MAELEZO JUU YA DUA AL-IFTITAH:

Dua al-Iftitah ilifundishwa na Imam wetu wa kumi na mbili (A.S) kwa ajili ya Mashia kusoma kila usiku wa mwezi wa Ramadhani. Dua hii ni bora sana kwa ajili ya kujenga mwelekeo mzuri wa mwanadamu kwa Mola wake kwa vile inazungumzia vipengele vingi vya udhaifu wa binadamu na neema za Allah. Dua hii inaweza kugawanyika sehemu mbili:

Uhusiano wa binadamu na Mwenyezi Mungu.

Viongozi wa ki-Ungu watakatifu.

Sehemu ya kwanza ya Dua hii inaelezea sifa mbalimbali za Mwenyezi Mungu, na inadhihirisha hali ya huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu juu ya mwanadamu. Sehemu hii ya Dua inaweza kugawanyika zaidi katika vifungu vifuatavyo:

KUMTUKUZA MWENYEZI MUNGU: Kama ilivyo taratibu ya Dua, Dua hii ya al-Iftitah inaanza na kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Hii sio kwa sababu kwamba Mwenyezi Mungu anahitaji kusifiwa kabla ya yeye kujibu Dua zetu, bali ni kumkumbusha mwombaji juu ya Mweza wa yote anayeongea naye, na hatimaye kuweka hofu juu ya Allah katika nyoyo ambayo mara nyingi zinakuwa hazizingatii.
Uanzaji wa Dua hii unamuweka muombaji katikati ya matumaini na hofu, mtazamo bora wakati unapoomba. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa huruma, lakini pia ni mkali wa kuadhibu. Binadamu wasiwe wenye kukata tamaa, wala wasijiamini sana bali wadumu katika njia yake.

MSISITIZO JUU YA UPWEKE (TAWHIID) WA ALLAH: Mwenyezi Mungu hana mshirika wala mtoto, na anayo mamlaka kamili na udhibiti usiogawanyika juu ya viumbe. Wakazi wa angani na mbiguni wanamtegemea yeye. Hii ni kuimarisha utegemeaji wa muombaji juu ya Mwenyezi Mungu, kwani hakuna mwengine tena anayeweza kumgeukia.

UKARIMU WA MWENYEZI MUNGU: Hazina ya Mwenyezi Mungu hazifilisiki wala haziishi, na wakati wote zinatolewa kwa ukarimu juu ya viumbe wake. Shida za binadamu ni nyingi mno, na kwa kuuwacha wazi mlango wa Dua, Mwenyezi Mungu amewapa ufunguo wa kwenye hazina zake. Milango yake wakati wote iko wazi, na hakuna muombi yoyote kwake yanayokataliwa bila ya majibu fulani.
Lakini mara nyingi mwanadamu ni mtovu wa shukurani, ana wakati wote ni mlafi. Anategemea kwamba Dua zake siku zote zitajibiwa mara moja. Wakati kuridhika kama huko hakupatikani, yeye anageuka, badala ya kujikumbusha yeye mwenyewe juu ya neema zote anazozifaidi.

MAHUSIANO KATI YA ALLAH NA MWANADAMU: Ni uhusiano wa ajabu kweli kweli! Ingawa ni mwanadamu anayemhitaji Allah, na anapaswa kujitahidi kumuelekea yeye; ni Mwenyezi Mungu anayemualika na kumhimiza yeye kuja, ambaye anaonyesha upendo na huruma na anaendelea kumpendelea kwa njia nyingi. Kama anavyosema Imam wa nne katika Dua Abu Hamza Shimali: "Shukurani zimwendee Allah ambaye huniitikia mimi pale ninapomwita, ingawa mimi ninasitasita pale anaponiita, na sifa ni kwa juu yake Allah ambaye hunipa mimi wakati ninapomuomba, ingawa mimi ni bakhili pale anaponiomba." Hii inafaa kuitafakari kwa wale wanaomdhania Mwenyezi Mungu kwamba ni bwana wa kidhalimu anayeweka sheria juu ya wanadamu.
Sehemu hii ya Dua ni somo bora sana katika mtazamo wa Kiislam wa sifa za Mwenyezi Mungu. Mola wa Uislam ni mwenye upendo, Mwenyezi Mungu ni mwenye huruma anayewatendea wanadamu kwa ubora zaidi kuliko wanavyostahili. Msingi wa uhusiano kati ya Mwenyezi Mungu na mwanadamu ni upendo wa Muumba juu ya viumbe wake. Ni juu ya mwanadamu kuupekua moyo wake kwa ajili ya mwitiko wa kutendeana.

