SHAHADAT: FATMA ZAHRA (a.s)

1- Mola mwingi wa Rehema, twakushukuru Jaliya
Mtume mpe salama, na watoto wake piya
Ni hao waliozama, kitabu kukichambuwa
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

2- Kajitokeza Fatima, mengi ametufanyiya
Apendeza kila zama, kama alivyo Nabiya
Ibilisi amezama, hawezi kumuingiya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

3- Muhammadi amesema, kwa kurudiarudiya
Kipande changu cha nyama, ni Fatima Zahriya
Na mimi yananiuma, mabaya akifanyiwa
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

4- Huyu mwanangu Fatima, hana wa kumfikiya
Wanawake wote wema, hadi iumbwe duniya
Hadi siku ya kiyama, Fatima ni malkiya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

5- Nyumbani kwa huyu mama, ndipo pa kukimbiliya
Masikini na yatima, wote walimtambuwa
Yeyote aliyekwama, kwake alikimbiliya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

6- Aliletewa Fatima, kikongwe kimezidiwa
Kilichokuja kwa wema, Madina kumtembeleya
Na njaa inamuuma, akamwambia Nabiya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

7- Apelekwe kwa Fatima, hadi alipoingiya
Akaambiwa Fatima, babu kaharibikiwa
Muhammadi kamtuma, uje kumsaidiya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

8- Akiba yake Fatima, alikwisha kuitowa
Mkufu wake Fatima, mzee kaupokeya
Hutoki kwa huyu mama, bila kukuzawadiya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

9- Akarudi kwa heshima, mkufu kashikiliya
Sahaba mwenye heshima, mkufu kaununuwa
Babu kataja gharama, palepale akapewa
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

10- Mkufu wake Fatima, ajabu karejeshewa
Mkufu wa huyu mama, mzee kasitiriwa
Kakombolewa mtumwa, ajabu ukatejea
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

11- Hivi alivyo Fatima, hivi ndivyo sawasawa
Wazazi wake Fatima, ni Khadija na Nabiya
Bahari mbili za wema, ndimo alimotokeya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

12- Alipokufa Hashima, vurugu ilitokeya
Kwenye nyumba ya Fatima, watu wamekimbiliya
Akaumizwa Fatima, dini akiiteteya
Kafariki Bi Fatima leo Tunamliliya

13- Afya ya bibi Fatima, ikaanza kupoteya
Hapana tena uzima, tangu kufa kwa Nabiya
Akiuwawa kinyama, usije kumkimbiya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

14- Akausiya Fatima, Zainabu kumwambiya
Husseni kumtizama, mwanangu nakuusiya
Akiuwawa kinyama, usije kumkimbiya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

15- Ali akamtazama, nae kamchaguliya
Akamuowe Fatima, wajina ametuliya
Upate mtoto mwema, mlinzi wa Huseiniya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

16- Maagizo ya Fatima, kamwe hayakurejeya
Abbasi mtoto mwema, Mola akawaleteya
Shujaa asiyekoma, hadi kaaga duniya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

17- Kwa leo bibi Fatima, aiaga duniya
Kaacha mipango vyema, kwa mila yake Nabiya
Tangulia ee Fatima, katuombee shifaa
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

18- Beti hii nasimama, siwezi kuendeleya
Roho yangu yaniuma, Fatima akiumiya
Hiyo siku ya kiyama, tutakuja jioneya
Kafariki Bi Fatima leo tunamliliya

Shairi na: Juma S. Magambilwa (Juma Shia)