Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuheshimiwa makubaliano ya nyuklia yaliyotiwa saini tarehe 24 Novemba 2013 kati ya Iran na kundi la 5+1 ndilo sharti la kuendelea na mazungumzo ya nyuklia.
Ayatullah Hashemi Rafsanjani amesema hayo leo wakati alipoonana na kundi la bunge la Kamati ya Siasa za Nje ya Baraza la Sanate la Italia hapa mjini Tehran na kujadiliana nalo mustakbali wa mazungumzo hayo ya nyuklia na kuongeza kuwa, baada ya kupita miaka mingi ya kulifanyia uadui taifa la Iran na kueneza chuki dhidi ya taifa hili duniani, hivi sasa Wamagharibi wamo katika mtihani mkubwa na wanapaswa waheshimu ahadi zao katika makubaliano ya Geneva ili kuonesha nia yao njema.
Ayatullah Rafsanjani aidha amesema, mazungumzo na maelewano ndiyo njia bora ya kutatua matatizo na migogoro ya eneo na akaongeza kuwa Marekani na waitifaki wake wajue kwamba mgogoro katika eneo hili hauinufaishi nchi yoyote ile na kwamba tatizo hilo haliwezi kutatuka kwa uingiliaji wa kijeshi. (irib)