Sehemu ya pili ya Dua hii inamtakia rehema na amani Mtume Mohammad (s.a.w.w) na Ma'asuumin wote, na halafu inazungumzia jukumu la Imam wa kumi na mbili (A.S).

KUMSWALIA MTUME MOHAMMAD S.A.W.W (SALAWAT): Baada ya imani juu ya Mwenyezi Mungu, sehemu muhimu ya dini inayofuata ni imani juu ya wale aliowatuma. Hivyo baada ya kukiri Ukuu na Upole wa Muumba, Dua hii inatufundisha sisi kuwakiri wale viongozi wa Ki-Ungu watukufu kama viongozi wetu kuelekea kwa Allah (s.w.t) Rehema na amani zinatumwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kama ishara ya mapenzi na shukurani kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na kutambua kwamba yeye ni binadamu na anahitaji huruma na neema kutoka kwa Allah. Inaimarisha vilevile ukumbusho kwa Mtume (s.a.w.w) na msukumo wa kuifuata njia yake.

REHEMA NA AMANI JUU YA MA'SUMIIN: Baada ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) warithi waandamizi wake wanakumbukwa na kuombewa. Hawa ndio viongozi halisi wa Umma wa Kiislam ambao waliteuliwa na Mwenyezi Mungu. Imani juu yao, na upendo kwao ni sehemu muhimu ya imani ya Kishia.

JUKUMU LA IMAM WA KUMI NA MBILI (A.S): Katika kila zama Mwenyezi Mungu huwa anaye mwakilishi wake ambaye anamwongoza viumbe wake kwenye kusimamisha haki na uadilifu katika ardhi. Huyo Imam wa kumi na mbili ndiye kiongozi wa zama zetu hizi, amabaye atakuja kudhihiri na dini ya Mwanyezi Mungu itashinda (dini zote) duniani.

Sehemu ya mwisho ya Dua al-Iftitah inazungumzia kuhusu kuja kwake kuwaandaa waumini juu ya kusimama kwa utawa wa Allah unaotarajiwa juu ya ardhi. Kuomba msaada na ushindi kwa ajili ya Imam wa kumi na mbili (Imam Mahd) kutukumbusha sisi kwamba tunamngojea yeye, na tunahitaji kujiandaa kwa ajili ya kuja kwake. Tunakuwa tunatambua wajibu wetu katika wakati wa kughibu (kufichika) kwake, na umuhimu wa kujifundisha sisi wenyewe kama wasaidizi wake. Tunaomba kwa ajili ya ndoto ya mwisho ya Muislam, dini ya Mwenyezi Mungu inapata umuhimu mkubwa, na ukafiri na unafiki vinadhalilishwa.

Dua al-Iftitah inatukumbusha sisi kwamba imani na vitendo vyote ni muhimu na vya lazima ili kuwa muumini halisi na wa kweli. Imani juu ya Mwenyezi Mungu inafungamana na kuufanyia kazi ujumbe wake uliokuja na Mtume wake, na kusimamisha dini yake duniani. Wakati ambapo hilo linaweza kufanyika tu kupitia kwa Imam, sisi tunapaswa kufanya kazi na kuomba kwa ajili ya kudhihiri kwake. Wanadamu wanaweza kufaidi uadilifu na amani halisi, na kutimizwa kwa haja zao, chini ya kiongozi huyo Mtukufu.

Dua al-Iftitah sio maombi tu kwa ajili ya shida na haja zetu, bali ni ufundishaji wa mizizi ya iman, na upangaji kwa ajili ya namna ya maisha. Inabakia kwetu sisi kuandaa jedwali la maisha yetu wakati tunaposoma Dua hii katika kila usiku wa Ramadhani.