Wakati Mwenyezi Mungu alipoteremsha maneno yake yasemayo: “Alif lam
Miym. Je, watu wanadhani wataachwa (wasitiwe katika misukosuko) kwa kuwa
wanasema: “Tumeamini” Basi ndio wasijaribiwe?” (Qur’an 29:1-2). Imam
Ali bin Abi Talib (a.s) anasema: Nilitambua ya kwamba fitina
haitotushukia wakati Mtume (s.a.w.w) akiwa pamoja nasi. Nikasema: “Ewe
Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, je wewe hukuniambia siku ya vita vya Uhud
wakati walipouawa Mshahidi miongoni mwa Waislamu, na mimi nikanyimwa
kuuawa Kishahidi, na nikaudhika kwa hilo (kutokuuawa Kishahidi).”
Ukaniambia: “Furahia, kwani kuuwa Kishahidi kuko nyuma yako.”
Aliniambia: “kwa hakika jambo hilo litatokea tu, basi itakuwaje
uvumilivu wako wakati huo? Nikasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu!
Jambo hili (kuuawa Kishahidi) si katika mambo yanayohitaji uvumilivu
(subira), bali ni katika mambo ya furaha na kushukuru.” Akasema: “Ewe
Ali! Kwa hakika watu watafitinishwa kwa mali zao baada yangu, na
watamsimanga Mwenyezi Mungu kutokana na imani zao na huku wakitarajia
Rehema zake na kujiaminisha dhidi ya adhabu yake, na watajihalalishia
aliyoyaharamisha ulevi kwa kuuita maji ya shayiri, na kitolewacho kwa
njia ya haramu kukiita zawadi, na riba kuitwa ni biashara.” Nikasema:
Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Ifikapo hali hiyo, niamiliane nao vipi!
Niamiliane nao kama waliotoka katika Uislamu au niamiliane nao kama
waasi? Alisema: “Amiliana nao kama waasi.”