ITIKADI INAYOHUSU UIMAMU KWA SHIA NA SUNNI

Bismillah Rahmanr Rahiim
Makusudio ya Uimamu katika mlango huu ni ule Uimamu mkuu kwa ajili ya Waislamu, yaani nakusudia Ukhalifa, utawala, kuongoza na kusimamia. Kwa kulinganisha baina ya Madhehebu ya Kisunni na ya Kishia Imamiyyah, basi hapana budi kwanza nitoe misingi ya Uimamu kwa pande zote mbili ili imbainikie msomaji na mwenye kuchunguza ni ipi misingi na mafunzo ambayo kila upande unayategemea, na pia afahamu kukinaika kwangu ambako kulinilazimisha kukubali kugeuka na kuacha vile nilivyokuwa hapo kabla. Uimamu kwa Mashia ni msingi katika miongoni mwa misingi ya dini kutokana na umuhimu mkubwa ulionao na ni daraja tukufu katika kuongoza Umma bora uliotolewa kwa watu. Pia uongozi huo unazo sifa kadhaa na mambo maalumu ya kipekee yanayouhusu nami ninataja baadhi yake tu. Miongoni mwa sifa hizo ni: Elimu, Ushujaa, Upole, Utakatifu, Kutosheka, Uchamungu, Kuupa nyongo dunia na wema n.k. Mashia wanaitikadi kwamba Uimamu ni cheo akitoacho Mwenyezi Mungu kumpa aliyemteua miongoni mwa waja wake wema ili aweze mtu huyu kusimamia suala nyeti ambalo ni kuongoza ulimwengu baada ya Mtume (s.a.w.w), na kwa msingi huu Imam Ali bin Abi Talib (a.s) alikuwa ndiye kiongozi wa Waislamu kwa kuchaguliwa na Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu alimpelekea wahyi Mtume wake ili amtawalishe (Ali) kuwa kiongozi (khalifa) wa watu. Bila shaka Mtume wa Mwenyezi Mungu alimtawalisha na akaujulisha Umma baada ya hija ya kuaga katika bonde la Khum, Waislamu nao walikula kiapo cha utii. Hivi ndivyo wasemavyo Mashia. Ama Masunni wao pia wanasema kuwa ni lazima kuwepo Uimamu ili kuuongoza Umma, lakini wao wanaupa Umma haki ya kumchagua kiongozi wake, na ndiyo maana Abubakar bin Abi Quhafah alipokuwa Imam wa Waislamu kwa kuchaguliwa na Waislamu wenyewe baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ambavyo (kama wasemavyo) alilinyamazia jambo la Ukhalifa na wala hakuubainisha Umma kitu chochote kuhusiana na suala hilo na akaliacha liwe ni mashauriano baina ya watu.

UKWELI UKO WAPI NDUGU ZANGU?
Mtu anayechunguza, akizingatia kauli za pande mbili na akafikiri kwa makini juu ya hoja za makundi haya mawili bila ya chuki basi huenda akaukaribia ukweli bila shaka yoyote. Mimi mwenyewe niliufikia ukweli kwa njia hii ifuatayo:

