UMUHIMU WA KUTAFITI NA KUHIFADHI HISTORIA YA UISLAMU.


Kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja sasa nimekuwa nikifanya utafiti na kupiga picha juu ya Misikiti ya kale nchini Tanzania (ikiwemo Ugunja na Pemba). Kwa lengo la kujua historia ya Uislamu Tanzania. Katika utafiti huu nimejifunza mengi, lakini hali ya Misikiti hiyo ya kale sio nzuri na inatia aibu Waislamu. Japokuwa kuna maeneo ambayo yametengwa, na Serikali ya Muungano na ya Zanzibar, kuwa ni maeneo ya kihistoria na utalii, kama vile Mikindani,Kilwa,Tongoni, na Pemba, lakini ukweli ni kwamba Misikiti haitunzwi na hakuna dalili kuwa ukarabati utafanyika hii karibuni, na hata Mwakani. Msikitini wa kala wa Mkambuu unaweza kuchukuliwa na bahari wakati wowote kama ambavyo visima vya maji vilivyoliwa tayari. Msikiti wa Mvita pale Mikindani (Pemba mnazi) umebaki jina tu, maana nje ndani umeharibika, na majani yanaunyemelea. Msikiti wa Ijumaa wa Pemba Mnazi, kwa kweli unatia aibu. Na Misiikiti yote hii ina umri wa zaidi ya miaka mia moja. Kituko kikubwa zaidi ni kule Bagamoyo. Nilikuwa napasaka mahali ambapo Bushiri-binSalim al-Harith (Mpinzani wa utawala wa Wajerumani), alipojenga Msikiti. Ilitumia siku mbili kujua mahala hapo. Na wazee wa Kiislamu wa miaka 65 na zaidi wa eneo hilo la Nzole walikuwa hawajui ulipo. Nilipofika eneo hilo nikakuta makaburi ya Mama Muislamu, Kaunde bin Mwalimu, anaonekana ni Mnyamwezi, liko chini ya mti wa mwembe halina historia wala tarehe. Ingawa niliambiwa hapo alikuwa akiishi Muarabu aliyekuwa tajiri sana miaka ya 1950. Nikakuta Msikiti uliobaki Nguzo nne tu. Na nilipofika kwenye Msikiti wa Bushiri, nikakuta hakuna kitu zaidi ya dalili ya ujenzi kuwa hapo paliwahi kuwa makazi. Japo kumetokewa Waislamu nisiowajua wamejenga msingi wa tofari tano kuzunguka Msikiti ulivyojengwa. Na ndio mwisho. Na aliyefanikisha nikamuona kaka wa Kisukuma, mhamiaji, ambaye hakuwa Muislamu. Baadaye nikagundua kuwa kuna kijiji kinaitwa Utondwe, kusini ya mji wa Saadani, ambacho kilikuwepo kabla ya miaka ya 1400. Kuwa kijiji hicho kilikuwa maarufu kwa Uislamu, biashara ya chumvi na watu wake hodari kwa kupiga mishale vitani. Haya aliyaandika Bwana Al-Masood. Msafiri na mwandishi maarufu enzi hizo, na kushadidiwa na Ibn Batuta katika maandishi yake ya Periplus. Nilisafiri kwa pikipiki kwa kilo Meta 50 kwenda na 50 kurudi. Nikaufikia Msikiti huo wa Utondwe. Lakini nilisononeka, kwani Msikiti ulikuwa katikati ya msitu mkubwa. Hauna mtunzaji na kaburi la Imam na Bint yake yako vcichakani. Kuna dalili kuwa kuna watu huenda kule kwa Hijja na Dua, lakini hakuna matunzo yoyote. Makaburi mengine yamefukiwa na mchanga, mengine yameliwa na mto Utondwe. Nina ushahidi wa picha kuwa maandishi ya Kiarabu yaliyokuwa katika Makaburi yalichukuliwa na watafiti wa Kizungu, na hatuwezi kuyapata. Je Waislamu mnafiriaje juu ya hili? Tumezembea kwa kudhani kuwa tunaweza kuaachia wasio sisi kutuandikia historia, na kututunzia pahala petu pa Ibada. Historia inaimarisha imani, na kuwasaidia Waumini kujua wapi wametokea na wapi walipo, na nini kifanyike kuikuza imani yao. Wengi wa Waislamu wanajua wapi dini hii Tukufukufu ilianzia, Makka, Madina na kwengineko. Lakini hawajui dini hii ilikujaje Tanzania, na ilisambaaje kafika huko iliko sasa hivi. Na nani aliwajibika. Ni wajibu wa Waislamu wenyewe kufikiria mbinu bora ya kutunza amali hii muhimu. Wabillah Tawfiq! Wasalaam. Na: Mohammad Mustapha Kayoka, barua pepe: ckayoka28@yahoo.com