SAVAK NA NJAMA YA KUZUSHA HITILAFU KWA VIONGOZI WA KIDINI NA MAULAMAA.


Baada ya kuachiwa huru Imam Khomein, Shirika la Ujasusi la Shah “Savak” lilitumia njama ya kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya Maulamaa na Viongozi wakuu wa dini kama njia ya kuvunja nguvu ya Wanamapambano katika vyuo vya kidini. Imam alivunja njama hizo, na kusema katika hotuba yake ya tarehe 15 Aprili 1964 katika Msikiti wa A’zam huko Qum kwamba: “Iwapo mtu atanivunjia heshima, akanipiga kofi usoni au akanipigia mwanangu kofi, naapa kwa jina la Mungu kwamba sitokuwa radhi kumuona mtu akisimama kunitetea dhidi ya mtu huyo. Sitokuwa radhi. Ninaelewa kwamba kuna baadhi ya watu wanaotaka kuzusha hitilafu katika jamii hii ima kwa makusudi au kwa kutojua. Mimi kutokea hapa nilipoketi ninaibusu mikono ya Marjaa wote huko Najaf, Mash-had, Tehran na kwengineko waliko. Ninaibusu mikono ya Maulamaa wa Kiislamu. Lengo letu ni kubwa zaidi kuliko mambo kama hayo. Ninanyoosha mkono wa udugu kwa mataifa yote ya Kiislamu na Waislamu wote duniani, Mashariki na Magharibi.”

Katika hotuba hiyo Imam Khomein aidha alifichua tena uhusiano wa siri wa Shah na Israel akanadi kwa sauti kubwa akisema: “ Enyi watu! Enyi walimwengu! Eleweni kwamba taifa letu linapinga mapatano ya aina yeyote na Israel. Anayefanya hayo si wananchi, na wala si wanazuoni wa dini. Dini yetu inatuamuru kutofanya mapatano na maadui wa Uislamu.”
Imam alimwita Shah kuwa ni “KIBWANA KIDOGO” na akamuhutubu kwa kusema: “Usifanye makosa. Hata kama Khomein atafanya mapatano na wewe Ummah wa Kiislamu hautapatana nawe. Usifanye makosa, kwani tungali katika handaki zetu za hapo awali. Tunapinga sheria zote zinazopingana na Uislamu. Tunapinga dhulma zote. Wananchi wanaichukia mno Israel na vibaraka wake na wanazichukia serikali zinazofanya mapatano na Israel.”