SAYYED HASSAN NASRULLA: SAUDIA NDIO KIKWAZO CHA UTULIVU WA SYRIA NA LEBANON.
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah
amesema kuwa Saudi Arabia ndiyo kikwazo kikuu cha kupatikana amani na
utulivu katika nchi za Syria na Lebanon. Huku akiashiria makundi ya
kigaidi yaliyohusika katika milipuko kadhaa ya mjini Beirut, Sayyid
Nasrullah amesema Saudia ndio kikwazo kikuu cha amani na utulivu wa
Lebanon na Syria. Ameashiria mapigano na milipuko iliyotokea katika mji
wa Tripoli kaskazini mwa Lebanon na kuongeza kuwa, matukio yanayojiri
mjini humo yanatokana na njama za maadui wanaokusudia kuitumbukiza
Lebanon katika vita vya ndani. Sambamba na kusisitiza juu ya udharura wa
kutatuliwa mgogoro wa kaskazini mwa Lebanon, Katibu Mkuu wa chama cha
Hizbullah amesema kwamba, serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka za
kutafuta mgogoro wa eneo hilo.
Katika upande mwingine, Sayyid
Nasrullah amesema, suala la kupindua kijeshi serikali ya Syria ni chaguo
lililoshindikana na kwamba pande zote isipokuwa Saudia, zinataka
kutatuliwa kisiasa mgogoro wa Syria. Sayyid Nasrullah vilevile
amesisitiza juu ya udharura wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa
nchini Lebanon chini ya uongozi wa Tamam Salam na kuongeza kuwa, Saudi
Arabia inazuia kuundwa serikali mpya nchini humo.
Kuhusiana na
hilo mtandao wa habari wa Syria umeashiria mapigano yaliyotokea kati ya
watu wenye silaha katika mji wa Tripoli kaskazini mwa Lebanon na kueleza
nafasi haribifu ya Wasaudi na mamluki wao katika eneo hilo. Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, mara zote makundi yenye silaha ya kigaidi na wafuasi
wao nchini Syria yanapopata kipigo kikali huanzisha mapigano katika eneo
la 'Jabal Muhsin' kwenye mji wa Tripoli .
Wachambuzi wa mambo
wanasema kuwa, ukosefu wa utulivu katika mji wa Tripoli kaskazini mwa
Lebanon unachangiwa na mgogoro wa Syria. Katika mapigano ya siku kadha
zilizopita kati ya wafuasi na wapinzani wa serikali ya Syria kwenye
maeneo ya Jabal Muhsin na Babul Bitana kwenye mji huo, watu 12 waliuawa
na wengine wasiopungua 100 wakiwemo askari 17 wa jeshi la Lebanon
kujeruhiwa. Serikali ya Lebanon imetangaza kuwa, imekabidhi jeshi la
Syria jukumu la kusimamia kikamilifu usalama wa mji wa Tripoli kwa muda
wa miezi 6.
Allama Sheikh Afifa Nablisi ambaye ni mkuu wa
Baraza la Maulamaa wa Jabal Amil nchini Lebanon ameielezea hali ya hivi
sasa ya mji wa Tripoli kuwa ni ya hatari sana na kusisitiza kuwa, kuna
haja jeshi na serikali zishughulikie haraka hali ya kaskazini mwa
Lebanon ili kuzuia mapigano zaidi. Pia Sheikh Mahir Hamud mmoja wa
viongozi wa Kisuni wa Lebanon sambamba na kukosoa machafuko
yanayosababishwa na makundi ya takfiri yanayofanyika kwa kutumia dini,
amesisitiza juu ya udharura wa kudumishwa uungaji mkono kwa muqawamah
dhidi ya adui Mzayuni. Sheikh Mahiz Hamuz ameongeza kuwa, utawala wa
Kizayuni wa Israel ndiye adui mkubwa wa makundi ya mapambano na kwamba
Israel inapanga njama za pande zote dhidi ya muqawamah na kutekeleza
jinai za aina mbalimbali.
Utawala wa Kizayuni wa Israel na
Saudia zinaripotiwa kufanya njama dhidi ya taifa la Lebanon katika hali
ambayo, siku ya Jumanne mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa Hizbullah
alishambuliwa na kuuawa shahidi na watu waliokuwa na silaha mjini
Beirut. Hizbullah imetangaza kuwa utawala wa Kizayuni ndio uliohusika
moja kwa moja mauaji ya kamanda huyo.