Abdul Malik al Houthi kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa utawala wa Israel, Marekani na baadhi ya waitifaki wao zinataka kuufanya mtumwa Umma wa Kiislamu.
Abdul Malik al Houthi ameongeza kuwa la kusikitisha ni kuwa watawala wa baadhi ya nchi za Kiislamu wanakiuka sheria za Kiislamu. Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameyasema hayo akilihutubia taifa Jumatano hii. Abdul Malik al Houthi amesema, maadui wa Umma wa Kiislamu wanataka kuiona Yemen na eneo zima likiwa vipande vipande na kugawanyika na ili waweze kudhibiti maliasili za nchi hiyo ya Kiarabu.
Amesema sera za Saudi Arabia zinafanana na zile zinazotekelezwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zengo lake ni kuuangamiza Umma wa Kiislamu bila ya nchi hizo kupata hasara.
Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi ya kijeshi nchini Yemen tarehe 26 mwezi Machi mwaka huu lengo lake likiwa ni kuisambaratisha harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Rais mtoro wa Yemen Abdu-Rabuh Mansour Hadi.