Harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imelaani taarifa iliyotolewa karibuni na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P)GCC ya kuliweka jina la harakati hiyo kwenye orodha ya "mashirika ya kigaidi" na kueleza kwamba hatua hiyo imechukuliwa katika muelekeo wa pamoja wa Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mrengo wa Hizbullah ndani ya Bunge
la Lebanon umetoa taarifa na kueleza kwamba hatua hiyo ya nchi wanachama wa
(P)GCC ni huduma kubwa ambayo nchi hizo imetoa kwa utawala wa Kizayuni baada ya
miongo saba ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Palestina.
Mbegu za awali za harakati ya
muqawama ya Hizbullah ya Lebanon zilichipua katika muongo wa 1980 baada ya nchi
hiyo kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la utawala wa Kizayuni. Mnamo
mwaka 1982, jeshi la Israel lilivuka mpaka wa Lebanon hadi ndani ya ardhi ya
nchi hiyo na kusonga mbele hadi mji mkuu Beirut.
Kutokana na kutawanywa vifaru vya
Israel kuanzia kusini mwa Lebanon hadi Beirut na kuingia askari wa jeshi la
wanamaji la Marekani na wa nchi za Magharibi ndani ya ardhi ya Lebanon na
kuanzisha vituo vyao mjini Beirut, hapo ndipo Hizbullah ilipojitosa kwenye
ulingo wa kukabiliana na hujuma za wavamizi wa Kizayuni na waungaji mkono wao
ili kuikomboa ardhi ya Lebanon na uvamizi huo.
Matokeo na matunda ya miongo miwili
ya mapambano ya vikosi vya muqawama dhidi ya jeshi la utawala wa Kizayuni
lililojizatiti kwa silaha za kisasa lilizopatiwa na Marekani yalikuwa ni
kuulazimisha utawala huo urudi nyuma kwa kuondoka mjini Beirut na kwenda kupiga
kambi kusini mwa Lebanon.
Hatimaye mnamo mwezi Mei mwaka 2000,
katika kipindi cha Uwazri Mkuu wa Ehud Barak, jeshi la utawala wa Kizayuni
lilifungasha virago usiku usiku na kukimbia kutoka kusini mwa Lebanon huku
likikiri kuwa limeshindwa kukabiliana na wanamapambano wa muqawama na
kulazimika baada ya miaka 22 kulifunga faili la uvamizi na kuikalia kwa mabavu
Lebanon.
Na hii ni pamoja na kwamba mnamo
mwaka 2006, kwa mara nyengine tena utawala wa Kizayuni ulipigishwa magoti
katika medani ya mapambano ulipofedheheshwa katika vita vya siku 33; ambapo
baada ya mwezi mmoja wa kuishambulia Lebanon kwa makombora ya angani, nchi kavu
na baharini, hatimaye jeshi la utawala huo likatangaza usitishaji vita wa
upande mmoja na kuacha uhasama wa mapigano; na hivyo kuhuisha tena kumbukumbu
ya kukombolewa kusini mwa Lebanon na harakati ya muqawama huku jeshi hilo
likikubali kimadhila kuwa limeshindwa na Hizbullah katika vita hivyo.
Tukiyatalii matukio yaliyojiri
katika miongo iliyopita itatubainikia ni jinsi gani ulimwengu ulioparaganyika
wa Waarabu, ukishirikiana na Marekani na utawala wa Kizayuni ulivyoyasaliti
malengo matukufu ya Palestina na vipi umekuwa ukitekeleza kutokea nyuma ya
pazia njama dhidi ya harakati za muqawama za Palestina na Lebanon. Mpaka kufkia
hadi kuwa utawala wa Kizayuni ambao hapo kabla ulikuwa ukitamani kuanzisha
uhusiano na nchi za Kiarabu na kuondokana na hali ya kutengwa, sasa
unazishurutisha nchi za Kiarabu ziiweke harakati ya muqawama ya Hizbullah
kwenye faharasa ya makundi ya kigaidi ili kuanzisha uhusiano na nchi hizo.
Ulimwengu wa Waarabu umefumbia macho
jinai za Israel na sera za kujipanua za utawala huo haramu ambao umelitia eneo
la Mashariki ya Kati kwenye hilaki ya vita kadhaa vikubwa na angamiizi, na
badala ya kushika panga zao kukabiliana Wazayuni maghasibu wanaelekezeana na
kuhasiriana wenyewe kwa wenyewe.
Utawala wa Aal Saud unaendeleza
mauaji nchini Yemen huku wananchi wa Bahrain nao wakiandamwa na wimbi la hujuma
na ukandamizaji wa muungano wa nchi za Kiarabu. Katika nchi za Syria na Iraq
pia magaidi na matakfiri wamezigeuza ardhi za nchi hizo machinjio ya raia wasio
na hatia.
Na hii ni katika hali ambayo nyuma
ya moto wote huo wa kuchochea uadui na mifarakano kuna fedha na silaha za
Marekani na utawala haramu wa Israel.
Kutokana na yote hayo haibakii tena
chembe ya shaka kuwa taarifa ya mawaziri wa nchi za Kiarabu wanachama wa (P)GCC
dhidi ya Hizbullah ni hidaya ya tunu na yenye thamani kubwa ambayo umetunukiwa
utawala wa Kizayuni wa Israel.../