Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa,
iwapo taifa la Iran litajikita katika kuimarisha uwezo wa ndani ya nchi, basi
Marekani na madola mengine makubwa hayawezi kuthubutu kufanya chochote dhidi ya
nchi hii. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumanne
mjini Tehran alipokutana na maelfu ya watu kutoka mkoa wa Ilam. Sambamba na
kutoa salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa kukumbuka kuzaliwa Imam Ali AS,
Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, kwa kutumiwa uwezo wa ndani ya nchi, Marekani
na madola mengine makubwa duniani kamwe hayataweza kulishinikiza taifa la Iran
kwa njia za kijeshi au zisizo za kijeshi. Ameongeza kuwa, madola makubwa
yafahamu kuwa taifa la Iran halitayapigia magoti kwani taifa hili liko hai na
vijana wake wako katika harakati ya mkondo sahihi. Kiongozi Muadhamu
amesema utekelezwaji sera za 'uchumi wa kimapambano' na kutegemea uwezo wa
ndani ya nchi ndio njia sahihi ya kutatua matatizo ya kiuchumi. Ayatullah
Khamenei amesema pale ubunifu na umahiri wa vijana unapotegemewa, ustawi
hupatikana. Ametoa mfano wa mafanikio ya kivitendo yaliyopatikana Iran kwa
kutegemea vijana na kutaja ustawi katika sekta za nyuklia, dawa, seli shina,
teknolojia ya nano na utengenezaji zana za kujihami. Ameendelea kusema kuwa vijana
wa Iran wanavutiwa na Uislamu, Qur'ani, umaanawi na mapenzi kwa nchi.
Ayatullahil Udhma Khamenei amesema moja ya somo tunalopata kutoka kwa Imam Ali
AS ni kujitahidi katika kuleta saada ya kweli katika jamii kwa kutatua matatizo
ya kimaisha na kiuchumi ya wananchi. Amesema hilo linawezekana kwa kuwepo
mipango sahihi na kutumia uwezo mkubwa wa vijana nchini Iran. Chanzo cha habari
(irib)