MGOGORO WA GHAZA NI KADHIA NYETI ZAIDI KATIKA ULIMWENGU WA KIISLAMU.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa mjini Tehran Hujjatul Islam Kadhim Siddiqi amesema kuwa, mgogoro wa Ghaza ni kadhia nyeti zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa. Aidha amelaani vikali jinai za kinyama za utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina wasio na ulinzi wa eneo hilo na kusisitiza kuwa, jinai za siku 30 sasa dhidi ya ukanda huo ambazo ni jinai zisizo na kifani, zimeudhihirishia ulimwengu kwamba utawala wa Kizayuni, hauheshimu hata kidogo sheria za kimataifa. Vile vile khatibu wa sala ya Ijumaa ya mjini ya Tehran amebainisha kwamba, Israel haisiti hata chembe kufanya jinai na kwamba mauaji ya hivi sasa ya watu 2,000 na kuwafanya makumi ya maelfu ya wengine kuwa wakimbizi, ni jinai ambazo hazina mfano wake katika historia ya utawala huo. Hujjatul Islam Kadhim Siddiqi ameonyesha kusikitishwa kwake na kimya cha taasisi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa kutokana na jinai za Israel huko Ghaza kwa kusema kuwa, taasisi hizo kubwa duniani zilionekana kwamba ziliasisiwa kwa lengo la kuzitetea nchi zinazodhulumiwa, hata hivyo kwa bahati mbaya kabisa, tunaziona taasisi hizo hizo zikifumbia macho jinai za utawala katili wa Kizayuni dhidi ya raia wa Ghaza bali hata zinaunga mkono unyama huo. Aidha ameupongeza muqawama wa watu wa ukanda wa Ghaza mbele ya mashambulizi ya kikatili ya Israel na kuongeza kuwa, muqawama huo ni wa kuigwa. Amekosoa pia mataimshi ya hivi karibuni ya Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyetaka kuachiliwa huru askari mmoja wa Kizayuni aliyetekwa nyara na wanamapambano wa Kipalestina wakati wa vita hivyo na kusema kuwa, matamshi hayo yanatia huzuni sana. Amehoji kwamba, inakuwaje mamia ya watoto wadogo wasio na hatia wanauliwa kinyama na askari hao wa Israel, lakini katibu huyo hasemi chochote bali anathubutu kutoa kauli ya kulaani kutekwa nyara askari mmoja tu wa utawala huo?