HISTORIA YA MWANAHARAKATI MKONGWE SHEIKH WAZIRI NYELLOW.

Mwaka 1994 mimi niliamua kuwa Shia Ithna Asharriyah na wenyeji wangu walionipokea ni Bilal Muslim Mission of Tanzania chini ya uongozi wa Maulana Akhtar Rizivi na utendaji wa Mzee Fidah Husain Hameer. Ombi langu la kwanza kwao ili niwe Mwanaharakati mzuri wa Madhehebu ya Ahlul Bayt (a.s) nijengewe Msikiti mjini Lushoto ambapo ndipo mimi kwa miaka karibu 15 nilifanikiwa kueneza Uwahhabi(Answaru Sunna) Wilaya yote ya Lushoto. Na nilifanikiwa kujenga misikiti isiopungua 10 chini ya African Muslim Agency. Mimi nilikuwa msitari wa mbele katika mapambano na madhehebu ya Sunni (Madhehebu ya Shafii) ambayo ndio yaliyokuwa Wilaya ya Lushoto na Tanga yote kwa jumla. Katika Tanzania yote kwa ujumla chini ya vijana wa Warsha ya Waandishi wa Kiislamu tulifanikisha kuanzisha Seminari za Kiislamu, nikiwa Kiongozi wa Idara ya D’awa, nilisimama mahakamani mwaka mzima kwa niaba ya Warsha ya Waandishi wa Kiislamu kuishitaki Wizara ya Elimu na BAKWATA kwa kuwanyima Waislamu wasiwe na Seminari zao wakati Wakristo wanazo. Kesi hiyo tulishinda na Masjid Qubah ikiwa Seminari ya kwanza Tanzania bila kuwa chini ya BAKWATA. Ushindi wa kesi hiyo ukafungua milango kwa Waislamu wakawa na Seminari zao. Almuntaziri ikiwa moja wapo. Kwa msingi huo tulikubaliana tujenge msikiti Lushoto mjini lakini kiwanja kiwe kwa jina la Rejesterd Trustees of Bilal Muslim Mission of Tanzania. Mimi nilitafuta kiwanja baada ya kukosa nilikubali kutoa kiwanja changu kilichoko mjini Lushoto (Wakfu) kwa Bilal Muslim Mission of Tanzania ili mradi tuwe na msikiti mjini. Insha’allah tutaendelea kuwapatia historia ya Mwanaharakati huyu mkongwe