ELIMU NI PAMBO LA MOYO.



Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alijali sana elimu na maarifa akabainisha nafasi ya elimu na jukumu lake katika maisha akasema:
“Kutafuta elimu ni faradhi kwa kila mwislam. Fuateni elimu toka kila sehemu mnayodhani mtaipata. Jifunzeni toka kwa wenyenayo hakika kujifunza kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni wema na kuitafuta ni ibada, kujikumbusha elimu hiyo ni Tasbihi na kuituimia ni Jihadi, kumfunza yule asiyejua ni Sadaka na kuieneza kwa wahusika ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa sababu elimu ndio alama ya halali na haramu, na minara ya watu wa peponi na ndio mfariji wakati wa upweke na rafiki wakati wa ugeni na upweke, na ndio msemeshaji wakati wa siri na upekee. Ni alama ijulishayo mambo ya siri nay a kudhuru, ni silaha dhidi ya maadui, na ni pambo kwa vipenzi.
Mwenyezi Mungu huwainua watu kupitia elimu, hivyo huwafanya viongozi bora ambao athari zao hunufaisha na vitendo vyao hufuatwa, mawazo yao utegemewa huku Malaika wakipenda urafiki wao, huwapangusa kwa mbawa zao na huwabariki katika Swala zao. Kila kibichi na kikavu huwaombea msamaha. Pia viumbe vya baharini na nchi kavu, kuanzia vidogo hadi vikubwa navyo huwaombea msamaha.
Hakika elimu ni uhai wa moyo dhidi ya Ujinga na ni nuru ya macho dhidi ya kiza na ni nguvu ya mwili dhidi ya Udhaifu. Humfikisha mja nafasi ya wenye heri na vikao vya watu wema na daraja la juu hapa duniani na huko Akhera. Kuitaja tu huwa sawa na kufunga, na kuisoma ni sawa na kusali Swala za usiku. Kupitia elimu Mola hutiiwa na undugu huunganishwa na haramu na halali hujulikana. Elimu huwa mbele ya vitendo na vitendo hufuata elimu. Mwenyezi Mungu huwapa watu wema na huwanyima waovu, hivyo ni jambo zuri sana kwa yule ambaye hajanyimwa na Mwenyezi Mungu fungu lolote la elimu. Sifa ya mwenye akili ni kumvumilia asiyejua na kumsamehe aliyemdhulumu, kumnyenyekea aliye chini yake na kushindana katika kutafuta wema dhidi ya yule aliye juu yake.
Anapotaka kuzungumza, kwanza hufikiria hivyo kama ni la heri huzungumza na kufaidika, na kama ni la shari hunyamaza na kusalimika. Iwapo utamfika mtihani hushikamana na Mwenyezi Mungu na huzuia mkono na ulimi wake. Aonapo jambo bora hulichangamkia na hapo aibu haimzuii wala tama haimpeleki pupa. Basi hizo ndio sifa za mtu mwenye akili.
Sifa ya mjinga ni kumdhulumu anayechanganyikana naye, kumdhulumu aliye chini yake, kumfanyia kiburi aliye juu yake. Huongea bila kufikiria, na akiongea hutenda dhambi na akinyamaza husahau. Iwapo utamfika mtihani basi huuendea pupa na kumcharua. Huwa mzito aonapo jambo la heri huku akijitenga nalo, hana hofu dhidi ya dhambi zake za mwanzo wala hatetemeki dhidi ya umri wake uliyobaki na dhambi alizonazo. Huwa mzito na mwenye kuchelewa dhidi ya jambo la heri. Hasikitikii heri yoyote iliyompita au aliyoipoteza. Hizo ni sifa za mjinga ambazo akili imenyimwa.

Ameipokea ndani ya kitabu Maniyyatul-Murid kutoka kwa Imam Ridhaa (a.s) kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w). Rejea hadithi hii kwa urefu ndani ya kitabu Taliful-Uqul.