FALSAFA YA HIJJA

Mwenyezi Mungu anasema:


“Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kwa watu siku ya Hijja kubwa kwamba Mwenyezi Mungu yu mbali na washirikina na (pia) Mtume wake (yu mbali nao) Basi kama mkitubu ndivyo kheri kwenu, na kama mkikataa basi jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu. Na wapashe khabari waliokufuru kwa adhabu iumizayo.”

(Qur’an: 9:3)

Hijja ni miongoni mwa ibada kubwa ya faradhi ya kidini, ni jumia ya ibada ambazo amali zake hasa zimekusudiwa kurekebisha mwenendo wa Kisiasana Kijamii na mataifa ya Kiislamu na kuunda jamii moja ya pekee ya kiislamu iliyojikomboa kutoka katika utawala wa kishirikina na kinafiki. Katika Hijja tu ndipo Mwenyezi Mungu anapowajulisha waja wake mandhar ya umoja wa Umma wa Kiislamu na kujibari (kujitenga) kwao na washirikina kwa njia ya kimantik. Hatua ya kwanza ya Hijja ni kuvaa Ihraamu na maana yake ni, kujiharamisha na kila kitu cha ubinafsi ili mtu aliyepotea aweze kujitambua mwenyewe.


Na anapojitambua nafsi yake, huitufu kaaba ya Mwenyezi Mungu ambayo ni nyumba ya Umma, na katika kuizunguka kwake, huungana na jamii zote za Kiislamu na kuwa wa moja baada ya kuungana katika umoja huo ambao ni miongoni mwa misingi muhimu ya falsafa ya Hijja, mahujaji huelekea kwenye jangwa la A’rafaat katika sura moja wakionyesha nguvu moja ya umoja wa Kiislamu, na nguvu moja ya kupambana na ulimwengu wa shiriki.


Wakati huu mahujaji hukusanyika katika Mash’ar ambapo hukusanya mawe ambayo inawabidi wayatumie kuwapiga mashetani katika siku ya Idd. Katika siku ya Idd, mahujaji huzirushia mawe jamarati ambazo ni alama za nguvu za kishirikina. Kitendo hicho ni alama na ni kujibari (kujitenga) mbali kabisa na washirikina ili wakome kabisa kuingilia maisha ya jamii iliyoungana ya Kiislamu. Kwa hiyo, hii falsafa tukufu ya Hijja inaeleweka vizuri katika Ayah hii ambapo Mwenyezi Mungu ameifanya nyumba yake mwenyewe kuwa ni nyumba yenye kuita kupambana na kusimama na kwa ajili ya ukombozi na Uhuru.