Baraza la Mawaziri la Saudi Arabia limepitisha sheria mpya inayoitwa “Makosa ya kigaidi na kufadhili Ugaidi kifedha. Kwa mujibu wa sharia hiyo, kila kitendo kinachofanywa na mtu au kundi lolote, kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kwa lengo la kuvuruga amani na usalama, kinahesabiwa kuwa ni kosa la kigaidi.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, kupitishwa sheria ya makosa ya kigaidi na Serikali ya Saudi Arabia ni hatua iliyochukuliwa ili kuwakandamiza zaidi wapinzani wa utawala huo wa kiukoo.
Kwa karibu miaka mitatu sasa Saudi Arabia inakabiliwa na wimbi la malalamiko na maandamano dhidi ya Serikali japokuwa upinzani mkubwa umekuwa ukishuhudiwa zaidi katika maeneo ya Mashariki mwa Saudia, lakini pia maandamano ya kupinga Serikali yanafanyika mara kwa mara katika mji mkuu wa kisiasa Riyadh.
Suala hilo limeutia wasiwasi utawala wa Ukoo wa Al-Saud na katika miaka mitatu iliyopita utawala wa Saudia umekuwa ukitumia siasa za ukandamizaji na kuwatia mbaroni waandamanaji ili kukabiliana na Upinzani.
Siasa za kimabavu za nchi hiyo zimekosolewa sana na Wanaharakati wa haki za Binadamu katika la Mashariki ya kati na hata kimataifa. Hivi sasa inaonekana kuwa, kwa hatua hiyo ya kupasisha Sheria ya makosa ya Ugaidi Serikali ya Saudia inataka kuhalalisha ukandamizaji wa wapinzani na kuipatia polisi fursa zaidi ya kudhibiti hali ya ndani ya nchi.
Kwa kuathiriwa na wimbi la mwamko wa Kiislam lililoibuka katika nchi nyingi za Kiarabu tangu mwaka 2011, Wananchi wa Saudi Arabia walipata nguvu za kuanzisha Harakati dhidi ya utawala wa Kifalme wa Al-Saud unaotawala nchi hiyo kwa kurithishana kiukoo.
Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo hazina misingi ya Demokrasia, nchi ambayo haina Bunge na nyadhifa nyingi za Serikali na Uwaziri na Ugavana hushikwa na wana mfalme au ndugu wa karibu wa Ukoo wa Al-Saud.