zinazotengenezwa na mashirika ya Israel kutoka kwenye maduka makubwa ya mjini hapo na kisha kuyateketeza moto. Gazeti moja la Kizayuni limeandika kwenye toleo lake la Jumatatu iliyopita kwamba, mashirika kadhaa ya Ulaya ambayo yamekuwa yakinunua bidhaa zinazozalishwa na Wazayuni kwa sasa hayanunui tena bidhaa hizo kutokana na wananchi wengi kuzisusia. Wafanyabiashara wengi wa Kizayuni wanaosafirisha bidhaa zao nchini Uingereza wanasema wateja wao huko London wameanza kukataa bidhaa zao zinazozalishwa kwenye vitongoji vya Walowezi wa Kizayuni wakisema kwa sasa wanunuzi wanakataa kununua bidhaa hizo. Suala hili linadhihirisha jinsi Wazayuni wanavyoendelea kutengwa kiuchumi na hata kisiasa na nchi mbalimbali duniani. Na si hayo tu bali pia huko nchini Uhispania, vyama mbalimbali vya siasa, mashirika ya kijamii na miungano ya vyama vya wanabiashara kwa pamoja vinaishinikiza serikali kusimamisha biashara zinazodhamini maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Tayari chama kimoja cha upinzani katika bunge la Uhispania kimewasilisha hoja ya kutaka biashara za Israel zisimamishwe nchini humo.
Nchini Ufaransa nako, gazeti la kila siku la LE MONDE limeandika kuwa, katika maandamano ya hivi karibuni ya kuwaunga mkono wananchi wa eneo la Gaza, waandamanaji walikuwa na orodha ya bidhaa zinazozalishwa na mashirika ya Wazayuni ambapo walisisitiza kugomewa bidhaa hizo. Maandamano kama hayo pia yamekuwa yakishuhudiwa huko Kuala Lumpur, Malaysia ambapo maelfu ya watu wamekuwa wakiandamana tangu yalipoanza mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza. Wananchi wa Malaysia wanaitaka nchi yao kukata uhusiano wowote ule na utawala wa Kizayuni sambamba na kupiga marufuku bidhaa za mashirika ya utawala huo au hata yale ya Malaysia yenye mfungamano na Israel.
Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanaamini kwamba, wimbi jipya la uungaji mkono wa walimwengu kwa Wapalestina na takwa la wapenda haki duniani la kususiwa bidhaa za Israel ni tishio kubwa kwa mustakabali wa utawala huo ghasibu na mabwana zake wa Ulaya na Marekani. Wajuzi wa mambo wanasema Israel inakabiliwa na uwezekano mkubwa wa kusambaratika kabisa kiuchumi na hata kisiasa kutokana na kuongezeka sauti za walio wengi wanaopinga jinai zake dhidi ya Wapalestina hususan katika Ukanda wa Gaza.