DAESH WAHUJUMU TENA MSIKITI NCHINI SAUDIA.


Watu wanne wameuawa nchini Saudi Arabia baada ya gaidi mmoja wa kundi la kitakfiri la Daesh kuulenga tena msikiti wa Mashia katika mji wa Dammam mkoa wa mashariki mwa nchi hiyo. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imesema hujuma hiyo imejiri katika eneo la kuegeshea magari la Msikiti wa Imam Hussein AS mjini Dammam yapata kilomita 400 kutoka mji mkuu, Riyadh. Vyombo vya habari vya Saudia vimemnukulu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani akisema gaidi aliyekuwa amejifunga mabomu, ambaye alikuwa amevaa nguo za kike, alijiripua katika eneo la kuegeshea magari msikitini hapo baada ya gari lake kusimamishwa na maafisa usalama. Hadi sasa watu wanne wamethibitishwa kuuawa katika hujuma hiyo na baadhi ya duru zinasema kati ya waliofariki ni gaidi huyo. Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza rasmi kuhusika na hujuma hiyo. Shabulio hilo la leo limekuja wiki moja tu baada ya mlipuko wa bomu ndani ya Msikiti wa Imam Ali AS katika eneo la al-Qadeeh mkoani Qatif, ambapo waumini 21 waliuawa shahidi wakiwemo watoto wawili. Matakfiri wa kundi la kigaidi la Daesh walisema wao ndio walifanya hujuma hiyo ya Ijumaa iliyopita.