"KUSHIRIKI WAIRAN KATIKA UCHAGUZI NI ISHARA YA UELEWA"

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema kujitokeza kwa wingi Wairani katika chaguzi mbili za leo ni ishara ya kuwa hai na kuwa na ufahamu na uelewa taifa la Iran.
Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqui katika hotuba zake za Ijumaa ameonyesha furaha yake kutokana na usalama na utulivu uliotawala zoezi la upigaji kura nchini kote, na kueleza kwamba:"Watu wa Iran wangali wanajitokeza kwa hamasa katika medani ili kulinda Mapinduzi ya Kiislamu; na moja ya dhihirisho hilo ni kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa leo wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge, na Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu."
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ameashiria njama za maadui za kutaka kujipenyeza na kueneza satwa yao ya kibeberu Iran hasa baada ya mapatano ya nyuklia. Amesema kubakia msingi wa Jamhuri katika mfumo kunategemea kujitokeza daima wananchi katika uchaguzi ambao huwa wanaainisha hatima na mustakabali wa Iran. Aidha amesema kubakia msingi wa Uislamu katika mfumo hutegemea Faqihi Mtawala.
Sheikh Kadhim Siddiqui amebainisha mbinu mbali mbali anazotumia adui kupenya Iran na kusema moja kati ya mbinu hizo ni ujasusi au kupewa mafunzo maafisa wa serikali wakiwa wanafunzi katika madola ya kigeni.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa amesema maadui wa mfumo wa Kiislamu wafahamu kuwa hadi leo Iran haijakubali kuwa chini ya satwa ya dola lolote la kigeni na nchi hii kamwe haitasalimu amri mbele ya adui yeyote.
Duru ya kumi ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na ya tano ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu zimefanyika huku mamillioni ya wananchi wakijitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura.