HISTORIA FUPI YA MSIKITI WA NYASSA (W) LUSHOTO MASJID IMAM ALI (A.S).



“Bismihi Ta’ala”

Mwenyezi Mungu anasema: " Zindukeni! Hakika wao ndio waharibifu lakini hawatambui" (Qur'an: 2:12)

Msikiti huu chimbuko lake au asili yake ni jitihada za busara ya chini kwa chini za ndugu yetu marehemu Shabiri Kaku. Shabiri Kaku alimuendea ndugu yetu Mzee Abbas Muhammad Husain (Benson) wa Arusha, akamwambia Lushoto tunae mtu anayeitwa Sheikh Waziri Omari Nyello pamoja na mwenzake anayeitwa Hibib Sheketo wote ni Mawahibi wenye jitihada kubwa za kueneza Uwahabi Wilaya ya Lushoto. Ninakuomba uwapelekee vitabu ili wasome huenda wakabadilika. Hasa Bwana Waziri Omari Nyello yeye ni mtu wa dini kweli kweli hana jambo la hovyo hata moja tangu ni mfahamu, ana bidii sana katika mambio ya dini. Hivyo naamini ukiwapelekea watu hawa vitabu mmoja wapo anaweza kubadilika. Hivyo mwaka 1992 Milladia nilitumiwa mzigo wa vitabu na Mzee Abbas Muhammad Husain kutoka Arusha. Katika jumla ya vitabu alivyonitumia ni kitabu cha Dr. Tijani kinachoitwa “Hatimae nimeongoka.” Kitabu hicho wakati huo kilikuwa cha Kiingereza kwa jina la “THEN I WAS GUIDED” kitabu hiki na vinginevyo kilinifanya nibadilike kutoka Uwahabi na kuwa SHIA ITHNA’ASHARIAH. Maneno haya ya mbinu ya marehemu Shabiri Kaku aliniambia nilipokwenda Arusha kumpongeza Mzee Muhammad Husain kwa kuninusuru na kuniwezesha kuyajua Madhehebu ya Ahlul Bayt (S.A). Aliniambia Mzee Abbas mwenyewe.
Baada ya kujitangaza rasmi mwaka 1994 kwa wenzangu wote wa Madhehebu ya Suni pamoja na Mawahabi kama wanavyoitwa jina hilo na Mashia Ithna’ashariah. Viongozi wa Bilal Mission of Tanzania chini ya Raisi wao Marehemu Maulana Sayyid Akhtar Rizvi waliniahidi kunisaidia kwa kila hali. Ombi langu kwao ili niweze kuyapa nguvu Madhehebu haya ya Ahlul Bayt (A.S) katika Wilaya ya Lushoto wanisaidie kwa kunijengea Msikiti. Katika Madrasa zangu mbili ambazo nilikuwa ninazisimamia moja ikiwa Lushoto mjini na nyingine Nyassa kijijini kwangu nilipozaliwa, niliwaondoa walimu wa Kiwahabi ambao nilikuwa nawalipa mimi Mwenyewe kwa pesa zangu zinazotokana na biashara zangu baada yake Bilal Muslim Mission of Tanzania walinipa walimu wa wili wa Madhehebu ya Shia Ithna’ashariah wakawa wanawalipa wao mshahara wa kila mwezi tangu mwaka 1995. Maana nilipokuwa kwenye Madhehebu ya Kiwahabi niliweza kujenga msikiti wa Kiwahabi Kizara ambapo ni karibu na Nyassa na tukaufanya ndio msikiti wetu wa Ijumaa badala ya msikiti wa zamani uliokuwa Ngaloi tuliokuwa tunaswalia Ijumaa kabla ya huu mpya. Msikiti huu wa Kizara niliujenga chini ya African Muslim Agency ambao nilikuwa karibu sana nao na tulisaidiana nao sana mpaka sasa hivi Wilaya ya Lushoto inayo misikiti karibu mitano iliyojengwa na African Muslim Agency. Pia mimi katika jitihada hizo nilifanikisha kuwapatia Waislamu wa Lushoto kiwanja kikubwa tu karibu Ekari 2 pale Lushoto mjini chini ya BAKWATA. Kiwanja hicho kinatazamana na ofisi za CCM (w). Hivyo niliwaambia viongozi wa Bilal walimu tu hawatoshi mpaka tuwe na msikiti ndipo Madhehebu ya Ahlul Bayt (A.S) yapate nguvu. Tulikubaliana nitafute kiwanja hapa mjini Lushoto na wao watatujengea Msikiti kwa vile mazingira yalivyo Lushoto mjini si rahisi kupata kiwanja nilitoa kiwanja changu mwenyewe kilichoko njini ili tuweze kupata msikiti hapa mjini Lushoto. Wao Bilal Muslim Mission of Tanzania walinipa sharti kwamba lazima nikibadili kiwe kwa jina Rejestered Trustees of Bilal Muslim of Tanzania kwa nia nzuri kabisa nilikibadili kiwanja changu hicho kuwa kwa jina la Regestered Trustees of Bilal Muslim Mission of Tanzania. Sio hivyo tu’ michoro yote ya majengo niligharimia mwenyewe na mpaka kupata kibali cha Halmamshauri ya mji wa Lushoto kujenga msikiti huo ambao tuliuita jina la Masjid Imamu Ali (A.S).
