IRAN YATIWA WASIWASI NA KUZIDI MACHAFUKO MISRI:


Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa inatiwa wasiwasi na kushtadi machafuko nchini Misri yanayosababishwa na ghasia kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji. Marzieh Afkham msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema leo kuwa, Tehran imekuwa ikifuatilia hali ya mambo ya Misri ambapo hivi karibuni machafuko yamesababisha mauaji na kujeruhiwa raia wengi wa nchi hiyo. Afkham ameeleza kuwa Tehran inasikitishwa na kuongezeka migogoro kila uchao kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji na kuzitaka pande mbili hizo kudumisha utulivu nchini humo na kutatua suutafahumu zao kwa mazungumzo ya kitaifa na kwa amani.

Misri imekumbwa na jinamizi la machafuko na migogoro tangu jeshi lilipompindua rais aliyechaguliwa na wananchi Muhammad Morsi, kusimamisha katiba na kuvunja Bunge mwezi Julai. Maelfu ya watu wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa tangu wakati huo kutokana na ghasia kati ya wafuasi wa Morsi, wanaompinga na vikosi vya usalama. (irib)


LEBANON: KIONGOZI WA AL-QAEDA AMEFIA HOSPITALINI:

Duru za Lebanon zimeripoti kuwa Majed al-Majed, kiongozi wa kundi la kigaidi lenye mfungamano na mtandao wa al Qaeda ambaye alikuwa ametiwa nguvuni kwa kuhusika na mlolongo wa mashambulio nchini humo amefia hospitalini. Duru hizo ambazo hazikutaka kutajwa zimethibitisha kuwa al Majed ambaye alikuwa na matatizo ya figo na hali yake kiafya ikiwa dhaifu amefariki. Kifo chake kimethibitishwa pia na Jenerali mmoja wa jeshi la Lebanon. Majed al-Majed ambaye alitiwa mbaroni siku ya Jumatatu iliyopita alikuwa kiongozi wa Brigedi za Abdullah Azzam, tawi la mtandao wa al Qaeda ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake za kigaidi katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati. Kundi hilo limehusika na shambulio la miripuko miwili ya mabomu iliyotokea tarehe 19 Novemba karibu na ubalozi wa Iran mjini Beirut, Lebanon. Watu wasiopungua 25 akiwemo Mkuu wa Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon Hujjatulislam Ibrahim Ansari waliuawa na wengine zaidi ya 160 walijeruhiwa katika shambulio hilo. Awali balozi wa Saudi Arabia nchini Lebanon Ali Saeed Asiri alikuwa ameitaka serikali ya Lebanon imkabidhi al-Majed ambaye ni raia wa Saudia kwa utawala huo wa kifalme endapo utambulisho wake ungethibitika. Itakumbukwa kuwa tarehe 3 ya mwezi uliopita wa Disemba, Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah alisema kwamba Saudi Arabia ndiyo iliyohusika na shambulio dhidi ya ubalozi wa Iran na kusisitiza kwamba hana shaka yoyote kuwa shirika la intelijinsia la Saudia lina mafungamano ya karibu na kundi la kigaidi la Brigedi za Abdullah Azzam. Majed al-Majed, gaidi aliyekuwa akisakwa na nchi nyingi aliwahi kuweko nchini Syria akishirikiana bega kwa bega na kundi la kigaidi la al-Nusra katika vita dhidi ya serikali ya nchi hiyo…/ (irib)


 WAPALESTINA WAPINGA KUREFUSHWA MAZUNGUMZO:

Kiongozi wa wawakilishi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika mazungumzo ya mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel amesema mamlaka hiyo inapinga kurefushwa kwa namna yoyote muda wa mazungumzo hayo. Saeb Uraiqat ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa leo na gazeti la Al Sharqul Awsat na kufafanua kwamba Wapalestina hawatokubali pendekezo lolote la kurefusha hata kwa siku moja muda wa mazungumzo ya mapatano na Israel na kwamba haiyumkiniki kukubali pendekezo kama hilo. Uraiqat ameongeza kuwa lengo la kufanya mazungumzo ya mapatano ni kutafuta mwafaka juu ya masuala wanayohitilafiana Wapalestina na Israel na si kutafuta mwafaka juu ya kurefusha muda wa mazungumzo, hivyo kama Israel ina nia ya kweli ya kufikia makubaliano ya kuleta amani katika Mashariki ya Kati inapaswa iafiki kuundwa nchi huru ya Palestina katika eneo la mipaka ya mwaka 1967 na mji mkuu wake ukiwa ni Quds tukufu. Mazungunmzo ya mapatano kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel yalianza tena mwezi Julai mwaka jana kwa upatanishi wa Marekani baada ya kusita kwa miaka kadhaa kutokana na hatua ya Tel Aviv ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina. Siku ya Alklhamisi iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry aliwasili Mashariki ya Kati kwa lengo la kuwapatanisha tena viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na wa utawala wa Kizayuni wakubali kuendelea na mazungumzo…/ (irib)
 

