VIKWAZO VYA MAREKANI NI FAHARI KWA MUQAWAMA.



Harakati ya Muqawama ya Lebanon Hizbullah imesema kuwa vikwazo vya Marekani dhidi yake ni ishara ya fahari kwa muqawama. Nabil Qawooq, Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Hizbullah ni ishara ya fahari kwa wamapambano na kwamba vikwazo hivyo havitakuwa na athari yoyote hasi kwa Hizbullah.
Sheikh Qawooq ameyasema hayo leo akijibu mswada mpya uliowasilishwa na Congress ya Marekani dhidi ya Hizbullah ya Lebanon. Sheikh Nabil Qawooq ameongeza kuwa baada ya kushindwa waitifaki wake katika kukabiliana na wanamapambano huko Syria na Lebanon, Marekani kwa mara nyingine tena inaitishia Hizbullah na kwamba suala hilo linaonyesha kuzidi kushindwa Marekani na waitifaki wake katika kukabiliana na muqawama.
Nabil Qawooq, vile vile amesema kuwa, kushindwa magaidi wa Kitakfiri katika eneo la al Qalamun huko Syria ni pigo jipya na la kiistratejia kwa utawala wa Kizayuni. Amesisitiza kufungamana harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah kwa siasa zake huko Syria na kuongeza kuwa magaidi wa Kitakfiri huko Syria hawana mafanikio watakayopata na njama zao zitaambulia patupu.