Mwaka 1996 kila kitu kikawa kimemalizika. Lakini viongozi wa Bilal wakawa wananizungusha tu hakuna kinachofanyika. Mwaka 1998 Baba yangu mzazi Mzee Omari Nyello alifariki hivyo familia yetu tuliamua kujenga msikiti hapa kijijini kwetu tena barabara kuu ya kwenda Lushoto, ni Kilomita 10 kwenda Lushoto na Kilomita tano kwenda Soni. Baada ya makubaliano haya Kifamilia tulikubaliana tutumie ramani zile zile za msikiti wa Lushoto uliotaka kujengwa na Bilal. Kazi ilianza kidogo kidogo mara moja mwaka huo huo. Mwaka 2002 mama yangu mzazi alifariki pia. Kwenye 40 yake niliamua kufanya kampeni kuweka jiwe la msingi kwa kushirikiana ndugu yangu Shabiri Kaku aliwaleta viongozi wote wa Khoja Shia Ithna’ashariah mpaka Imamu wa Msikiti wetu wa Tanga, na mimi kutoka Dar es Salaam niliwaleta baadhi ya viongozi wa Bilal na WIPHAS pamoja na kiongozi wa kitengo cha Iran kilichoko chini ya Bilal Sayyid Muhammad Taqqi Tabatabai pamoja na Maalimu Issa Mdhamini na Mwenyekiti wa Bodi ya WIPHAS. Waliweka jiwe la msingi tarehe 8 Rajab 1423 sawa na tarehe 15 Septemba 2002. Pia mchango wa Shs 3,000,000/= pesa taslimu pamoja na Ahadi. Pia wageni hao tuliwaonyesha viwanja viwili vya Bilal Muslim Missio of Tanzania kile nilichotoa wakfu na kingine nilikipata baadae, kiwanja hiki cha pili kinapakana na msikiti wa Masuni ulioko Chakichaki hapa Lushoto. Kumbe kitendo cha kujenga msikiti huu wa Mashia ambo sikuuhusisha na Bilal Muslim Mission of Tanzania wala WIPHAS kiliwaudhi sana viongozi wa Bilal na WIPHAS.
Kilichofuatia ni fitna zilizofanywa na viongozi wa jumuia hizo 2 wasisaidie kwa madai kwamba haifai kusaidia maana Sheikh Waziri anajenga msikiti wa baba yake. Fitna nyingine walioeneza ni kwamba hakuna faida ya kujenga Sikiti lote hili kubwa ambalo wanaweza kuswali watu zaidi ya 500 kijijini. Mwaka 2004 nilifiwa na mdogo wangu kwenye arobaini (40) yake pia nilifanya kampeni nyingine tuliwaaalika Mashia walioko Tanga na Dar es Salaam pamoja na Mkurugenzi wa kitengo cha utamaduni cha Iran. Safari hii nsikiti ulikuwa umefikia kukamilika sehemu ya chini yaani Under ground ambayo sehemu ya wanaume na wanawake ina ukubwa wa Squre mt. 176. Hafla ya ufungaji huu ilifanyika tarehe 10 Shaabani 1425 A.H. Sawa na tarehe 25 Septemba 2004 A.D. Ufungaji huo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa kitengo cha utamaduni cha Iran akishirikiana na Imamu wa msikiti wetu wa Khoja Shia Itha’ashariah Tanga. Baada ya hapo ilipofanywa harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti zilipatikana Shs 30,000/= tu. Hapa lazima kama utazingatia hali halisi utaona kwamba kuna mambo yanayopita chini kwa kuhakikisha zoezi zima kumalizika msikiti halipo.

Imam Ali bin Abi Talib (a.s) anasema:

"Imani ni kuchagua kusema ukweli hata kama utakudhuru, kuliko uongo ambao utakunufaisha. Na maneno yako yasiwe mengi kuliko matendo yako, na umuogope Mwenyezi Mungu pindi uwazungumzapo watu wengine."

Imam Khomei (R.A) anasema:

"Tekeleza wajibu wako katika dini lolote litakalokuwa na liwe"

pia kasema:

"Kukaa kimya ni sawa na kuunga mkono dhulma"

"Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule azuiaye Msikiti ya Mwenyezi Mungu ya kwamba humo lisitajwe jina lake na kujitahidi kuiharibu? Hao haitawafaa kuingia humo (Misikitini) ila kwa kuogopa, watapata fedheha katika dunia na Akhera wana adhabu kubwa. (Qur'an: 2:114)