LARIJANI: MUQAWAMA, NGUVU PEKEE DHIDI YA ISRAEL

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu amesema kuwa, ushindi wa Hizbullah katika vita vya siku 33 dhidi ya utawala wa Kizyauni ni ushindi mkubwa ndani ya Lebanon na katika eneo zima la Mashariki ya Kati. Ali Larijani amesema hayo kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 8 wa ushindi wa mapambano katika vita vya msimu wa joto mwaka 2006 vinavyojulikana kama vita vya siku 33.
Spika wa Bunge la Iran ameeleza kuwa mashambulizi ya adui mzayuni mwaka 2006 dhidi ya Lebanon, yamekuwa na mafanikio muhimu katika eneo na kwamba mbinu za ulinzi na kijeshi za Hizbullah dhidi ya uvamizi wa Israel zimeleta mabadiliko ya kipekee yaliyobadilisha uwiano katika Mashariki ya Kati.
Larijani aidha amesema, jitihada zote zilizofanywa na Israel ili utawala huo uweze kuwa nguvu kubwa zaidi katika eneo zimegonga ukuta na kwamba uwiano wa nguvu umekuwa kwa madhara yake.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, Julai mwaka 2006 jeshi la Israel lilianza mashambulizi makubwa ya pande zote dhidi ya Lebanon kwa kisingizio cha kuwakomboa askari wake wawili lakini vita hivyo vilimalizika kwa ushindi wa Hizbullah na wananchi wa Lebanon.