MAMILIONI YA MAHUJAJI WAELEKEA MINA, KESHO ARAFA.

Mamilioni ya mahujaji waliokwenda kutekeleza ibada ya Hija katika mji mtakatifu wa Makka leo wameelekea Mina katika siku ya Tarwiya ambako watakesha leo na kuamkia Arafa mapema kesho asubuhi.
Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu wameshinda katika eneo hilo la Mina lililoko umbali wa kilomita 7 kutoka Masjidul Haram. Siku hii ya leo tarehe 8 Dhulhija ilipewa jina la Siku ya Tarwiya kwa maana ya kujitosheleza kwa maji kwa sababu zama hizo mahujaji walikuwa wakijizatiti kwa maji ya kutosha kwa ajili ya kisimamo cha siku ya Arafa tarehe 9 Dhulhija ambayo ni nguzo muhimu ya ibada ya Hija. Mahujaji kesho watashinda Arafa wakiomba dua na kumtaradhia Mola Muumba na wataondoka hapo magharibi wakielekea Muzdalifa.
Idara inayosimamia Hija nchini Saudi Arabia imetangaza kwamba imetayarisha mahema laki moja na sitini elfu yanayoweza kukabiliana na moto kwa ajili ya mahujaji katika eneo la Mina. Mahujaji zaidi ya milioni mbili wanatekeleza ibada ya Hija mwaka huu katika mji mtakatifu wa Makka.
Hadi sasa mahujaji 332 wamepoteza maisha kwa sababu mbalimbali tangu Waislamu kutoka meneo mbalimbali ya dunia wawasili katika ardhi ya Hijaz kutekeleza ibada ya Hija.