HIZBULLAH: LEBANON HAITATAWALIWA NA SAUDIA.

Harakati ya Hizbullah imeonya kuwa Lebanon kamwe haitakuwa chini ya mamlaka ya Saudi Arabia licha ya kuwepo mashinikizo ya ufalme huo kwa maafisa wa Lebanon.
"Lebanon haitakuwa chini ya utawala wa Saudi au dola lingine lisilo Saudia", amesema Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah Sheikh Naim Qassem.
Alitoa kauli hiyo jana Ijumaa kufuatia hatua ya Saudi Arabia kukata msaada wa kijeshi wa dola bilioni nne. Saudia imekata msaada huo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Gibran Bassil kukataa kuomba msamaha baada ya kupinga muswada uliotayarishwa na ufalme huo dhidi ya Iran katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Aidha Saudia imeyawekea vikwazo mashirika manne ya Lebanon na watu watatu wanaodaiwa kuwa na mfungamano na Hizbullah. Wakuu wa Riyadh pia wamewataka Wasaudi waondoke Lebanon huku kukiwa na tetesi kuwa raia wengi wa Lebanon wanaofanya kazi Saudia watatimuliwa.
Sheikh Naim Qassim amesema Saudi ndiyo inayopaswa kuiomba Lebanon msamaha kwa hatua zake za uhasama. Amesema kwa muda mrefu sasa Saudia imekuwa ikitafuta kisingizio cha kuihujumu Lebanon na Hizbullah na sasa inatumia mwanya uliojitokeza.
Mawaziri kadhaa wa Lebanon wamesema nchi hiyo katu haitaiomba Saudia msamaha huku Waziri Mkuu, Tammam Salam akitoa wito kwa nchi hiyo kuungana kukabiliana na mashinikizo ya Saudia. Habari nyingine zinasema Saudia pia imekata misaada ya kijeshi kwa Lebanon baada ya mwanamfalme wa ukoo wa Aal Saud kuendelea kushikiliwa Lebanon baada ya kukamatwa akiwa na dawa za kulevya katika uwanja wa ndege wa Beirut mwezi Oktoba mwaka jana. Abdul-Mohsen al-Waleed Al Saud alipatikana na tani mbili za mihadarati aina ya amphetamine captagon.
Sababu nyingine ya hasira za Saudia ni ushindi wa wapignaji wa Hizbullah dhidi ya magaidi wanaopata himaya na misaada ya Saudia nchini Syria. 

SAUDIA, UTURUKI NDIO MUHIMILI MKUU WA ISIS.
Mshauri wa Rais wa Syria amesema kuwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh linaweza kuangamizwa haraka iwapo baadhi ya nchi za eneo hasa Uturuki na Saudi Arabia zitaacha kuliunga mkono kifedha na kisiasa kundi hilo la wakufurishaji.
Katika mahojiano na Televisheni ya RT, Bi. Bouthaina Shaaban amesema magaidi wanaopata himaya ya kigeni ni kizingiti kikuu katika kumaliza mgogoro nchini humo.
Mshauri huyo wa Rais Bashar al Assad pia amezikosoa nchi za Magharibi na hasa Marekani kwa kuunga mkono kisiasa kundi la ISIS.
Akigusia mazungumzo ya amani baina ya serikali ya Syria na kile kinachotajwa kuwa ni upinzani, amesema mazungumzo hayo hayajaweza kufanyika kwa sababu makundi ya upinzani yanaungwa mkono kifedha na nchi mbali mbali. Amesema upinzani nchini Syria ni upinzani pekee duniani ambao ni kibaraka wa madola ya kigeni dhidi ya nchi yao.
Buthaina Shaaban ameelezea matumaini yake kuwa usitishwaji vita nchini Syria unaoanza siku ya Jumamosi utafanikisha kufikiwa umoja wa kitaifa na kuongeza kuwa Wasyria wamepigana miaka mitano ili kuhakikisha nchi yao haigawanywi vipande vipande.
Katika kipindi cha karibu miaka mitano ya hujuma za magaidi Syria, takribani watu 470,000 wamepoteza maisha na mamilioni ya wengine kuachwa bila makazi.