WABUNGE IRAN WATAKA MAREKANI ILIPE FIDIA.




Wabunge nchini Iran wamepitisha muswada wa sheria ya kuishurutisha serikali ya Iran kuitaka Marekani iilipe fidia Jamhuri ya Kiislamu kutokana na jinai za Washignton dhidi ya nchi hii na raia wake.
Muswada huo umepitishwa katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, siku ya Jumanne ambapo wabunge 174 wameuunga mkono huku wengine saba wakiupinga na wane wakijizua kupiga kura.
Muswada huo ukiidhinishwa kuwa sheria, serikali ya Iran itawajibika kuitaka Marekani ilipe fidia kutokana na hatua ya mahakama za nchi hiyo kupora mali za Iran kwa visingizio mbali mbali.
Ikumbukwe kuwa mwezi uliopita wa Aprili, Mahakama ya Rufaa ya Marekani, ilitoa hukumu ya kuchukua udhibiti wa dola bilioni mbili za Iran zilizo katika benki za nchi hiyo kwa akijili ya kulipa fidia familia za wanajeshi wa Marekani waliouawa mwaka 1983 mjini Beirtu kufuatia mlipuko wa bomu ambao Marekani inadai Iran ilihusika nao. Iran imekanusha vikali kuhusika na malipuko huo na kusema fedha zilizochukuliwa na mahakama hiyo ya Marekani ni mali ya Benki Kuu ya Iran.
Mbunge Hamid Rasa'ei aliwasilisha muswada huo na kusema Iran inapaswa kuchukua udhibiti wa meli za Marekani zinazopita katika Lango la Hormuz katika Ghuba ya Uajemi.