Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya hapa mjini Tehran amesema kuwa,
kukubali misingi ya dini, kutii msingi wa "Wilaya," maadili mema na
kuheshimu sheria, ni mambo muhimu anayotakiwa awe nayo rais ajaye wa
Iran. Ayatullah Khatami amesema kuwa, ikiwa rais atakayechaguliwa
nchini, atakuwa mwenye kukubaliana na misingi ya dini, utawala wa faqihi
na kufuata sheria, kamwe hatokubali nchi hii ikanyagwe na maadui na pia
hatolegeza misimamo mbele ya vitisho vya maadui. Ameitaja kazi ya
kumchagua rais wa baadaye wa Iran kuwa inahitaji kufanywa kwa umakini na
uangalifu mkubwa na kuongeza kuwa, ikiwa taifa la Iran litawachunguza
vizuri wagombea watakaoshiriki katika uchaguzi wa mwaka huu, bila ya
shaka yoyote litaweza kumpata mtu mwema zaidi na anayefaa zaidi
kuliongoza taifa hili. Aidha Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo
hapa mjini Tehran ameashiria njama za wakoloni na utawala haramu wa
Kizayuni, za kujaribu kuzuia ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi
wa rais wa mwezi Juni mwaka huu hapa nchini na kusisitiza kuwa,
mabeberu wa dunia wanakusudia kuharibu anga huru ya kufanyika uchaguzi
nchini Iran na hivyo kuchafua sura ya taifa hili kimataifa. Lakini
amesisitiza kuwa, njama hizo zitavunjwa na hamasa kubwa ya wananchi
katika uchaguzi wa tarehe 14 Juni mwaka huu. Kuhusiana na matukio
yanayoendelea huko Syria na jinai ya kuvunjia heshima haram ya sahaba wa
Mtume Muhammad (SAW) Hujri bin Adi (RA), Ayatullah Ahmad Khatami
amesema kuwa, hatua ya maulama wa Kisuni na Kishia duniani ya kulaani
kitendo hicho kiovu inaonyesha kuwa maulama hao wako macho dhidi ya
fitina za kimadhehebu na vitendo vyovyote vya kuzusha mizozo na
mifarakano katika safu za Waislamu. Kuhusiana na mashambulizi ya hivi
karibuni ya ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Syria amesema
kuwa, mashambulizi hayo yamefichua jinsi wapinzani wanaopigana dhidi ya
serikali ya Damascus walivyo wasaliti kutokana na kushirikiana kwao na
utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa na watu wa Syria. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/habari/iran/item/31757-rais-wa-iran-anapaswa-awe-na-maadili-mema-na-mtiifu-kwa-allah