KUTESWA WATOTO WA KIPALESTINA NDANI YA JELA ZA UTAWALA WA ISRAEL:
 
Hatua ya kuteswa na kupigwa watoto wa Kipalestina wanaoshikiliwa ndani ya jela za utawala wa Israel imeibua malalamiko mengi kutoka jumuiya za Kipalestina na kuakisiwa pia na jumuiya za kutetea haki za binadamu na vyombo vya kupasha habari vya eneo la Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla. Gazeti la al Watan linalochapishwa Saudi Arabia liliandika katika toleo la jana Ijumaa, jinsi watoto wa Kipalestina wanavyoteswa kwenye jela za Israel, na kufafanua kuwa, baadhi ya watoto hao kwa miezi kadhaa sasa wamefungiwa ndani ya seli ambazo juu ziko wazi, katika msimu huu wa baridi kali. Ripoti hiyo inaeleza kuwa, watoto hao wa Kipalestina  wanatishiwa  kutendewa vitendo vya kinyama vya ubakaji, na baadhi yao wanafunguliwa mashtaka mahakamani bila ya mawakili wa kuwatetea. Ripoti hiyo imeeleza kuwa, tuhuma zinazowakabili watoto wengi wa Kipalestina ni kuwatupia mawe askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel.  Ripoti hiyo inaeleza kuwa, asilimia 74 ya watoto wa Kipalestina wanakabiliwa na mateso ya kupigwa mara kwa mara kwenye jela za Israel. Ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye gazeti la al Watan imeeleza kuwa, utawala wa Israel unawaweka watoto wenye umri wa miaka 14 kwenye  seli za watu wazima, suala ambalo linakinzana na misingi ya haki za binadamu. Hii ni katika hali ambayo, kanali ya televisheni ya al Aalam iliripoti hivi karibuni kuwa, tokea mwaka 2009 hadi sasa, makumi ya watoto wa Kipalestina wamepoteza maisha yao ndani ya jela za Israel wakati wakisailiwa na majeshi ya Israel. Ripoti hiyo ya al Aalam ilimnukuu mtoto mmoja wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 14 akielezea machungu na mateso wanayoyapata watoto wa Kipalestina ndani ya jela za Israel. Mtoto huyo wa Kipalestina anaeleza kuwa, askari magereza wanapoingia kwenye vyumba vya kusaili watoto wa Kipalestina, huvikamata vichwa vya watoto hao na kuvipigisha ukutani, kisha huwapiga ngumi, vibao na  mateke mwilini. Kijana huyo anayekaa katika kijiji cha Husan huko Baitul Lahm ameeleza kuwa, askari wa Israel huwalazimisha kukubali kwamba waliwarushia mawe askari wa Israel, na kama watakataa kukiri  wanatishiwa kufanyiwa vitendo vya kinyama vya unyanyasaji wa kijinsia, kubakwa na kunajisiwa. Taasisi ya Kutetea Haki za Binadamu ya 'Betsalem' ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu  imeeleza kuwa, hadi kufikia Juni 2013, Wapalestina wasiopungua 64 waliuawa shahidi kwenye seli za kituo  kikuu cha polisi huko Israel. Taasisi  hiyo imeeleza kuwa, kati ya wahanga hao, 56 walikuwa watoto wanaotoka katika miji minane ya eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Kabla ya hapo, Waziri anayeshughulikia masuala ya mateka wa Kipalestina aliutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutenda jinai za kivita dhidi ya mateka wa Kipalestina walioko gerezani na hasa watoto wadogo. Duru za Kipalestina zinaeleza kuwa, watoto wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye gereza la Hasharon, kwa muda mrefu sasa hawapati usingizi na wala hawapewi huduma za matibabu pindi wanapokumbwa na maradhi. Waziri huyo wa Kipalestina amesema kuwa, viongozi wa magereza kwa makusudi kabisa huwatelekeza  wafungwa wagonjwa bila ya kuwapatia matibabu, hadi wanapokaribia kupatwa na umauti. Hii ni katika hali ambayo, Taasisi ya Wafungwa wa Kipalestina ilitangaza kuwa, watoto 200 wa Kipalestina ni miongoni mwa wafungwa zaidi ya elfu tano wakubwa wanaoshikiliwa ndani ya jela na magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel. (irib)