1. Uimam ndani ya Qur'an Tukufu:

Mwenyezi Mungu Anasema: "Na kumbukeni Ibrahim alipofanyiwa mtihani na Mola wake kwa amri nyingi naye akazitimiza, (Mwenyezi Mungu) akamwambia hakika mimi nitakufanya uwe kiongozi wa watu wote. Ibrahim akasema: na miongoni mwa kizazi changu (wafanye wawe viongozi) akasema, ahadi yangu haiwafikii madhalimu". (Qur'an, 2:124). Ndani ya aya hii Tukufu, Mwenyezi Mungu anabainisha kwamba Uimam ni cheo kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, na humpa cheo hicho yule amtakaye miongoni mwa waja wake pale aliposema: "Nitakufanya kiongozi (Imam) wa watu". Kama aya ilivyobainisha kwamba Uimam ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu hawaipati isipokuwa waja wema ambao Mwenyezi Mungu amewateua kwa ajili ya lengo hili, na hii hutokana na kuwakanusha kwake madhalimu ambao hawasitahiki ahadi hiyo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwenyezi Mungu amesema: "Na tumewafanya kuwa Maimam wanaoongoza kwa amri yetu na tukawapelekea wahyi wa kufanya mambo ya kheri na kusimamisha Sala na kutoa Zaka na wakawa ni wenye kutunyenyekea". (Qur'an, 21:73). Pia amesema Mwenyezi Mungu: "Na tukawafanya miongoni mwao kuwa Maimam wanaoongoza kwa amri yetu, (hii ni kwa kuwa) walisubiri na walikuwa wakiziamini aya zetu". (Qur'an, 32:24). Vile vile amesema: "Na tunataka kuwafanyia ihsani wale waliodhoofishwa katika ardhi na kuwafanya kuwa Maimam na kuwafanya kuwa warithi". (Qur'an, 28:5). Huenda baadhi ya watu wakafikiria kwamba aya hizi zilizotajwa zinajulisha kwamba Uimam uliokusudiwa hapa ni Utume na Unabii, (kufikiri) hivyo ni kosa katika maana ya ujumla ya Uimam, kwani kila Mtume ni Nabii na ni Imam, na siyo kila Imam ni Mtume au Nabii!!. Na kwa lengo hili basi Mwenyezi Mungu ameweka wazi ndani ya kitabu chake kitukufu kwamba, waja wake wema inawezekana kwao kumuomba yeye Mwenyezi Mungu cheo hiki kitukufu ili wasimamie jukumu la kuwaongoza watu, ili wapate malipo makubwa.Mwenyezi Mungu amesema: "Na wale ambao hawashuhudii ushuhuda wa uongo na wanapopita penye upuuzi hupita kwa heshima, na wale ambao wanapokumbushwa aya za Mola wao hawaziangukii kwa uziwi na upofu, na wale wanaosema, Mola wetu tupe miongoni mwa wake zetu na watoto wetu yaburudishayo macho yetu na utujaalie kuwa Maimam wa wachamungu". (Qur'an, 25:72-74). Kama ambavyo Qur'an vile vile imetumia tamko la Imamah ili kujulisha viongozi na watawala madhalimu ambao wanawapoteza wafuasi na raia wao na kuwaelekeza kwenye maovu na mateso duniani na akhera. Imekuja ndani ya Qur'an simulizi juu ya Firauni na majeshi yake pale Mwenyezi Mungu aliposema: "Basi tukamtesa yeye na majeshi yake na tukawatumbukiza baharini basi angalia ulikuwaje mwisho wao, na tuliwafanya kuwa Maimam waitao kwenye moto na siku ya Qiyama hawatasalimishwa, na tukawafuatishia laana katika dunia hii na siku ya Qiyama watakuwa miongoni mwa wenye hali mbaya mno". (Qur'an, 28:40-42). Na kwa msingi huu, kauli ya Mashia iko karibu na kile ambacho Qur'an imekithibitisha, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameweka wazi kwa maelezo ambayo hayatoi nafasi yoyote ya mashaka, kwani Uimam ni cheo kitokacho kwa Mwenyezi Mungu na hukiweka pale atakapo. Na cheo hicho ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo amekataa wasiipate madhalimu, na kwa kuwa mtu asiyekuwa Ali miongoni mwa Maswahaba wa Mtume bila shaka yoyote kuna kipindi kabla ya Uislam alifanya ushirikina. Hapana shaka kwa ajili hiyo wanakuwa miongoni mwa madhalimu, hivyo hawasitahiki ahadi ya Mwenyezi Mungu ya Uimam na Ukhalifa, na hapo inabakia kauli ya Mashia ya kwamba Imam Ali bin Abi Talib peke yake ndiye alistahiki ahadi ya Mwenyezi Mungu ya Uimam (Ukhalifa) kuliko Maswahaba wengine, kwani yeye Ali (a.s) hakuabudia sanamu, bali Mwenyezi Mungu ameutukuza uso wake kinyume cha Maswahaba, kwani Ali (a.s) hakupata kusujudia sanamu. Na iwapo patasemwa kuwa Uislam unafuta yaliyotendeka hapo kabla, sisi tutasema ndiyo lakini bado inabakia tofauti kubwa kati ya yule aliyekuwa mshirikina kisha akatubu na yule aliyekuwa mtakatifu na hakumtambua Mola mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu.

