TAHADHARI KUHUSU ISRAEL KUIBA VYANZO VYA NISHATI LEBANON.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia vibaya pengo la kisiasa nchini Lebanon, hasa kutokuwepo kwa rais, kuiba na kupora utajiri wa gesi na mafuta ya nchi hiyo. Tokea tarehe 25 Mei mwaka 2014 baada ya kumalizika muhula wa urais wa Michel Suleiman, Lebanon imekuwa na pengo la kisiasa kwa sababu ya hitilafu miongoni mwa wanasiasa nchini humo ambao wameshindwa kuafikiana kuhusu nani anapaswa kuchukua nafasi ya urais. Kadhia hii imepelekea kuibuka matatizo makubwa katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Gazeti la As Safir la Lebanon katika toleo lake la hivi karibuni limeandika kuhusu namna utawala wa Kizayuni unavyopora mafuta na gesi ya Lebanon. Wazayuni wanatumia vibaya pengo hilo la uongozi Lebanon na pia kupuuza na kukiuka sheria za kimataifa katika kupora kwa wingi utajiri wa mafuta na gesi ya nchi hiyo. Gazeti hilo limekosoa vikali serikali ya Lebanon kwa kutozingatia kadhia ya Wazayuni kuiba mafuta na gesi ya nchi hiyo katika maeneo ya pwani. As Safir limeitaka serikali kuchukua hatua za haraka na kuwasiliana na taasisi za kimataifa ili kuzuia uporaji zaidi wa utajiri huo wa nishati muhimu ya Lebanon.
Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berry amesisitiza umuhimu wa Walebanon kunufaika na utajiri wao wa mafuta na gesi na kuelezea matumaini yake kuwa mwaka huu wa 2015 utakuwa mwaka wa kuhuisha haki za Lebanon katika sekta ya mafuta. Berri ameongeza kuwa, suala la kutokuwepo serikali Lebanon na kujishughulisha nchi hiyo na vita dhidi ya ugaidi ni mambo ambayo yameupa utawala wa Kizayuni mwanya wa kuiba mafuta na gesi ya nchi hiyo. Weledi wa mambo ya kisiasa wanaamini kuwa, hatua ya utawala haramu wa Israel ya kuiba gesi na mafuta ya Lebanon ni jambo ambalo litapelekea viongozi wa nchi hiyo kuchukua hatua za dharura kutekeleza mkakati wa kuchimba utajiri wake huo ili kuiwezesha nchi hiyo kupata pato zaidi na kuinua uchumi wake dhaifu.
Wakuu wa Wizara ya Uchumi ya Lebanon wanasema katika hali ambayo nchi hiyo ina deni la dola bilioni 66, kunufaika na mafuta yatakayochimbwa kunaweza kuwa chanzo kizuri cha pato katika kuimarisha uchumi na kupunguza madeni ya kigeni.
Kwa kuzingatia hayo, kutokana na kuwa Lebanon haina vyanzo vya fedha na wataalamu wanaoweza kutoa msukumo unaohitajika katika sekta za mafuta na gesi, mashirika ya kimataifa yatapewa kandarasi za kuchimba mafuta na gesi katika pwani ya nchi hiyo na hivyo kuuruhusu utawala wa Kiayuni kuendelea kupora utajiri wa nchi hiyo. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Bahari ya Mediterranean ina hifadhi kubwa ya gesi na mafuta hasa katika maeneo ya pwani ya Lebanon, Cyprus, Syria na Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Kwa msingi huo utawala wa Israel unatekeleza njama mbali mbali ili kuteka na kupora aghalabu ya utajiri huo jambo ambalo limepelekea kuibuka hisia kali dhidi ya utawala huo ghasibu miongoni mwa mataifa ya eneo hilo. Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/…/49830-tahadhari-kuhusu-israel-ku…