Katika hali ambayo fikra za walio wengi duniani katika wiki
za hivi karibuni zimekuwa zikijielekeza zaidi kwa harakati za magaidi wa
kitakfiri huko Iraq na Syria, utawala wa Kizayuni ambao ulikuwa ukisubiri
kupata fursa ya kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi wala
hatia, hivi sasa umeziweka katika ajenda yake kuu chokochoko zake mpya huko
Palestina. Masuala hayo yanadhihirisha wazi kwamba eneo la Mashariki ya Kati
lingali linakabiliwa na hatari kubwa kutoka kwa Wazayuni na matakfiri. Vyombo
vya habari vimeripoti kuwa, jeshi la utawala wa Kizayuni limeanzisha
mashambulio makubwa ya anga katika eneo la Ukanda wa Ghaza. Baada ya Baraza la
Mawaziri la utawala wa Kizayuni kuidhinisha kushadidishwa mashambulizi huko
Ghaza, ndege za kivita za utawala huo juzi usiku ziliyashambulia karibu maeneo
yote ya Ukanda wa Ghaza. Usiku wa kuamkia leo Jumatano pia, utawala katili wa
Kizayuni umefanya mashambulizi ya kinyma huko Ghaza na kuwaua shahidi
Wapalestina kadhaa. Baadhi ya vyombo vya habari vya Kiarabu vimeripoti kuwa,
operesheni ya nchi kavu ya jeshi la utawala wa Kizayuni huko Ghaza ambayo
imepewa jina la "mwamba mgumu" imeanza sambamba na mashambulizi ya
anga ya jeshi la utawala huo. Baraza la Mawaziri la Israel lilitangaza katika
kikao chake cha dharura kuwa, jeshi la utawala huo litazidisha mashambulizi
dhidi ya raia wa Palestina. Hii ni katika hali ambayo utawala wa Kizayuni
katika siku za hivi karibuni pia umezidisha vitisho vyake kwa raia wa Palestina
na kuzusha tuhuma mbalimbali dhidi ya Wapalestina ili kuhalalisha hatua yake ya
kushadidisha mashambulizi dhidi ya wananchi wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza.
Kivyovyote vile, jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni kupitia mashambulizi
ya pande zote huko Ghaza ni ukumbusho wa mashambulizi ya huko nyuma ya utawala
huo dhidi ya Ghaza, mashambulizi yaliyopelekea utawala huo utende jinai za
kutisha dhidi ya Wapalestina. Kuendelea uchokozi huo wa utawala wa Kizayuni
huko Ghaza ni sawa kabisa na kukiuka makubaliano ya usitishaji vita
yaliyofikiwa kati ya utawala wa Kizayuni na Wapalestina baada ya kushindwa
utawala huo katika vita vya siku 8 ulivyovianzisha dhidi ya Ghaza mwishoni mwa
mwezi Novemba mwaka 2012. Utawala wa Kizayuni unaendeleza mashambulizi yake
dhidi ya Wapalestina katika hali ambayo kwa mujibu wa makubaliano ya huko
nyuma, Israel inapaswa kujiepusha na uchokozi wa aina yoyote ile au kutoa
vitisho vyovyote dhidi ya raia wa Palestina. Hii ni katika hali ambayo, kabla
ya kufikiwa usitishaji vita wowote au makubaliano ya amani kati ya Wapalestina
na utawala wa Kizayuni, walimwengu wanashuhudia kushtadi jinai za utawala huo
ghasibu na suala hilo linadhihirisha wazi namna Israel isivyoheshimu masuala
kama amani wala usitishaji mapigano. Upuuzaji na kimya cha jamii ya kimataifa
kwa ombi la Wapalestina ambao daima mwamekuwa akitaka kudhaminiwa usalama wao
kwa kufikiwa usitishaji vita wa kudumu na kuulazimisha utawala wa Kizayuni
uheshimu makubaliano hayo, yote hayo yameitia kiburi Israel cha kuendeleza
mshambulizi yake ya kikatili dhidi ya Wapalestina. Utawala wa Kizayuni
unaendeleza jinai na mashambulizi yake katika Ukanda wa Ghaza kwa malengo
maalumu moja likiwa ni kufelisha mchakato wa umoja wa kitaifa kati ya
Wapalestina. Hata hivyo uzoefu wa vita vya huko nyuma vilivyoanzishwa na
utawala wa Kizayuni katika eneo hili vikiwemo vita vya siku 22 vilivyoanzishwa
na Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Ghaza vya mwaka 2009 na vile vya siku Nane
dhidi ya eneo hilo mwaka 2012 unaonyesha kuwa, mashambulizi mapya ya hivi sasa
ya utawala wa Kizayuni hayatakuwa na lolote ghairi ya kugonga mwamba tu
kutokana na kushindwa mara kadhaa Israel mbele ya muqawama wa wananchi wa
Palestina. Kuendelea jinai hizo na vitendo vya kujitanua vya utawala wa
Kizayuni katika mwaka huu pia kunabainisha wazi kuwa, Wapalestina na hasa
wakazi wa Ukanda wa Ghaza wangali wanakabiliwa na chokochoko na jinai za
Israel. Mazingira kama hayo yanatoa udharura kwa jamii ya kimataifa kuchukua
hatua kali na za haraka ili kuushinikiza utawala wa Kizayuni usitishe jinai
zake hizo dhidi ya wananchi wa Palestina wasio na ulinzi wala hatia wa Ukanda
wa Ghaza.