2.Uimam katika Sunna ya Mtume:

Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema kauli nyingi kuhusu Uimam, kauli ambazo zimenakiliwa na Mashia na Masunni ndani ya vitabu vyao na Musnad zao, kuna wakati alizungumza juu ya Uimam kwa tamko la " Al-Imamah" na wakati mwingine kwa tamko la "Al-Khilafah" na kuna wakati alitumia tamko la "Al-Wilayah" au "Al-Imarah". Kuhusu tamko la Al-Imamah imekuja kauli ya Mtume kama ifuatavyo: "Maimam wenu bora ni wale munaowapenda nao wanakupendeni, na mnaowaombea naowanakuombeeni, na Maimam wenu waovu ni wale munaowachukia nao wanakuchukieni na munawalaani nao wanakulaanini". Wakasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu je, tuwapige upanga?". Mtume akasema: "Hapana maadam wanasali sala miongoni mwenu".

Taz: Sahihi Muslim J. 6 uk. 24 Babu Khiyaril-Aimati wa Shirarihim.

Na amesema pia Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuwa: " Baada yangu watakuwepo Maimam ambao hawatafuata muongozo wangu na wala hawatafuata suna yangu, na watakuja simama miongoni mwao watu ambao nyoyo zao ni nyoyo za shetani zikiwa  ndani ya miili ya watu".

Taz: Sahihi Muslim J. 6 uk. 20 Babul-Amri Biluzumil-Jamaah Inda Dhuhuril-Fitan.

Na kuhusu tamko la "Al-Khilafah" imekuja kauli yake Mtume Muhammad (s.a.w.w) kama ifuatavyo: "Dini haitaacha kuwa imara mpaka kiama kitakaposimama hadi wakufikieni Makhalifa kumi na mbili na wote watatokana na Makuraishi". Na imepokewa kutoka kwa Jabir bin Samurah amesema: "Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: "Uislam hautaacha kuwa na nguvu kupitia kwa Maimam kumi na mbili, kisha alisema neno ambalo sikulifahamu, nikamwambia baba yangu, Mtume amesemaje? Akasema wote ni kutokana na Makuraishi". Na imekuja kauli ya Mtume kuhusu tamko la "Al-Imamah" kama ifuatavyo: "Itakuwepo aina fulani ya Maamiri ambao mtawatambua na mtawapinga mwenye kuwatambua amejitakasa na mwenye kuwapinga amesalimika, lakini yeyote atakayewaridhia na kuwafuata.... Wakasema Je, tuwapige akasema: hapana maadam wanasali".

Taz: Sahih Muslim J. 6 uk. 23 Babu Wujubil-Inkari Alal-Umarai.

Na amesema tena Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuhusu tamko la "Al-Imarah". "Watakuwepo Maamiri kumi na wawili wote ni Makuraishi".

Taz: Sahih Bukhar J. 8 uk. 127.

 Na imekuja kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) akiwatahadharisha Sahaba wake: "Mtaupupia Uamiri na kutakuwa na majuto siku ya Qiyama, mwenye kunyonya ameneemeka, na aliyeacha kunyonya ameathirika".

Taz: Sahih Bukhari J. 8 uk. 106

Kama ambavyo Mtume Muhammad (s.a.w.w) amezungumza tena kwa tamko la "Wilayah". "Mambo ya watu hayataacha kuwa na mafanikio maadamu watakuwa wanatawaliwa na watu kumi na wawili wote ni Maquraishi".

