WANIGERIA WATAKA KUACHILIWA HURU SHEIKH ZAKZAKY.

Wananchi wa Nigeria wameandamana na kutoa wito wa kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Kanali ya Press TV inaripoti kwamba, wakazi wa mji wa Abuja nchini Nigeria jana walifanya maandamano, ambapo mbali na kulalamikia vitendo vya utumiaji mabavu na mashinikizo ya serikali dhidi ya Waislamu wametaka kuachiliwa huru mara moja, Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa kizuizini kwa miezi kadhaa sasa.
Waandamanaji hao walisikika wakipiga nara za kukemea vikali utumiaji mabavu na mauaji ya vikosi vya usalama vya Nigeria dhidi ya Waislamu katika mji wa Zaria miezi kadhaa iliyopita.

Maandamano ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Waandamanaji hao wametia saini barua ambayo wameituma kwa Kamisheni ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini humo wakitaka kuachiliwa huru mwanazuoni huyo wa Kiislamu.
Ripoti zinasema kuwa, hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky kizuizini ni mbaya. Pamoja na hayo, serikali ya Nigeria imekataa kumuachilia huru alimu huyo wa Kiislamu.
Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, jicho la kushoto  la Sheikh Zakzaky limepofuka na kwamba maafisa usalama wamekuwa wakikataa mwanazuoni huyo wa Kiislamu kupatiwa matibabu.
Wananchi wa Nigeria wamekuwa wakiandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kuachiwa huru haraka kiongozi huyo wa Kiislamu.

Jeshi la Nigeria lilipowashambulia Waislamu mjini Zaria Disemba 2015
Itakumbukwa kuwa Disemba mwaka jana askari wa jeshi la Nigeria walishambulia marasimu ya kidini ya Waislamu wa Kishia katika mji wa Zaria kwa kuwatuhumu kuwa walizuia msafara wa mkuu wa jeshi na pia kujaribu kumuua, madai ambayo yalikanushwa na Waislamu hao. (parstoda)