Jumuiya
ya Waislamu nchini Nigeria imelaani mauaji ya Waislamu wa Kishia
yaliyotekelezwa katika siku ya kimataifa ya Quds. Kwa mujibu wa ripoti
hiyo jumuiya hiyo imelaani mauaji hayo iliyoyataja kuwa ya kinyama.
Aidha jumuiya hiyo imeongeza kuwa, hakuna sababu yoyote ya kuhalalisha
mauaji hayo hasa kwa kuzingatia kuwa, Waislamu hao wa Kishia waliuawa
wakiwa wanaandamana kwa amani katika siku hiyo ya
kimataifa ya Quds. Jumuiya hiyo ya Waislamu wa Nigeria imesisitiza
kuwa, ni jukumu la serikali kutoa mwanya kwa wafuasi wa dini kutekeleza
matukufu yao bila kizuizi chochote. Hii ni katika hali ambayo Harakati
ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria, imeituhumu serikali ya Abuja kwa
kuandaa mpango wa kutekelezwa mauaji hayo ya mjini Zaria katika jimbo la
Kaduna. Tukio hilo lilitokea wakati Waislamu wa Kishia walipoungana na
Waislamu wengine duniani katika maandamano ya kimataifa ya siku ya Quds
mjini hapo ambapo polisi walianza kuwamiminia risasi waandamanaji na
kuua watu 33 akiwamo mtoto mmoja wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa
jamii ya Waislamu wa Kishia nchini humo. Aidha katika tukio hilo idadi
ya Waislamu wengine walijeruhiwa huku watoto wawili wa sheikh huyo
wakitekwa nyara na kupelekwa kusikojulikana, ambapo nao waliuawa muda
mchache baadaye. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Waislamu hao,
askari wa serikali walitoka mjini Abuja wakiandamana na magari ya
kijeshi mjini Zaria kwa lengo la kutekeleza hujuma hiyo.