Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Syria amesema kuwa, muungano wa kijeshi wa kimataifa unaoendesha mapambano dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh umeshindwa kulisambaratisha kundi hilo na badala yake umezidi kuliimarisha na kulipa nguvu. Khalid Khoja amesema kuwa, stratejia za muungano huo wa kijeshi wa kimataifa unaoongozwa na Marekani zimefeli kwani badala ya kuwaangamiza magaidi wa Daesh, zimezidi kuwapa nguvu magaidi hao. Kiongozi huyo wa muungano wa upinzani huko Syria amesema malengo ya siri ya Marekani katika mgogoro wa Syria na Iraq yamezidi kuwapa nguvu magaidi. Khalid Khoja amesema, Marekani inalegeza kamba makusudi kwenye mashambulizi yake dhidi ya Daesh ili mgogoro wa Syria na Iraq uendelee kubakia kwa muda mrefu kwa maslahi ya watawala wa Washington na waitifaki wao.