' BOKO HARAM HAWANA UHUSIANO WOWOTE NA UISLAMU'



Ayatullah Naser Makarem Shirazi Marjaa Taqlidi amesema kuwa, kundi la wanamgambo wa Boko Haram wa Nigeria halina uhusiano wowote na dini tukufu ya Kiislamu. Ayatullah Makarem Shirazi amebainisha kwamba, wanamgambo wa Boko Haram wa Nigeria hawana wanachojua kuhusiana na Uislamu licha ya kuwa wanajinasibisha na Uislamu. Marjaa taqlidi huyo amesema kuwa, athari za kundi la Boko Haram chimbuko lake ni mti khabithi uliopandwa na makundi ya kitakfiri ambao athari zake zinajitokeza siku baada ya siku. Ayatullah Makarem Shirazi amesisitiza kwamba, ulimwengu unapaswa kufahamu kuwa, kundi la Boko Haram halitokani na Uislamu wala na Waislamu na kwamba, wanamgambo hawa ni washenzi ambao hata hawapaswi kuitwa binadamu. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa Waislamu kuwa macho na makundi ya kijahili kama haya ambayo hayatumii akali wala mantiki. Waislamu wanapaswa kuwa macho wasije wakawapa visingizio maadui wa Uislamu huko Ulaya na Marekani ili kuendesha propaganda chafu dhidi ya Waislamu, amesisitiza Ayatullah Makarem Shirazi. Chanzo cha habari (irib)

IRAN: MAREKANI HAITORUHUSIWA KUKANYAGA MSTARI MWEKUNDU.

Kamanda wa ngazi za juu katika jeshi la Iran amesema taifa hili halitaruhusu Marekani kukanyaga mstari mwekundu katika mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea kati ya Tehran na kundi la 5+1. Brigedia Jenerali Masoud Jazayeri amesema mafanikio ya kijeshi na kiulinzi ya Iran ni mstari mwekundu na kwamba Marekani isijaribu kuwashinikiza wanadiplomasia wa Tehran wakubali kulegeza kamba katika sekta hiyo. Afisa huyo mwandamizi wa jeshi la Iran amewataka wanadiplomasia wa Tehran kuwa macho dhidi ya njama hizo za Marekani na waitifaki wake kwenye kundi la 5+1.
Katika miezi ya hivi karibuni Marekani imekuwa ikisema kuwa, makubaliano ya mwisho ya Iran na kundi la 5+1 ambayo yatapelekea kuondolewa vikwazo vyote dhidi ya taifa hili sharti yajumuishe mambo mengine yasiyohusiana na kadhia ya nyuklia. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na suala la haki za binadamu, wafungwa wa kisiasa, na uwezo wa kijeshi wa Iran. Washington inataka Tehran ipunguze kasi katika jitihada zake za kujiimarisha kijeshi na kiulinzi. Iran imesisitiza kuwa mazungumzo yanayoendelea ni ya nyuklia tu na wala hakuna suala lingine likatalojadiliwa nje ya kadhia ya nyuklia.




NDEGE ZA ISRAEL ZAKIUKA TENA ANGA YA LEBANON.

Ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel kwa mara nyingine tena zimekiuka anga ya Lebanon. Jeshi la Lebanon limetangaza katika taarifa yake kwamba, ndege za kivita na za kijasusi za Israel zimepaa katika anga ya Lebanon kusini mwa nchi hiyo na katika maeneo mengine ya nchi hiyo. Taarifa ya jeshi la Lebanon imebainisha kwamba, hatua hiyo ya jeshi la utawala haramu wa Israel, kwa mara nyingine tena imekiuka wazi mamlaka ya kujitawala ya Lebanon na kupuuza pia azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.  Serikali ya Lebanon imelaani mara chungu nzima hatua za jeshi la Israel za kukiuka mara kwa mara anga na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.


Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, ni upumbavu wa mwisho wa adui kudhani kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itawekea mipaka na kikomo mipango yake ya makombora. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo wakati alipotembelea maonyesho ya mafanikio ya kikosi cha anga na anga za mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kusema mbele ya makamanda wa jeshi hilo kuwa, katika mazungumzo yanayoendelea kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1, Wamagharibi wamezuka na tamaa mpya za kutaka Iran iwekee kikomo mipango yake ya makombora licha ya kwamba madola hayo siku zote yanatoa vitisho vya kijeshi dhidi ya Iran, ndio maana kuwa na matarajio hayo ni upumbuvu wa mwisho.
Amesema, vipaji, uwezo na nia ya kweli ni mambo muhimu kwa ajili ya kuimarisha nguvu za kila taifa na amewataka viongozi wote wa Iran, kadiri watakavyokuwa na ubunifu na kufanya jitihada mbalimbali katika siasa za nje na mabadilishano ya kimataifa, lakini watambue kuwa hawapaswi kuyakwamisha na mazungumzo mahitaji ya Iran na baadhi ya masuala kama vikwazo, bali watafute njia nyingine za kutatua masuala hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, uadui dhidi ya taifa la Iran unatokana na kuwa taifa hili limeamua kuwa huru na kushikamana na Uislamu na Qur'ani.
Ameongeza kuwa: Uislamu na Qur'ani inayataka mataifa ya Waislamu kusimama imara juu ya miguu yao wenyewe na wategemee utambulisho wao wa Kiislamu, kibinadamu na kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na kutokubali kudhindwa na dhulma ya kimataifa, hivyo maadamu taifa la Iran litaendelea kushikamana na Uislamu, Qur'ani na malengo yake matukufu, basi uadui wa mabeberu nao utaendelea kuwepo.