Taz: Sahih Muslim J. 6 uk. 3

Na baada ya maelezo haya mafupi juu ya maf-humu ya Al-Imamah na Al-Khilafah ambayo nimeitoa ndani ya Qur'an na Sunna sahihi ya Mtume bila ya tafsiri wala taawili, bali nimetegemea vitabu vya Kisunni bila ya (kutegemea) vitabu visivyokuwa vyao miongoni mwa (vitabu vya) Mashia, kwani jambo hili (yaani la Ukhalifa wa Makhalifa kumi na wawili na wote ni Makuraishi) kwa Masunni ni katika mambo yanayokubalika na wala hakuna utata juu yake, wala hawatofautiani wawili kuhusu nalo na hiyo ni pamoja na kufahamu kwamba baadhi ya wanachuoni wa Kisunni wanabainisha kwamba Mtume (s.a.w.w) amesema: "Kutakuwepo na Makhalifa kumi na wawili wote ni katika bani Hashim".

Taz: Yanabiul-Mawaddah J. 3 uk. 104

Na imepokewa kutoka kwa Shaabi, naye kutoka kwa Mas-Rooq, amesema: "Wakati fulani sisis tulikuwa kwa ibn Mas-ud tunaaridhi Misahafu yetu kwake basi kijana fulani akamwambia, hivi Mtume wenu alikuusieni kuwa watakuwepo Makhalifa wangapi baada yake, akasema: hakika wewe ni mdogo kwa umri na jambo hili hajaniuliza mtu kabla yako, ni kweli alituusia Mtume wetu (s.a.w.w) kwamba baada yake watakuwepo Makhalifa kumi na wawili kwa idadi ya Mabwana wa kizazi cha Israeli......

Taz: Yanabiul-Mawaddaah J. 3 uk. 105.

Na baada ya haya, hebu basi na tuangalie juu ya kusihi kwa madai ya kila upande kwa kuyapitia maandiko yaliyowazi kama ambavyo tutajadili taawili ya kila moja ya pande mbili hizi kuhusu suala hili muhimu ambalo limewagawa Waislam tangu siku aliyofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) mpaka leo hii, na kutokana na kutengana huko kukawa kumetokea Madh-hebu mengi na makundi mengi na mafundisho mengi ya kifikra na maneno, wakati hapo zamani Waislam walikuwa ni umma mmoja. Basi kila tofauti iliyotolewa baina ya Waislam sawa sawa iwe ni ya Fiqhi au tafsiri ya Qur'an au katika kuifahamu Sunna tukufu ya Mtume, basi asili yake na sababu yake ni Ukhalifa. Nikitu gani basi kitakujulisha huo Ukhalifa ni jambo gani? Ukhalifa ambao baada tu ya Saqifah limekuwa ni jambo ambalo kwa sababu yake hadithi sahihi na aya zilizo wazi zilikuwa zikipingwa na (badala yake) kutengenezwa hadithi nyingine zisitokuwa na msingi ndani ya Sunna ya Mtume ili tu kuthibitisha na kuupa usahihi Ukhalifa ulio patikana ndani ya Saqifa?. Jambo hili linanikumbusha namna ilivyo Israel na hali halisi iliyopo, nayo ni kuwa, Wafalme na Maraisi wa (Mataifa ya) Waarabu walikutana na wakaafikiana kuwa wasiitambue Israel na wala wasifanye uhusiano nao wala amani, kwa maana kwamba kilichochukuliwa kwa nguvu kirudishwe ila kwa nguvu. Baada ya miaka michache (Waarabu) wakakutana upya, mara hii kwa ajili ya kuvunja uhusiano wao na Misri ambayo imetambu kuwepo kwa Wazayoni, na baada ya miaka michache wakarejesha uhusiano wao na Misri na hawakuilaani kuhusu uhusiano wake na Israel pamoja na kuwa Israel haikubaliani na haki za Taifa la Wapalestina na haikubadilisha chochote kutoka kwenye msimamo wake, bali ilizidisha kero zake na ikaongeza kuwakandamiza wananchi wa Palestina.

Basi historia inajirudia yenyewe kwani Waarabu wamezoea kukubaliana na matokeo yalivyo.